SAMANTHA CAMERON: Kutoka mke wa Waziri Mkuu hadi mbunifu mavazi

NI Mfanyabiashara wa Uingereza na mke wa David Cameron, Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza, Samantha Cameron anazindua lebo mpya ya mitindo inayoitwa ‘Cefinn.’

Jina la chapa hiyo inatokana na majina ya watoto wake Elwen, Florence, Ivan na Nancy. Picha za kwanza za mkusanyiko wa mavazi hayo ambayo yatazinduliwa wakati wa majira ya kiangazi mwakani, kwa upekee wa aina yake unaweza kuyaona kwenye Jarida la Vogue katika chapisho lake la mwezi Januari, ambalo litaanza kupatikana kwenye stendi za magazeti kuanzia Desemba 5, mwaka huu.

Mavazi hayo yanatarajiwa kuuzwa kati ya Paundi za Uingereza 100 na 300, yatakuwa ya aina 40 na yataanza kupatikana mapema mwakani katika maduka ya Net-A-Porter, Selfridges na tovuti yake yenyewe www. cefinn.com. “Nahisi kuna chapa nyingi za Marekani na Ufarasna nje huko zinazofaa na kuendana na ubunifu wa kisasa, kulingana na bei na mtindo sahihi, lakini hakuna chapa nyingi za Uingereza zinazojaza nafasi hiyo,” Samantha analieleza Jarida la Vogue.

Samantha, ambaye ni Mkurugenzi wa zamani wa ubunifu wa Kampuni ya Smythson, ambako bado anafanya kazi ya ushauri alilieleza Jarida la Vogue kuwa ana msukumo wa kuanzisha lebo hiyo inayotokana na herufi za kwanza za watoto wake. Anabainisha kuwa ingawa alipinga msukumo wa kubuni mavazi yake kwa akili zake mwenyewe kwa kile alichoeleza kwamba ‘itakuwa haina maana’ na kuongeza kuwa, “ nimetumia muda mwingi kuwajaza mawazo marafiki zangu.”

Hivi sasa mwanamama huyo ni Balozi wa Baraza la Mitindo la Uingereza na mara kwa mara unaweza kumuona akiwa amevaa mavazi yenye lebo za Uingereza ikiwa ni pamoja na Roksanda, Christopher Kane na Erdem. Alisema atazindua mitindo yake mbalimbali ili ‘kubuni sare kwa wanawake wa mjini walio na shughuli nyingi” na kuongeza kuwa alihisi kuna pengo katika soko kwa ajili ya lebo za Uingereza ambazo zinatoa mavazi kwa ajili ya wanawake kuvaa mchana hadi usiku.

Samantha ni nani hasa

Samatha ni mtoto wa Sir Reginald Sheffield na Annabel Jones ambaye alizaliwa Aprili 18, 1971. Mwanamama huyu alibahatika kukulia kwenye eneo la shamba lenye ekari 300 lililokuwa Lincolnshire Kaskazini. Familia yake ilikuwa na muunganiko wa tabaka la makabaila. Alipewa mafunzo binafsi kwanza katika Shule ya St Helen na St Katharine, Oxfordshire, na kisha katika Chuo cha Marlborough, Wiltshire.

Baada ya kumaliza kozi ya msingi ya sanaa, msichana huyo kijana mwenye ari alijiunga na Chuo cha Bristol Polytechnic kwa ajili ya Shahada ya Sanaa. Alijipatia sifa kwa tabia ya uasi fulani, ingawa inaonekana vyombo vya habari navyo vimeweka chumvi. Mbunifu huyu anaelezwa kuwa na tatuu ya pomboo kwenye kifundo cha mguu. Wakati akiwa mwanafunzi alikutana na David Cameron akiwa na umri wa miaka 25 wakati huo.

Samantha alikuwa rafiki wa karibu na dada mdogo wa David, Clare na ingawa wawili hao walishawahi kukutana mara kadhaa, lakini mpaka wakiwa mapumziko mjini Tuscany mwaka 1992 wakati wa kumbukumbu ya ndoa ya wazazi wa David na Clare ndipo mahaba baina ya Samantha na David yalipochipuka. “Alikataa kwa muda… hakutaka kumwambia yoyote kuwa ana uhusiano na Tory,” aliwahi kukiri David.

Samantha aliwahi kuzungumza kwenye mahojiano ya televisheni mwaka 2010 kuwa, “ alikuwa tofauti na rafiki yangu yoyote niliyewahi kukutana naye kabla na kuongeza kuwa “Nilimuona akivutia (David). Alikuwa akinichekesha sana, mwenye mvuto na akili. Tulielewana siku ya kwanza.” Wenza hao walifunga ndoa miaka minne baadaye mwaka 1996, wakati huo akiwa ni Mkurugenzi wa Ubunifu wa Smythson, Kampuni kubwa ya vifaa katika mtaa wa Bond.

Mwaka 2002 mtoto wao wa kwanza Ivan alizaliwa. Lakini hali haikuwa nzuri. Ivan alipata mchanganyiko wa magonjwa ya kupooza ubongo na kifafa kikali. “Taarifa kama hizo zinakupata kama umegongwa na treni,” alisema David. “ Unashikwa na huzuni kwa muda kwa sababu unasononeka huku ukiwa katikati ya matumaini na uhalisia. Lakini unayapita juu yake kwa sababu kwetu ni mtoto wa kipekee.”

Waliendelea kupata watoto wengine wawili zaidi, Nancy, aliyezaliwa Januari 2004 na Arthur aliyezaliwa Februari 2006. Lakini bahati mbaya mwaka 2009, walimpoteza Ivan aliyefariki dunia akiwa amelazwa hospitali akipatiwa matibabu. Kwa pamoja wanandoa hao walifarijiana baada ya kupoteza mtoto wao na mwaka 2010. Kabla ya David kuanza kampeni walitangaza habari njema ya ujio wa mtoto wao wa nne.

“Tulitamani kupata mtoto mwingine wa kiume baada ya Ivan kufariki dunia,” anasema David. Mtoto wa kike alizaliwa mwezi mmoja mapema wakati familia ikiwa mapunzikoni Cornwall, Agosti 2010, ndio mtoto wa pili kuzaliwa wakati baba yake akiwa Waziri Mkuu katika kipindi cha miaka 150. “Tuliamka asubuhi tukafikiri ana uchungu, kwa hiyo tukafikiri tutafika hospitali kwa ajili ya kuangalia afya tu kawaida… lakini mambo yaliongezeka, kila kitu kilikwenda haraka haraka na mtoto alizaliwa,” alisema baba mwenye furaha.

Samantha anasema Nancy na Arthur walifurahi kupata mtoto mpya kwenye familia. Kazi na Siasa Kazi ya Samantha akiwa Smythson ilimuewezesha kupata Tuzo ya Jarida la Uingereza la Glamour ya Mbunifu Bora wa vifuasi (Best Accessory Designer) mwaka 2009. Alikuwa msemaji wa kampuni ya mavazi kutoka Taiwan ya Shiatzy Chen. Siku mbili baada ya mumewe kuwa Waziri Mkuu, Samantha alijiengua ukurugenzi na kubakiwa na jukumu la kuwa mshauri ndani ya Smythson, mara mbili kwa wiki.

Samantha pia alifanya kazi kama Balozi wa Baraza la Mitindo Uingereza na amechangia sana katika Wiki ya Mitindo London. Mwaka 2010, alitajwa katika orodha ya Jarida la Tatler ya watu 10 wanaovaa vizuri. Mwanamama huyu pia anajishughulisha na masuala ya hisani. Juni 2013 alichaguliwa kuwa patroni wa Kituo cha Hisani Uingereza kinachoitwa Vitalise. Amekuwa akijitolea pia katika taasisi isiyokuwa ya kiserikali ya Dress for Success, ambayo hutoa mavazi bure na ushauri kwa wanaokwenda kwenye usaili hasa wanawake wasiokuwa na kazi.

Desemba 11, mwaka jana ilitangazwa kuwa Samantha atakuwa mmoja wa watu maarufu 16 watakaoshiriki kwenye shughuli inayojulikana kama Great Sport Relief Bake Off, na kurushwa kwenye vyombo vya habari mwaka 2016 kama sehemu ya kukusanya harambee. Samantha ni Balozi wa taasisi ya hisani ya Save the Children.

Mwezi Machi 2013, baada ya kutembelea kambi ya wakimbizi ya Syria iliyopo Lebanon, alisema;“ kama mama, inatisha hadithi kutoka kwa watoto niliokutana nao, hakuna mtoto anapaswa kupitia walichopitia. Kila siku zinavyokwenda, watoto zaidi na wazazi wanauawa, watoto wengi zaidi wasiokuwa na hatia wanakufa.”