Nyota nyimbo za injili imezimika kama mshumaa

WIKI hii nyota ya muziki wa injili Afrika Kusini ilizimika ghafla na kusababisha mshtuko na majonzi kwa mashabiki wa muziki huo nchini humo na kimataifa, baada ya mwanamuziki Sfiso Ncwane kufariki alfajiri ya Jumatatu.

Usiku wa Jumapili, Sfiso alikimbizwa hospitalini na kutibiwa tatizo la figo, hakuna aliyetarajia kuwa mwanamuziki huyo angeweza kupoteza maisha.

Lakini baada ya kupigania uhai wake, asubuhi ya Jumatatu saa 3:30 madaktari walitangaza msanii huyo maarufu kwa wimbo Kulungile amefariki dunia.

Mke wa Sfiso, Ayanda alilazimika kubeba mzigo huo mzito na kuwataarifu watoto wao Ngcweti na Mawenza siku ya Jumatatu mchana, kuwa baba yao hawatamuona tena.

Kwa mshtuko na huzuni ya kumpoteza baba yao, watoto hao wawili wa kiume waliandika ujumbe uliogusa mioyo ya watu kwenye mitandao ya kijamii.

Mtoto mkubwa, Ngcweti aliandika: Baba asante kwa kila kitu ulichoifanyia familia yote, najua haukuwa na nia ya kutuacha. Matarajio yetu utalala mahali pema peponi na ninakuahidi nitafuata nyayo zako. Hatakuwepo baba anayetupenda kama wewe.”

Mtoto mdogo yeye aliandika: “Baba yangu shujaa. Tutakulindia mama siku zote.”

Muda mfupi baada ya kutangazwa kifo chake, watu wa kada mbalimbali walituma salamu za pole kwa familia ya msanii huyo akiwemo Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma. Zuma alisema:

“Kifo cha Bwana Ncwane ni hasara kubwa kwa nchi. Aligusa mioyo ya mamilioni ya watu. Alikuwa mmoja wa wasanii bora wa injili kuwepo hapa nchini na ameondoka akiwa kijana mdogo sana. Tumehuzunika sana. Roho yake ilale mahali pema peponi, alisema Rais wa Afrika Kusini.”

Sfiso ni tunda jema la Afrika Kusini, kijana wa miaka 37 aliyependwa na watu wa rika zote Afrika Kusini na mashabiki wa muziki wa injili.

Alimpenda Mungu, aliimba kwa mapenzi yake yote akisambaza injili kwa njia ya nyimbo.

Kijana huyu alizaliwa na kukulia kusini Jimbo la Kwazulu-Natal eneo linalojulikana kama Mthwalume Aprili 21, mwaka 1979. Kijana huyu alilelewa na shangazi yake tangu akiwa na wiki mbili, baada ya mama yake kumuacha.

Akiwa na umri mdogo, Sfiso alimpokea Yesu baada ya kipaji chake kugundulika katika kanisa moja.

Sfiso amekuwa na hatua kadhaa za mabadiliko baada ya mkewe Ayanda kumtambulisha kwa Mtumishi wa Mungu, Mchungaji Francis Anosike mwaka 2006.

Kijana huyo aliamua kutubu na kuokoka mwaka 2006. Maisha yake yalibadilika kuwa mazuri zaidi baada ya kufunga ndoa na patna wake wa siku nyingi na mama watoto wake, Ayanda.

Mungu aliwabariki watoto wawili, Ngcweti (9) na mdogo Umawenzokuhle (4).

Sfiso aliendelea kufanikiwa kuwa na ushuhuda kwa watu, kuwa kumtumainia Mungu kunalipa na aliwathibitishia watu hilo, kwa kuwa mwanamuziki wa injili mwenye maono nchini mwake.

Tabia yake ya unyenyekevu, tabia njema, kujiheshimu na kuheshimu wengine vilimwezesha kujijengea heshima na hadhi kwa mashabiki na wafuasi wake.

Pamoja na kutoka kwenye familia masikini, Sfiso aligundua kipaji alichopewa na Mungu yaani sauti nzuri ya kuimba. Alianza kuimba akiwa na umri wa miaka minane.

Akiwa na umri wa miaka 10 alianza kuimba nyimbo za injili. Wakati akipitia matatizo ya kiafya, ikiwa ni pamoja na kuzimia, kupigwa na radi na ugonjwa wa akili akiwa mvulana mdogo, hakusita wala kuacha kumtukuza Mungu kwa sauti yake nzuri.

Akiwa kwenye miaka 19 alianza kupiga kinanda, gitaa la besi na ngoma bila kupata mafunzo yoyote rasmi, ambavyo vilimwezesha kualikwa kutoa burudani katika makanisa, sherehe za harusi, hafla na misiba. Hatimaye, kuna mtu alimuona na alisaidia kufungua milango yake kwa kuimba kwa weledi. Kisha alirekodi albamu yake ya kwanza aliyoipa jina la Vulamasango, yenye maana ‘Fungua Milango.’

Kijana huyu alirekodi albamu yake ya kwanza kitaaluma chini ya kampuni ya Bula Music na kuzalishwa na Tshepo Ndzimande, ambaye ndiye amewafanyia kazi pia wasanii kama Lundi Tyamara, Kholeka na wengine.

Albamu hiyo ilitwa Makadunyiswe. Kazi hiyo ilimtambulisha vyema katika tasnia ya muziki wa injili. Mwaka uliofuata, alitoa albamu aliyoipa jina la Inombolo Yasezulwini aliowashirikisha wasanii nguli, Vuyo Mokoena na Zodwa Twecu, na albamu hiyo ilikuwa albamu bora iliyouza.

Mwaka 2003 alitoa albamu Umkhuleko na anaamini albamu hiyo alipewa na Mungu, kwani ilileta matumaini kwa maisha ya watu na iliuzwa kwa mamilioni na kubadilisha taifa. Ilikuwa albamu namba moja katika vituo vyote vya redio Afrika Kusini na ilimtambulisha vyema katika nchi jirani za Afrika na hatimaye kumfanya kuwa nyota wa nyimbo za injili. S’fiso alifuata kampuni ya CCP Records ambayo ni sehemu ya kampuni kubwa ya muziki EMI Records.

Akiwa juu kisanii, S’fiso alitoa albamu yake ya kwanza akiwa na EMI aliyoipa jina la “Baba Ngyavuma”.

Mwaka 2006 alithibitisha kuwa mwaka bora kwa S’fiso tangu alipopewa fursa ya kufanya kazi na Malkia wa Injili– Rebecca Malope, Winnie Mashaba, Sipho Makhabane na wengine.

Baadaye alitoa albamu kwa mfumo wa DVD na albamu yake ya mwisho na EMI ikiitwa Isiphephelo Sami. Kutokana na kupenda muziki, S’fiso alizindua kampuni yake binafsi ya muziki aliyoipa jina la Sfiso Ncwane Productions.

Albamu yake Baba Ngyavuma, ambayo ndani yake uko wimbo uliompatia tuzo unaoitwa Phakama Nkosi yeZulu. Hiyo ndio ilikuwa sadaka ya kwanza ya kampuni ya “Sfiso Ncwane Productions” ambayo iliuza zaidi ya albamu 70, 000.

Malengo yake ya muda mrefu kwa kampuni yake ikiwa ni kusaidia wasanii wanaochipukia na wenye vipaji kwa kuwasaidia kuzalisha na kuandika nyimbo.

Mwaka 2011 mwishoni, Sfiso alitoa wimbo uliotamba na kujipatia umaarufu ‘Kulungile Baba’, ndani ya miezi 16 ulitamba vilivyo na kuuza nakala 328,000 na hadi leo bado unauzika kama keki.

Kulungile Baba ulipendekezwa kama Wimbo Bora wa Mwaka katika Tuzo za Crown, ulishinda pia tuzo kubwa katika tasnia ya muziki zinazoitwa SAMA19 na kujinyakulia tuzo ya ‘Rekodi ya Mwaka ’ 2013 na alishinda Tuzo ya AGMA, hizo ni tuzo za injili zinazotolewa London, Uingereza.

Msanii huyu aliyeumbwa kwa moyo wa unyenyekevu na kujali wengine, katika maisha yake amekuwa akifanya kazi za kibinadamu akisaidia jamii kama shukrani za kumuunga mkono muda wote wa kazi yake ya kueneza injili. Hivyo aliamua kufungua Mfuko wa Ufadhili wa S’fiso Ncwane.

Kupitia mfuko huo amekuwa akichangia sare za shule kwa watoto wa shule zaidi ya 1,000 na amechangia zaidi ya Randi 10,000 kwa shule zilizopo maeneo ya vijijini. Kama hilo halitoshi, S’fiso aliamua kurekodi albamu ambayo mapato yake alitoa kwa watoto yatima Johannesburg.

Mwanamuziki huyu mkubwa Afrika Kusini ametoa sana kwa wenye mahitaji na wala hakuwa mtu wa kutafuta sifa kwa watu kwa sababu ya utoaji wake.

Aliamini Mungu akisema, “Imebarikiwa mikono inayotoa". Huyo ndio Sfiso, msanii wa injili ambaye atakumbukwa na wengi kama mtumishi wa Mungu, msanii na mhisani asiyekuwa na makuu.

Katika hatua nyingine, inaelezwa kuwa nyota huyo wa Injili alikuwa aende kutoa burudani nchini Zimbabwe na alimuomba mbunifu mmoja wa Zimbabwe nchini Afrika Kusini amshonee nguo ya kipekee kwa ajili ya kuvaa atakapotoa burudani mjini Harare, Desemba 9.

Sfiso alikuwa atoe burudani kwa kushirikiana na mwanamuziki wa Zimbabwe, Tatenda Mahachi, ambaye wameshirikiana kwenye wimbo Ngiyamthanda uJesu mwaka jana.

Mara ya mwisho waliimba wote mjini Durban, mwezi Mei. “ Mara ya miwsho tulizungumza Ijumaa iliyopita alipothibitisha kuwa yuko tayari kuja Zimbabwe,” alisema Tatenda.

Lakini mbunifu huyo wa mitindo wa Zimbabwe, Thembani Mubochwa amebakiwa na koti ambalo alimshonea mwanamuziki huyo. Karibu muongo mmoja uliopita Thembani pia alimshonea suti ya harusi Sfiso na mkewe Ayanda, gauni la harusi.

Sfiso alizikwa jana na taarifa ya shughuli nzima ya mazishi na maziko yake zilitolewa na msemaji wa familia Sipho Makhabane, aliyethibitisha kufanyika ibada mbili za kumkumbuka na maziko.

Ibada ya kwanza ilifanyika Alhamisi katika Kanisa la eThekwini Community, mjini Durban. Ibada ya pili ilifanyika Ijumaa katika Kanisa la Grace Bible, mjini Soweto.

Shughuli mazishi za nyota huyo wa nyimbo za injili zilifanyika jana katika Uwanja wa Moses Mabhida, Durban, kisha mwili wake kuzikwa katika makaburi ya Heroes Acre, KwaZulu-Natal.