SAMWEL MPARANGE: Mtawa, mganga, mfugaji na mkulima

NAFIKA kitongoji cha Nandanga kilichopo katika kijiji cha Itete barabara kuu itokayo Ifakara kuelekea wilaya mpya ya Malinyi mkoani Morogoro na kukuta nyumba moja ya kisasa iliyojitenga, ambayo inanipa hisia kuwa mmiliki wake atakuwa na sifa mbili kubwa, moja ya ukulima na ya pili, ufugaji.

Nikiwa naendelea kutafakari ni nani mkazi wa nyumba hiyo, mimi na mwenyeji wangu aliyeniwezesha kufika wilayani Malinyi, Mkurugenzi wa Halmashauri mpya ya Malinyi, Marcelin Ndimbwa, ghafla anajitokeza mzee mfupi, mwenye rangi angavu ya mwili, akiwa na nywele nyeupe kichwani na kutukaribisha. Wakati salamu baina ya wageni na mwenyeji wetu zikiendelea, haraka haraka naanza kuchunguza mazingira yanayozunguka nyumba hiyo.

Kwa haraka naona nyumba hiyo ikiwa na paneli ya umemejua katika paa lake na chini upande wa kulia kuna ungo mkubwa wa kunasa mawimbi ya televisheni. Natupia macho yangu upande wa nyuma wa nyumba na kuwaona vijana wasiopungua 15 wenye umri wa kati ya miaka 14 na 20 wakifanya shughuli mbalimbali, zikiwemo za kuweka pumba kwenye tanuru ili kuchoma moto. Mbali ya vijana hao, naliona trekta lenye tela, halafu naona majengo mawili pembeni yaliyojengwa kama nyumba za kuishi.

Napata shauku ya kufahamu zaidi, mzee huyu ninayemuona mbele yangu ni nani, vijana wale ni akina nani, majengo yanayozunguka nyumba ile ni ya nini, na maswali mengine mengi yanaibuka kichwani mwangu na hivyo kutamani kupata majibu. Bila kujitambulisha yeye; mzee huyu anatambulisha msa- fara wetu kwa wale vijana; “jama- ni huyu ndiye Mkurugenzi wetu wa Malinyi (Ndimbwa).

Kwa wale msiomfahamu basi ndio wakati wa kumfahamu,” anamaliza kutoa utambulisho mfupi na kuondoka kuelekea yalipo majengo yale ambayo bado nilikuwa sijajua ni ya nini. Baada ya kulifikia jengo la kwanza lililojengwa kwa matofali ya kuchoma kwa mfano wa yai, mzee huyu anasema hilo ni zizi la mifugo aliloamua kulijenga kisasa. Anasonga mbele kuliendea jengo la pili ambalo limejengwa mfano wa nyumba ya kuishi.

Anasema ni nyumba ya kufugia ng’ombe na nguruwe kwa njia ya kisasa. Ndani tunawakuta ng’ombe wakubwa wa kisasa anaowataja kwa majina ya Baraka, Julai na Chausiku. Tunashuhudia pia kuwepo kwa nguruwe wa kisasa wakubwa wakiwa na vitoto.

Ni kutokana na kile ninachoendelea kukiona kutoka kwa mzee huyu, naanza kuamini kuwa kuna mambo mengi makubwa yamejificha nyuma ya huyu mzee, nalazimika kuomba kufanya mahojiano ya kina naye ili kumfahamu zaidi na hakika nafurahia uamuzi wangu hadi leo kutokana na kusikia mambo makubwa kutoka kwake. Kwa jina anaitwa Samwel Mparange. Ingawa awali nilihisi mzee huyu kuwa na sifa za ufugaji na ukulima, nabaini mengi kutoka kwake.

Mparange ni mtawa sawa na watawa wanawake wa Kanisa Katoliki tuliozoea kuwaona. Anasema aliamua kwa hiari yake kuingia katika maisha ya utawa, lakini uamuzi wake huo ukiwa umetanguliwa na uamuzi mgumu zaidi na ulioleta patashika baina yake na nduguze, pale alipoamua kuondoka katika dini yake ya awali ya Uislamu na kujiunga na Ukristo.

“Ulikuwa ni uamuzi wangu tu. Ulileta mzozo katika familia lakini baadaye walinielewa. Niliamua kumtumikia Mungu kwa upande huu. Sijutii kuwa mtawa na hivyo kutooa na kutozaa watoto wangu mwenyewe, kwani hivi sasa nina watoto wengi (yatima) kuliko wale ambao ningewazaa,” anasema. Kutokana na kuwa mtawa, Mparange hajawahi kuoa wala kupata watoto katika maisha yake yote. Aliamua kwa ridhaa yake kukabidhi maisha yake kwa Mungu na apate muda mwingi wa kusaidia jamii yenye uhitaji maalumu.

Na hilo limewezekana kwani kupitia kazi mbalimbali alizowahi kufanya ikiwemo kuwa Mganga Msaidizi katika hospitali mbalimbali nchini, Mparange ameweza kufanya kazi nyingi, ikiwemo ya kutoa huduma kwa wajawazito wakati wa kujifungua. Anasema ingawa ilikuwa maajabu wakati huo kwa mganga mwanamume kutoa huduma kwa wakina mama wanapojifungua, lakini huduma aliyokuwa anaitoa ilifanya wajawazito wengi kupenda kujifungua mikononi mwake.

Anasema hilo lilitokana na huruma ya ajabu aliyokuwa nayo kwa wakina mama wakati wa kujifungua. “Hakika nilikuwa na huruma sana. Wanawake wengi waliokuwa na matatizo wakati wa kujifungua walikuwa wanaletwa kwangu na nilikuwa nawasaidia kujifungua vizuri na wengi walikuwa wananipa zawadi ya watoto wao kwa kunifanya kuwa baba yao wa heshima. Huruma yangu kwao iliwafanya pia wanipachike majina mbalimbali likiwemo la Baba Haleluya.”

Mparange, mtawa wa tatu wa Mt Francisco, akisimulia historia ya maisha yake anasema alizaliwa Desemba 25, 1949 na kupata elimu ya msingi katika Shule ya Msingi Kiswago iliyopo Kata ya Sofi wilayani Malinyi na kumaliza mwaka 1965. Anasema mwaka 1968 alijiunga na Shule ya Kati (Middle School) katika Shule ya Sofi, mwaka 1972 alijiunga na sekondari ya Kwilo iliyopo Mahenge Ulanga.

Anasema kati ya mwaka 1973 na 1975 alijiunga na Kambi ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) mkoani Tanga. Anasema alianza kazi ya mganga msaidizi mkoani Tanga, lakini baadaye alifanya kazi hiyo katika maeneo ya Kilosa, Morogoro, Sumbawanga na hatimaye akarudi nyumbani katika hospitali ya jirani ya Mtimbira wilayani Malinyi wakati huo wilaya ikiitwa Ulanga, akiifanya kazi hiyo kuanzia mwaka 1978 hadi 1985.

“Kikwazo kikubwa kwa kazi yangu ya mganga msaidizi ilikuwa ni uelewa wa wananchi. Pamoja na kuwa huduma za afya zikiwemo za wajawazito kuzalishwa zilikuwa zikitolewa bure, lakini mwamko wa watu kufika hospitali ulikuwa ni mdogo. “Ukiondoa kikwazo hicho, binafsi nilikuwa nafurahi sana kufanya kazi ya uganga hasa kuwasaidia kina mama kujifungua. Nilikuwa na huruma kuliko manesi wanawake. Wagonjwa walinipenda sana na kwa vile nilikuwa natembelea maeneo mengi nilikuwa naitwa kwa majina mbalimbali.

“Kila nikimzalisha mtoto, mama mwenye matatizo ya uzazi basi mtoto aliyezaliwa alikuwa wangu. Nakumbuka siku naondoka katika kazi hii pale Mtimbira, wakina mama waliandamana hadi kwa viongozi wa wilaya, yaani Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi,” alisema Mparange. Anasema ilipofika mwaka 1989 ndipo alipoamua kufanya rasmi kazi za utawa katika Kanisa la Itete, kazi yake kubwa ikiwa ni kulea watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu, kazi anayoifanya hadi leo.

“Tangu wakati huo kazi yangu kubwa imekuwa ni kulea watoto yatima. Kwa sasa tunao watoto yatima 36, maana wengi wameondoka kwenda kufanya kazi za kujitegemea, lakini huko nyuma kituo chetu kilikuwa na watoto zaidi ya 100,” anasema. Katika kudhihirisha nia yake ya dhati ya kuwasaidia wananchi masikini, ikiwemo watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu, Mparange anasema aliamua kuanzisha shule yake ya sekondari aliyoibatiza jina la Bishop Mchonde Memorial School yenye kidato cha kwanza hadi cha nne iliyoanza mwaka 2008.

Anasema kazi ya shule hiyo ambayo ni ya bweni yenye mchanganyiko wa wanaume na wanawake, ni kuwasaidia watoto yatima wanaolelewa katika Kituo cha Itete kupata sehemu ya kupata elimu ya sekondari, huku akisema watoto hao wanachukua asilimia 95 ya watoto masikini.

“Kwa upande wa shule naweza kusema natoa huduma tu na wala siangalii faida kama wanavyofanya wamiliki wengi wa shule hivi sasa. Kwa taarifa yako, hapa nalima mpunga, mboga, matunda na pia nafuga, lakini vyote hivi navitumia kwa chakula kwa watoto wangu pale shule,” anasema. Ninapomuuliza kuhusu ufugaji na hasa ninapoanza kutaja majina ya ng’ombe wa kisasa anaowafuga, nabaini uso wa Mparange kubadilika na kuwa wenye simanzi kidogo.

Anasema pamoja na kuwa na ng’ombe Baraka, Julai na Chausiku, lakini hivi karibuni alimtoa sadaka ng’ombe aliyekuwa anajulikana kwa jina la Sokoine kwenye sherehe ya uzinduzi wa nyumba ya watawa wa Kanisa Katoliki Mbingu. Hata hivyo pamoja na furaha ya kutoa sadaka hiyo, lakini alishindwa kuvumilia namna ng’ombe huyo alivyochinjwa.

“Kutokana na ukubwa aliokuwa nao haikuwezekana kumchinja kama ilivyo kawaida. Ililazimika afungwe kwenye mti na apigwe risasi. Alipopigwa risasi ya kwanza kichwani nilivumilia, akapigwa ya pili nikavumilia, alipopigwa ya tatu, alipiga magoti, hapo sikuweza kuvumilia tena niliwaambia jamani sitaki risasi tena, naomba sasa mumchinje kawaida. “Ilibidi wamchinje kwa tabu sana maana alikuwa mkubwa sana. Shingo yake tu ilikuwa na kilo 56, nyama yake ililiwa na watawa kwa wiki nzima bila kuisha. Mbegu ya ng’ombe huyo niliipata kutoka Denmark.”

Hata hivyo, katika mazungumzo yetu nabaini kuwa Mparange ana mafunzo makubwa ya namna ya kufuga kisasa. Ingawa ng’ombe Sokoine alitolewa kama sadaka, lakini ng’ombe Baraka ni mfano mwingine wa ng’ombe gumzo nchini kwani katika maadhimisho ya Nanenane mwaka huu ng’ombe huyo amekuwa bora kwa Kanda ya Mashariki akiwa na uzito wa tani 2.5.

Ng’ombe wengine Julai na Chausiku pia si wa mchezo mchezo, kwani ni miongoni mwa ng’ombe wanaotegemewa kuwa tishio nchini kwani pamoja na kuwa na umri mdogo hivi sasa maumbo yao ni makubwa na wanapendeza machoni. Kwa upande wa nguruwe pia Mparange anajivunia mafanikio. Kama ilivyokuwa kwa ng’ombe Sokoine, mtawa huyo aliwahi kutoa sadaka pia ya nguruwe mkubwa aliyekuwa anajulikana kwa jina la Jenerali kwenye shughuli ya kumpongeza Baba Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Ifakara, Askofu Salutaris Libena.

Anasema mafanikio yake katika ufugaji yanatokana na mafunzo aliyoyapata kupitia Mradi wa Esowe wa namna ya kufuga kisasa. Mazungumzo yangu na mtawa huyu, hayaishi hivi hivi, namuomba anipe maoni yake ya namna anavyoona mambo yanakwenda kwa Taifa la Tanzania na bila kusita anasema analiona tatizo kubwa la watu kukosa uzalendo kwa taifa lao na hasa katika kufanya kazi za kujitolea.

“Yaani sasa hivi kila kitu kinageuzwa dili. Wakati wetu tulikuwa wazalendo na tulikuwa tunafanya mambo kwa kujitolea kwa manufaa ya taifa, lakini sasa hali ni tofauti sana. Kila kitu inaangaliwa faida. “Napongeza sana hatua zinazoanza kuchukuliwa na serikali ya sasa ya Awamu ya Tano (ya Rais John Magufuli). Hili suala la kuanzisha elimu bure kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne limenifurahisha sana. Bila Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere kufanya elimu bure mimi nisingesoma.

“Wakati ule wa mwanzo ada ya kidato cha kwanza hadi cha nne ilikuwa Sh 250 ikawa inanipa tabu sana kulipa hadi pale Mwalimu Nyerere alipofuta kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne. Lakini kwa vile kidato cha tano na sita ilikuwa Sh 960 nilishindwa kulipa ndio maana nikaenda Chuo cha Uganga.

“Sasa naona falsafa za Mwalimu Nyerere zinarudi, nafurahi sana. Na kwa dhati naomba niwapongeze Mkuu wa Wilaya ya Malinyi, Majura Kasika, Mkurugenzi Mtendaji, Ndimbwa na Mwenyekiti wa Halmashauri, Nasoro Liguguda kwa kufanya kazi kwa staili ya Rais Magufuli. Hamasa wanayotupa katika kilimo, ufugaji na katika mambo mengine ni chachu ya maendeleo ya haraka kwetu,“ anasema.

Hadi hapo niliweza kumfahamu kwa kina mzee huyu Samwel Mparange, mtawa, mganga msaidizi, mkulima, mfugaji, mkazi wa kitongoji cha Nandanga wilayani Malinyi mkoani Morogoro.