ELIZABETH SWAI: Mjasiriamali aliyebobea katika elimu ya ufugaji

SEKTA ya ufugaji kwa muda mrefu imekuwa ikichukuliwa kama sekta ya kawaida ambayo haina mchango mkubwa sana kwenye kuinua kipato cha mtu mmoja mmoja.

Lakini kwa sasa kumekuwa na fursa nyingi zaidi katika ufugaji na wapo wafugaji wanaonufaika na sekta hiyo. Pia wapo wanawake ambao wamezishika fursa zipatikanazo katika ufugaji kujihusisha katika sekta hiyo kwa njia tofautitofauti zikiwapo za kujinufaisha au kuwanufaisha watu. Elizabeth Swai, amejikita katika sekta ya ufugaji kwa kuuza vyakula vya kuku, kutotoresha vifaranga na kuuza na pia kutoa huduma nyingine zinazohusiana na ufugaji.

Yeye ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa kampuni ya AKM Glitters Limited inayojihusisha na bidhaa za ufugaji pamoja na chakula cha kuku, hiyo kwake sio tu biashara kama biashara ila ni shughuli ambayo ameisomea pia. Mwanamama huyu alianzisha kampuni hiyo mwaka 2006 ambapo hapo ikiwa ni baada ya kuacha kazi katika Shirika la Umoja wa Mataifa lijishughulishalo na masuala ya Chakula, FAO.

Elizabeth anasema aliamua kuacha kazi sio kwa kuwa alikuwa na matatizo na mwajiri wake huyo au alifukuzwa, ila anaweka wazi kuwa aliona fursa kubwa katika sekta ya ufugaji. Anasema kuwa akiwa na FAO alikuwa na nafasi nzuri ambayo alikuwa akiona kuwa ingeweza kuendelea kumpatia mshahara mzuri na kujiwezesha zaidi kimaisha. Anaweka wazi kuwa aliona kuwa akiwa na ofisi hiyo ni sawa na kuwa hafanyi yale ambayo alikuwa akitakiwa kuyafanya kwa undani zaidi na hivyo kuamua kuacha kazi na kufanya kazi zake.

Anaweka wazi kuwa ikiwa ni baada ya kuifanyia kazi ofisi pamoja na ofisi nyingine zilizo chini ya Umoja wa Mataifa kwa miaka 17 alipata ujuzi wa mambo mbalimbali na ndio yaliyomwezesha kuanzisha kampuni yake hiyo. Anasema pia aliwahi kufanya kazi na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia wakimbizi, UNHCR, akiwa anafanyia kazi zaidi mkoani Kigoma.

Akizungumzia historia ya kampuni yake hiyo ya ufugaji, anasema alianzisha kampuni hiyo kwa kuwa alikuwa na shauku pia ya kusaidia jamii ya wafugaji. Anasema kuwa baada ya kuianzisha mwaka 2006 na kuanza kazi rasmi ikiwa imesajiliwa mwaka 2007, alifanya kazi kwa muda na kisha mwaka 2009 hadi 2012 aliamua kujiendeleza zaidi katika elimu ya masuala ya ufugaji. Anasema, alianza biashara yake hiyo akiwa ameweka kipaumbele zaidi katika nidhamu ya kazi yake hiyo.

Anasema amekuwa akiiona kampuni yake hiyo ikikua siku hadi siku na kisha kuja kufikia hatua ya kufahamika na kuendeleza kazi kwa ufanisi zaidi. Kwa sasa imekuwa ikiendeshwa si tu kama ofisi ila ni kama pia mradi wa kuwasaidia wafugaji wa kuku. Katika shughuli zake za kuelimisha katika suala zima la ufugaji wa kuku anasema kuwa ameweza kuwafikia wafugaji kutokea mikoa ya Morogoro, Tabora, Dodoma, Simiyu, Singida, Manyara, Shinyanga vijijini pamoja na sehemu mbalimbali za Mkoa wa Dar es Salaam.

Anasema katika Dar es Salam kampuni yake imewafikia wafugaji kutokea maeneo ya Tandika, Kimara, Bunuu, Visiga, Bagamoyo pamoja na Tegeta. “Lengo la kampuni hii kubwa ni kuwaona wafugaji wa kitanzania wanakuwa kiuchumi na kunufaika na kila kile kitokanacho na sekta hiyo kuanzia mifumo hadi sera za kuwainua wafugaji,”anasema Elizabeth. Anaongeza kuwa, “kampuni hii imekuwa mstari wa mbele kusikiliza sauti za wafugaji na kuziwakilisha kwa wahusika na hasa kwa wale wanaosimamia shughuli za kiserikali katika wilaya husika”.

Anasema kampuni yake hiyo imekuwa ikiwatumia vijana kutokea vyuo vya ufugaji na kilimo katika kutoa elimu hiyo kwa wafugaji hasa wa mikoani. Anasema kila mwaka wamekuwa wakichukua wanafunzi hadi 50 ambao wanawaongezea ujuzi kuhusu masuala ya elimu na kisha kuwapeleka mikoani kuwafundisha wafugaji. Anasema, vijana hao wamekuwa wakiishi vijijini hadi kwa muda wa miezi mitatu ambapo moja kati ya vitu wanavyowafundisha wafugaji ni pamoja na utunzaji wa fedha.

Anasema kwa kuwa wafugaji wamekuwa wakipata faida kutokana na ufugaji wao huo, hivyo kuna umuhimu wa kuwaelimisha kuhusu suala zima la kuendesha biashara hiyo pamoja na kuimarisha vikoba vyao. Anaweka wazi kuwa kupitia kampuni yake hiyo amekuwa akiwaelekeza wafugaji kuhusu namna ambavyo wanaweza kunufaika na fedha za serikali zitolewazo kwa wafugaji.

"Najua kuna fursa nyingi katika ufugaji na hasa huu wa kuku kwa kuwa kwanza ni miradi ambayo imekuwa ikiwainua kimaisha wafugaji wengi na hivyo AKM Glitters Company imekuwa ikiwaelezea wafugaji ni wapi kuna fursa wanazoweza kunufaika nazo," anasema Elizabeth. Akizungumzia ni kwa namna gani anaweza kusimamia familia pamoja na shughuli zake hizo, anaweka wazi kuwa yeye ni mama wa mtoto mmoja na kwa miaka mingi ameweza kumudu suala zima la familia na biashara zake.

Anasema kama mwanamke mjasiriamali anakumbana na changamoto mbalimbali, lakini anasimama na kuzishinda kwa kuwa amekuzwa katika misingi ya kutafuta. Kutokana na umahiri wake huo katika sekta ya ufugaji amejikuta akishirikiana na wadau wengine mbalimbali katika kuanzisha miradi kadhaa ya kuwasaidia wakulima na sekta ya kilimo kwa ujumla. Yeye ni mwanzilishi wa mtandao wa Wanawake wa Afrika wanaojihusisha na Kilimo na pia ni mwanzilishi wa Africa Agriculture Academy.

Anawataka wanawake kujitambua na kuwa na nia ya kufanikisha kila kile wanachoamua kukifanya huku akiweka wazi kuwa anachukia wanawake wanaojipendekeza na kujikuta wakiwaangamiza wenzao. Anasema wapo wanawake ambao wanapenda kujipendekeza na kuwa tayari hata kuwatukuza wengine wa nje ya nchi huku wakidharau kuwainua watanzania wenzao. Anawataka wanawake kuwa na hali ya kujiamini, kujiona ni sawa na wajasiriamali wengine, kujiheshimu pamoja na kujiendeleza kielimu.

Lakini pia anachukizwa na tabia ya watu wanaokula fedha za serikali zinazolenga kuwasaidia wafugaji na kutaka kuona kuwa fedha hizo zinakwenda moja kwa moja kwa wafugaji husika. Anamuomba Rais John Magufuli kuhakikisha kuwa anaitazama sekta hiyo ya wafugaji ili katika harakati zake za kuwa na Tanzania ya viwanda aone kuwa hiyo sekta inaweza kuchangia kitu. Anasema zipo taasisi za kifedha ambazo zinaweza kuwasaidia wafugaji, lakini kunakuwa na changamoto kadhaa inazowawezesha kufanikiwa katika hilo.

Kwa upande wake Elizabeth ametoa ajira ya kudumu kwa wafanyakazi wake 20 huku akiwa amejipanga kuajiri wafanyakazi wengine 77 watakaokuwa na jukumu la kuhudumia wafugaji katika mradi mkubwa anaotarajia kuuanzisha mwezi ujao. Elizabeth mbali na kutumia muda wake mwingi kufanya kazi na kusaidia jamii ya wafugaji lakini mwanadada huyo anapenda pia kujihusisha na masuala kadhaa ya kijamii.

Anapenda kusikiliza muziki hasa nyimbo za Bongo Fleva akiwa anavutiwa zaidi na msanii Nasib Abdul a.k.a Diamond Platinum huku akiwa anapenda pia nyimbo za Oldies. Anapenda kusoma vitabu pamoja na kuangalia filamu na hasa vyote vile vyenye kuchochea mfumo chanya. Mwanadada huyu anaonekana kuwa ni nadhifu na mwenye kujipenda pia hasa akiwa anaamini kuwa kila anachoweza kukifanya ni lazima akifanikishe kwa nguvu zake bila ya kutegemea uanamke wake ila uwezo wake kwa kuwa anaamini kuwa anaweza, ataweza na lazima afanikiwe.