DK THERESIA NKYA: Daktari wa Falsafa aliyetimiza ndoto zake za uanasayansi

WANAWAKE wengi wamekuwa wakikabiliwa na changamoto mbalimbali maishani mwao, jambo linaloweza kuwakatisha tamaa kufanya maendeleo yao kuanzia shule, kazini na maeneo mbalimbali.

Leo tunaye Mwanasayansi Mtafiti Mwandamizi na Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) Amani, Muheza mkoani Tanga, Dk Theresia Nkya akiwatia moyo wasichana na wanawake wanaopitia changamoto mbalimbali.

Anasema akiwa mwanafunzi alikuwa na msukumo wa kutaka kusoma masomo ya sayansi kutokana na matamanio yake ya kuwa mwanasayansi mahiri, hivyo alipata msukumo na mazingira rafiki ndani ya familia na katika shule ambazo alisoma kuanzia shule ya msingi mpaka vyuo vikuu yamemwezesha kufikia ndoto yake ya kuwa mwanasayansi mahiri.

Dk Theresia anasema mchango mkubwa aliupata kutoka kwa mama yake mzazi, Lucy Nkya mwanamke aliyewahi kuwa Waziri wa Afya katika serikali zilizopita ambaye ni Daktari akiwa na Taaluma ya Sayansi kitaifa na kimataifa. Anasema mpaka kupata Shahada ya Uzamivu (PhD) amepitia changamoto mbalimbali, lakini kubwa ni wakati akiwa sekondari alinyanyaswa na wanafunzi wenzake ambao hawakuwa na nidhamu na nia ya kusoma kwa bidii kwa sababu walimuona kama ana kimbelembele cha kusoma kwa bidii na kufaulu hasa katika masomo ya sayansi.

“Hii iliwafanya waanze kuninyanyasa kwa maneno ya kejeli na hata kunitishia kunipiga, hata hivyo sikukata tamaa nilikazana na kusoma kwa bidii,” anasema. Anaeleza changamoto nyingine kuwa alipokuwa Chuo Kikuu nchini Marekani akichukua Shahada ya Kwanza, makundi ya marafiki ambayo yalikuwa na mwelekeo walikuwa wakimshawishi kuingia kwenye tabia mbaya ili asisome kwa bidii.

“Kwa kuwa nilikataa kujiunga na makundi hayo mabaya, nilisingiziwa kila jambo baya na kuonekana kama ni mshamba na sijichanganyi na wenzangu, niliyaachilia mbali hayo bila kuyajali niliendelea kusoma kwa nguvu zangu zote,” anaeleza. Anasema bado hata alipokuwa Chuo Kikuu cha Muhimbili wakati akisomea Shahada ya Uzamili, aliendelea kupata upinzani kutoka kwa mmoja wa wahadhiri mwanamke ambaye alimhakikishia na kumtisha kwamba hatamaliza masomo hayo kwa sababu zake binafsi ambazo hakuzijua.

“ Ilinibidi niongeze nguvu ya kusoma ili asipate sababu ya kunifelisha ambayo matokeo yake nilipata madhara ya kiafya ya vidonda vya tumbo kwa sababu ya msongo wa mawazo, hata hivyo Mungu wangu alinisaidia nilifaulu mitihani yangu yote na kuwa pekee mpokea Shahada ya Uzamili ya Parasaitolojia na Wadudu wanaodhuru binadamu kwa mwaka wa 2010 katika chuo hicho,” anaeleza.

Dk Theresia anaeleza kuwa wazazi wake wamechangia kufika hapo alipo, kwani ndiyo walimshawishi kuweka malengo ya juu kielimu maana hata wao wamesoma vizuri sana. Anamuelezea baba yake aliyekuwa Profesa wa Uchumi na mama yake ambaye ni Daktari Bingwa wa Afya ya Akili (Psychiatry) na ya Jamii (Public Health). Mwanasayansi huyo mcheshi anasema mume wake pia amechangia kufikia hapo alipo, hasa alipokuwa akisomea Shahada yake ya Udaktari wa Falsafa, kwa kumtia moyo na kumuinua pale alipokuwa amekata tamaa kutokana na changamoto nyingi alizokumbana nazo.

Mtaalamu huyo anaeleza kuwa wakati anasoma Shahada yake ya Kwanza nchini Marekani (Bachelor of Science) alifanya kazi za kulea watoto pamoja na msaidizi muuguzi aliyethibitishwa (certified nursing assistant) ili kujiongezea kipato kwa ajili ya mahitaji yake ya kila siku. Mwanamke huyo ambaye ameolewa, mwenye mtoto mmoja wa umri wa miaka mitatu kasoro, anasema alianza kazi NIMR mwaka 2007 kabla mama yake hajateuliwa kuwa waziri katika wizara ya afya hivyo kukanusha tuhuma kuwa mama yake alimuweka kufanya kazi.

“Hamna mahali popote katika kazi yangu ambapo wadhifa wa mama yangu umetumika kunivusha au kunisukuma au kupendelewa, nimesoma na nimepanda vyeo kutokana na elimu yangu, taaluma yangu na juhudi kubwa ya ufanyaji kazi wangu kwa ubora, maarifa na umahiri mkubwa,”anasisitiza. Dk Theresia anasema katika harakati zake za kusoma hatasahau tukio la ugonjwa wa baba yake kwani ilikuwa changamoto kubwa, kwani ndiye aliyemhimiza kusomea PhD.

“Nakumbuka nikiwa mtoto baba alirudi kutoka masomoni akaniambia yeye ni dokta wa filosofia, nikamwambia baba na mimi nataka kuwa kama wewe kabla sijafikisha miaka thelathini. Kwa bahati mbaya baba yangu hakuweza kuhudhuria mahafali yangu wakati natunukiwa PhD kwa sababu ya kuumwa sana na baada ya muda mchache alifariki dunia,” anasema. Anasema katika kumkomboa mwanamke, anatarajia kuhamasisha wanawake wote walio katika uongozi, uhadhiri au taaluma nyingine kuwa mkombozi wa mwanamke ni mwanamke mwenyewe hivyo lazima kupendana na kusaidiana ili kila mmoja aweze kufikia malengo aliojiwekea.

Dk Theresia anasema yuko kwenye harakati ya kuanzisha ‘mentorship program’ ambayo itawapa nafasi wasichana wanaosoma sayansi hapa nchini kuzungumza na kushirikishana changamoto wanazokutana nazo na wanawake ambao wameshapitia changamoto hizo. Anawaeleza watoto wa kike kuwa wanaweza kusoma masomo ya sayansi kwa wazazi kuwasaidia na kuwatia moyo huku wakipeana ushauri, msaada na msukumo ili watoto wa kike waweze kupata mazingira wezeshi yatakayowawezesha kufikia ndoto zao za kuwa wanasayansi na wanataaluma bora.

Anasema akinamama wawape watoto wao nafasi ya kusoma wanaporudi nyumbani, kuwafuatilia katika masomo yao na inapobidi kuwatafutia masomo ya ziada (tuition) baada ya shule na wakati wa likizo kwani mama ndio dira na mfano wa kuigwa na watoto wetu hususani mabinti. Mwanadada huyu anaeleza historia yake kuwa ni mtoto wa tatu kuzaliwa katika familia ya watoto wanne ya Profesa Estomih Nkya (marehemu) na mkewe Dk Lucy Nkya.

Anasema alizaliwa Januari 1, 1984 katika hospitali ya mkoa Morogoro, na baadaye kusoma shule ya msingi Mwere na kuhamia shule ya msingi Bungo na baada ya hapo Morogoro International School. Alisoma sekondari katika Shule za Mama Clementina Foundation Kilimanjaro Academy iliyopo Moshi na baadaye kumalizia kidato cha nne Shule ya St. Constantine International iliyopo Arusha.

Kwa mujibu wa Dk Theresia elimu ya juu alisoma nchini Marekani katika Chuo cha Elimu ya Juu kinachojulikana kama Houston Community College ambapo alisoma masomo ya kujitayarisha kuingia kusoma Shahada ya Kwanza na baadaye alianza masomo ya Shahada ya Kwanza katika Chuo Kikuu Texas Southern na kuhitimu mwaka 2006. Anasema alirejea nchini na kufanya kazi katika Shirika lisilo la kiserikali la Faraja Trust Fund na watoto waliokuwa wanaishi na virusi vya Ukimwi, kisha kupata kazi NIMR- Kituo cha Amani kilichopo Muheza, Tanga mbako yuko mpaka sasa.

Lakini mwaka 2008 alianza masomo ya Shahada ya Uzamili (Masters’ degree in Parasitology and Medical Entomogy) katika Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikihsi Muhimbili(Muhas) ambapo alihitimu na kupata Shahada ya Uzamili daraja la juu akiwa mhitimu pekee. Hakuridhika mwaka 2011 alianza mafunzo ya PhD katika Chuo cha Tumaini-Makumira KCMU-College na kufanya kozi shirikishi na chuo kilichopo Ufaransa kiitwacho Grenoble University na kuhitimu mwaka 2015.

Anasema katika maisha yake amewahi kupata tuzo ya uanafunzi bora kutoka chuo kikuu cha Muhimbili na mwezi Aprili mwaka huu aliteuliwa na Waziri wa Maliasili na Utalii kuwa mjumbe wa bodi ya Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI). Pia amepata fursa ya kuchangia sera ya nchi katika matumizi ya viuatilifu (insecticides) katika kupambana na malaria.

Anaeleza kuwa mbali na majukumu yake ya kikazi anapenda kujishughulisha na masuala ya ujasiriamali hususani bidhaa za urembo, huku akipendelea kusoma vitabu, muziki, kusafiri na kuangalia filamu.

“Nishauri serikali pamoja na kutoa elimu ya bure kwa watoto ihakikishe walimu wanafundisha wanafunzi inavyotakiwa kwa viwango na pale inapobidi wapewe motisha, vitendea kazi vipatikane na mazingira ya kusomea hususani madarasa. “Pamoja na serikali kujitahidi kutoa dawa za kichocho na minyoo mashuleni pamoja na chanjo ningependa kushauri serikali kuangalia namna ambayo watoto watapata chakula shuleni kwa sababu njaa ina mchango mkubwa sana katika kudumaza maendeleo ya elimu kwa watoto,” anashauri Dk Theresia.

Anashauri pia serikali katika maeneo ya vijijini yenyewe au ishawishi mashirika yasiyokuwa ya kiserikali au watu binafsi wajenge maktaba ili watoto wajenge mazoea na wawe na mazingira ya kuweza kujisomea vitabu vya ziada na kiada ili waweze kupanuka kitaaluma. Huku akiwataka wazazi wajenge tabia ya kufuatilia maendeleo ya watoto wao kitaaluma na wakati mwingine pia watoe ushirikiano na walimu katika malezi ya watoto.