GREDAH MWAKYEMBE: Mtumishi anayehaha kuokoa pensheni ya uzeeni

“KWA jina naitwa Gredah Mwakabumbe, au ukipenda unaweza kuniita kwa jina letu maarufu la ukoo la Mwakyembe. Mimi ni Ofisa Tarafa katika Tarafa ya Tukuyu Mkoani Mbeya, nikiwa nahudumia kata tatu za Bulyaga, Msasani na Bagamoyo.”

Gredah anatoa maelezo hayo ya utambulisho wake binafsi akiwa amejumuika na wakulima wenzake wanaoendesha kilimo cha zao la mpunga katika Skimu ya Umwagiliaji ya Itete, iliyopo wilayani Malinyi mkoani Morogoro. “Nimelazimika kutumia likizo yangu hii ya Novemba (2016), kusafiri kutoka katika makazi yangu na kituo changu cha kazi vilivyopo Tukuyu mkoani Mbeya kuja hapa Itete, wilayani Malinyi katika Mkoa huu wa Morogoro ili kuja kushiriki katika kilimo hiki cha mpunga,” anasema.

Ingawa mama huyo anaeleza jitihada mbalimbali ambazo amekuwa anazichukua katika kushiriki katika shughuli za kilimo, lakini navutiwa zaidi na maelezo yake kwamba anahangaika na kilimo usiku na mchana ikiwa ni mkakati wake wa kutathimi kazi sahihi ya kufanya baada ya kustaafu.

“Natarajia kustaafu kutoka katika utumishi wa umma ifikapo Mei, 2018 kwani nitakuwa nimetimiza miaka 60 kamili na kwa hiyo nitalazimika kustaafu kwa lazima kwa mujibu wa sheria. Nataka nikistaafu niwe nimefanya maandalizi ya kutosha ya ni kazi au shughuli gani itanifaa,” anasema Ofisa Tarafa huyo ambaye anachangia michango yake katika Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa NSSF.

Maelezo ya Gredah yananifanya kukumbuka ushuhuda ambao umekuwa unatolewa katika maeneo mbalimbali na wastaafu wa serikali ambao wengi wamekuwa wakijutia namna walivyotumia malipo yao ya pensheni ya kustaafu kwa shughuli ambazo hatimaye ziliwaingiza katika umasikini mkubwa.

Mbali ya wao wenyewe kutoa ushuhuda huo, lakini pia familia za wastaafu wengi zimekuwa zikitoa ushuhuda wa namna wazee wao walivyojiingiza katika miradi ambayo haikufanyiwa utafiti wa kina na kujikuta wakipoteza fedha zao za pensheni hatua ambayo imewaharakishia vifo wapendwa wao hao pale walipokumbwa na shinikizo la damu kutokana na mshituko.

“Mimi nimekuwa mkulima kwa miaka mingi sana. Kila ambako nimekuwa nikipangiwa kuwa kituo changu cha kazi nimekuwa pia nikiendesha shughuli za kilimo. “Nimewahi kufanya kazi Kyela, huko nilikuwa najishughulisha na kilimo cha mpunga. Kwa upande wa Rungwe (Tukuyu) nimekuwa nafanya shughuli za kilimo cha mazao mbalimbali kama ndizi, viazi mviringo na mahindi.

“Hata hivyo kilimo changu kwa miaka yote kimekuwa kilimo cha kuganga njaa, yaani kilimo ambacho hakinifanyi kwenda sokoni badala yake natumia mazao ambayo nimezalisha mwenyewe kwa nguvu zangu. “Kilimo cha Kyela kilikuwa kinanifanya nisinunue mchele,” anasema Gredah ambaye kabla ya kuwa Ofisa Tarafa amewahi kushikilia wadhifa wa Mtendaji wa Kata katika maeneo mbalimbali ikiwemo katika vilima maarufu vya mjini Mbeya vya Kawetele.

Akizungumzia ni kwanini ameamua kutupia jicho katika sekta ya kilimo, kama kimbilio lake baada ya kustaafu Gredah anasema; “ Unajua Mungu amempa kila mtu shughuli ya kufanya. Mimi naamini Mungu amenipangia kilimo kuwa shughuli yangu kuu.” Anasema anaamini hilo kwa vile licha ya mpunga aliolima katika eneo la ekari 10, kijijini Namawala, Ifakara mkoani Morogoro katika miaka ya hivi karibuni kusombwa na maji, kutokana na mvua kubwa iliyonyesha, hawezi kuondoa dhana kuwa kilimo ndio mkombozi kwake baada ya kustaafu.

“Hili suala lilinivuruga sana kichwa. Ilifikia mahali nikasema silimi tena mashamba makubwa ya mbali, nitaendelea kulima kilimo cha kuganga njaa. Kaka yangu Edward Mwakyembe (Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mawasiliano wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar) alinitia moyo. “Yeye ndiye aliyenihamasisha kuja huku Malinyi, Aliniambia kaka yako (Marcelin Ndimbwa- Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi) yupo huko na wana skimu nzuri sana ya umwagiliaji ambayo unaweza kulima kwa mwaka mzima. “Baada ya kukubaliana naye, nikaja hapa katika Skimu hii ya Umwagiliaji ya Itete nakumbuka ilikuwa mwezi wa nane. Nikakuta watu wanapanda mpunga, nikavutiwa, nikasema likizo yangu ya mwezi wa 11 nitakuja kutafuta mashamba na kulima,” anasema.

Tofauti ya Kilimo na Biashara Akizungumzia tofauti iliyopo baina ya kilimo na biashara anasema kwake anaona biashara ni ngumu zaidi kuliko kilimo na ni vigumu kwa mtu asiyejua kanuni za biashara kuweza kufanikiwa, tofauti na ilivyo katika kilimo.

“Biashara ya kawaida nimewahi kujaribu. Tuna kikundi chetu kinaitwa Weyambe Group. Kupitia kikundi hiki tumekuwa tunafanya biashara mbalimbali ikiwemo usindikaji wa mvinyo wa ndizi, tangawizi, limao, nanasi na pia tumekuwa tunasindika unga,lakini bado haioneshi mwanga kama ni eneo salama kwa fedha zangu za pensheni, sana sana inasaidia tu katika kulipa ada za watoto,” anasema.

Akizungumzia malengo yake ya kilimo kwa msimu huu, katika Skimu ya Kisasa ya Itete, Gredah anasema ni kulima ekari 10 ambazo zitampa mwanga wa kujua kama ni eneo sahihi kwake kuweza kutulia na kuendelea na shughuli za kilimo kwa maisha yake yote.

“Hivi sasa hakuna tena maisha ya longolongo, ili upate fedha ni lazima ufanye kazi kwa makini. Naona kuwa watu sasa wanafuata mkumbo tu kwa kulalamika kuwa fedha hakuna, lakini ukweli ni kwamba waliokuwa na fedha sio sisi, sisi tulikuwa tunapata upepo tu wa fedha walizokuwa wanazipata hao wajanja wanaolalamika.” “Ilikuwa inanishangaza sana naona kwenye WhatsApp watu wanajaza fedha kwenye ndoo, kwa njinsi walivyokuwa wanacheza na dili za ujanja ujanja, maisha hayo sasa hakuna, ni lazima kujituma na kufanya kazi. Nchi hii watu wameihujumu sana, sasa ngoja tufuate maadili,” anasema.

Anasema kamwe hataki kuona anakumbatana na matatizo kama ya wastaafu wengine ambao baada ya kulipwa pensheni zao walijikuta wameingia katika miradi ambayo iliwasababishia hasara kubwa na kuwapa umasikini wa kudumu.

“Unashangaa mtu anastaafu ananunua teksi au daladala. Baada ya siku mbili unasikia pancha, siku mbili hiki na kile vimeharibika, mara baadaye kuku wananza kutagia katika teksi au daladala yako. “Afadhali hata kununua pickup ambayo unaweza kuitumia kwa kazi za shamba na ujasiriamali mwingine katika sekta ya kilimo,” anasema. Kuhusu maisha yake, Gredah mama wa watoto sita, watano wa kike na mmoja wa kiume, alizaliwa Mei 13, 1958 katika Kisiwa cha Mafia kilichopo mkoani Pwani, ambako baba yake alikuwa mtumishi akifanya kazi ya askari polisi.

Baadaye alipata elimu ya msingi katika Shule ya Msingi Mwela iliyopo Kisiwani Zanzibar alikohitimu darasa la saba mwaka 1972. Anasema kusoma kwake huko kulitokana na baba yake kuhamishiwa huko ambako alifanya kazi na kuishi kwa muda mrefu wa maisha yake. Kwa upande wa elimu ya sekondari, anasema aliipata katika Shule ya Sekondari ya Langoni iliyopo Shirati mkoani Mara na kuhitimu Kidato cha Nne mwaka 1976 na mwaka 1979 alianza utumishi katika Shirika la Biashara la Mkoa (RTC) Mbeya.

Tukio la kukumbukwa Akizungumzia tukio ambalo hawezi kulisahau katika safari yake ya utumishi wa umma, Gredah anasema ni lile lilitokea muda mfupi baada ya kuhitimu elimu yake ya Kidato cha Nne ambapo alikwenda Karagwe mkoani Kagera kwa kaka yake ili kutafuta kazi na kufanikiwa kupata kazi ya ukarani serikalini Bukoba Mjini. “Nakumbuka baada ya kupata kazi ile ya ukarani sasa nikawa narudi Karagwe kwa marehemu kaka (bila kumtaja), kuchukua nguo nianze maisha ya kuajiriwa.

Sasa wakati tupo eneo la Zam Zam Kashai, tukasikia kishindo cha bomu. “Hilo lilikuwa bomu la kwanza kurushwa katika ardhi ya Tanzania na majeshi ya Nduli Idd Amin Dadaa, mkoani Kagera katika harakati zake zilizoshindwa za kupora kipande cha ardhi ya Tanzania. “Kazi ikaishia hapo hapo, baada ya hapo tukachukuliwa tukawekwa mafichoni na askari wetu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania.

“Baada ya hapo tukasafirishwa hadi Mwanza na baadaye kila mtu akapelekwa nyumbani kwao, mimi nikarudishwa Mbeya, na baadaye ndiyo nikajiunga na RTC, na kufanya kazi sehemu mbalimbali kama Chunya kule Mkwajuni na Kyela. “Baada ya miaka miwili mitatu ya kufanya kazi RTC nikaamua kuacha na kuomba kazi ya Katibu Kata, na baadaye Ofisa Tarafa na Katibu Tarafa ambao sasa wanajulikana kama Maofisa Tarafa,” anasema.

Huyo ndiye Gredah Mwakyembe, Ofisa Tarafa wa Tarafa ya Tukuyu Mjini ambaye ana uhusiano wa kiukoo na Waziri wa Sheria na Mambo ya Katiba, Dk Harrison Mwakyembe, na undugu wa tumbo moja na mwandishi wa habari mwandamizi wa mkoani Mbeya, Felix Mwakyembe.