GRACE MBOWE: Mpishi mwenye ndoto ya kumiliki mgahawa Marekani

GRACE Mbowe (40) ni mwanadada wa Kitanzania anayeishi Marekani akifanya shughuli zake mbalimbali zinazoweza kumuingizia kipato, ikiwemo upikaji wa vyakula vyenye asili ya Kitanzania.

Mwanadada huyo amekuwa akipika kwa oda maalumu katika shughuli mbalimbali za watanzania na wageni ambao wamekuwa wakifurahia vyakula hivyo. Grace anayejinasibu kupenda sana shughuli za mapishi, anaeleza kuwa na ndoto ya kumiliki mgahawa wa kisasa nchini humo utakaokuwa ukipika vyakula vya kitanzania na kufanya chapati, vitumbua na sambusa ziingie na kuuzwa katika maduka makubwa nchini humo ‘supermarkets’ nchini humo.

Mbowe anaeleza kuwa yeye anapenda sana kupika kwani tangu akiwa mdogo yaani kwa umri wa miaka minne hadi mitano alikuwa akicheza michezo ya kujipikilisha kwenye makopo kwa kutumia moto na kuungua kisha kuchapwa na mama yake aliyekuwa akimkataza kuchezea moto, lakini hakuacha.

Anasema kabla hajaamua kuishi nchini Marekani, aliwahi kujishughulisha na upikaji chakula katika vibanda yaani Mama Lishe na kwa mama yake aliyekuwa akimiliki mgahawa wake mkoani Arusha karibu na kituo kikubwa cha mabasi ambapo alikuwa akipika chakula na kupata wateja wengi. Grace ni mzaliwa wa mkoa wa Kilimanjaro na kabila lake ni Mchaga aliyeishi miaka mingi mkoani Arusha na baadaye nchini Marekani, alikoanza kuishi akiwa na miaka 28 na ni mama wa watoto wawili.

Anaeleza kuwa kutokana na kupenda kupika, anapokuwa jikoni anakuwa huru sana na kufurahia kupika huku akiwa hapati tatizo lolote au kuchoka kupika. Anasema mwaka 2004 alipofika nchini humo kutokana na masuala yake binafsi hakuweza kujishughulisha na masuala ya kupika, lakini hata hivyo alifanya kazi katika mgahawa mmoja katika mji wa New York pamoja na kusimamia uendeshaji wa Subway Fast Food.

Anasema lakini baada ya kupata vibali vyake vya kuishi nchini humo aliamua kusoma kwa kuongeza ujuzi katika fani yake ya Dawa (medical field), hivyo alipomaliza ili kujiongezea kipato akaanza kufanya kazi mbili ili aweze kusomesha watoto wake aliokuwa amewaacha nchini Tanzania wakati huo na ilipofika mwaka 2010 aliwachukua watoto wake na kuanza kuishi nao nchini humo.

Grace anasema watoto wake kwa sasa wako vyuo vikuu hivyo anaendelea kufanya kazi hiyo ya kawaida ambayo anakiri siyo anayopendelea kama kupika lakini anaifanya kwa ajili ya kuwasaidia watoto wake na kuweza kukidhi mahitaji yake ya kila siku kama kulipa tozo mbalimbali.

Lakini anakiri kuwa kila siku roho yake inamsuta na kujisikia vibaya kwa kutoendeleza kipaji chake cha kupika kwa kuwa na sehemu maalumu lakini anakwamishwa na pango kubwa inayotozwa kwa ajili ya kuweka mgahawa kwani bei zao ni kuanzia Dola za Marekani 6,000 hadi 10,000 kwa mwezi. Mwanadada huyo anasema pango hilo ni kwa maeneo ya miji ya New York au Washington Dc ambako ndiyo maeneo mazuri kwa vyakula vya aina ya kitanzania kutokana na kuwa na watu wengi wanaopenda kujaribu aina tofauti za vyakula vya asili, hivyo aliamua kuanza kupika nyum- bani kwake anapoishi.

Anasema katika jimbo analoishi Pittsburgh, Pennsylvania hakuna watanzania wengi, wengine ni wanafunzi wakati raia wa Kenya ni wengi kuliko watanzania, hivyo amekuwa akipika kulingana na oda anazopata kwa watu wenye shughuli mbalimbali. Grace anasema kutokana na changamoto hiyo hawezi kujitangaza sana na kwa sasa ana wateja wachache wanaoweka oda wakiwa na sherehe ndogo kama ‘baby showers’ au kumbukumbu ya siku ya kuzaliwa ambapo kila wakati amekuwa akiongeza idadi ya wanaohitaji kutokana na uzuri wa vyakula vyake.

Anasema ingawa wapo wanaolalamika kuwa bei ni kubwa lakini akishakula chakula chake hukisifia kwani aliishaweka viwango maalum vya upikaji wa vyakula vyake. Grace anasema kutokana na kutokuwa na sehemu maalumu wala leseni hawezi kujitangaza kwa wazungu isipokuwa lengo lake kubwa ni kutangaza chakula cha nchini kwa baadhi ya watu anaowafahamu ili wafahamu kisha atakapopata eneo maalumu atapata wateja wengi zaidi.

Anasema kwa baadhi ya wazungu anaofahamiana nao na aliowahi kuwaonjesha chakula cha kitanzania wamekipenda sana na kumshauri kamwe asiache kupika ila aweke mikakati na kujitanua kwa kuwa na eneo maalumu kwa ajili ya kupika kila wakati ili wengi zaidi wapate nafasi ya kuonja na kula chakula hicho.

Katika kuonesha ana dhamira ya kweli kum wezesha kuwa na eneo maalumu kwa ajili ya kupika chakula hicho ameanza shule ya upishi kwa ajili ya kujiendeleza huku akiwa amesajili jina la “Kilimanjaro Kitchen” ili kulihifadhi kwa ajili ya nyakati zijazo akiwa na eneo lake kama mipango yake ikienda vile alivyopanga. “

Sasa hivi nafanya tu kazi kwa bidii na kujiweka sawa, huku nikiendelea kufanya utafiti nihamie jimbo gani ili nikaendeleze biashara yangu kutokana na kuwa jimbo hili ninaloishi sasa siyo rafiki kwa biashara hii, kwani nilihamia huku kwa ajili ya shule za watoto lakini sasa ninampango wa kuhama,“ anasema.

Grace anasema anafikiri kuhamia jijini New York kwa sababu ndiyo eneo nzuri kwa biashara kama hiyo, pamoja na kukamilisha ndoto yake ya kutaka vitumbua ,chapati na sambusa vinauzwa katika ‘supermarket’ kwa kuzisambaza yeye mwenyewe baada ya kupika ili kujiongezea wateja zaidi.

“Najua sio rahisi lakini nataka ndoto yangu hii iendelee kuishi na niitimize kwa sababu naamini kuwa nitafanikiwa siku moja,” anaeleza. Kwa mujibu wa Grace, anapendelea kupika vyakula vyote anavyovijua vya kitanzania isipokuwa mapishi kama sambusa yanayochukua muda mwingi zaidi anauza moja dola za Marekani mbili pamoja na chapati lakini maandazi ni bei tofauti kulingana na upishi wake kutochukua muda kama hivyo vingine.

Anasema viungo kwa ajili ya vyakula kama pilau ananunua katika duka kubwa linalojulikana kama ‘Indian Store’ wakati unga wa mahindi na ndizi anapata katika maduka ya ‘Spanish Stores’. Grace, mama wa watoto wawili wenye umri wa miaka 19 na 23 anakataa kuwaelezea zaidi anasema anapendelea sana kusikiliza nyimbo za bongo flava hususan zinazoimbwa na mwanamuziki Nassib Abdul maarufu Diamond Platnumz’.