Teknolojia inamkutanisha dereva na abiria

TEKNOLOJIA ya Habari na Mawasiliano (Tehama) inaendelea kushika kasi kila kukicha, huku vijana wakiwa wamehamasika zaidi katika kubuni mbinu zinazotoa mbadala wa changamoto mbalimbali nchini. Mbinu mbalimbali za kiteknolojia zimebuniwa na hasa zaidi zikiwa zenye kulenga kutoa majibu kuhusu taarifa mbalimbali.

Kijana mbunifu Justine Kashaigili ni mmoja kati ya vijana ambao wametumia teknolojia na kuja na mbinu mbadala zenye kulenga kutatua kero ya usafiri hapa nchini.

Kashaigili mwenye umri wa miaka 24, anasema kwa sasa sehemu mbalimbali hapa nchini kumekuwa na changamoto kadhaa za usalama wa watumiaji wa huduma za usafiri.

Anasema huku usafiri mkubwa ukiwa ni wa teksi, bajaji na pikipiki maarufu bodaboda bado aina hiyo ya usafiri inakabiliwa na changamoto kadhaa.

Ubunifu wake Kashaigili kwa sasa amebuni mbinu ya kiteknolojia, App iitwayo Twende ambayo inamkutanisha abiria na dereva wa usafiri kirahisi zaidi.

Abiria akitumia simu yake ya kisasa aina ya Smartphone anaweza kupakua huduma hiyo kwenye Google play store na kisha kujisajili ili kutumia huduma hiyo.

Kwa kufanya hivyo anakuwa ameunganishwa na dereva wa teksi, bajaji au bodaboda ambaye anakuwa karibu na eneo alipo na kisha anaweza kuwasiliana naye kirahisi na kukubaliana bei.

Kijana huyo ambaye hadi sasa ameajiri watu sita wanaoshirikiana naye katika kutoa huduma hiyo, anasema baada ya kubaini ukubwa wa tatizo hilo ambalo aliliona tangu akiwa chuoni, aliumiza kichwa katika kutafuta njia mbadala zenye kulenga kukabiliana na tatizo hilo.

Mhitimu huyo wa Shahada ya Sayansi ya Kompyuta, DT 228 kutokea Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) anasema tangu akiwa mwaka wa kwanza chuoni hapo huo ukiwa mwaka 2011, alikuwa akikerwa na changamoto za usafiri unaowakumba wakazi wa jiji.

Anasema hali hiyo ilikuwa ikimkera na hasa zaidi wakati akiona wananchi wakiwa wanasumbuliwa kujadiliana bei na watoa huduma za usafiri.

"Najua, mtu anaweza kusimamisha teksi au bajaji na hapo ndipo anaanza kujadiliana bei, wakati huo huo muda unakuwa unapotea wakati wakijadiliana bei, lakini pia kama mtoa huduma akikataa kuafiki bei iliyopendekezwa basi mteja anakuwa hana jinsi nyingine zaidi ya kuendelea kungojea usafiri mwingine," anasema kijana huyo.

Wazo lilipotokea Anasema wakati akiwa chuoni hapo akiendelea na masomo yake, alianza kutafuta mbinu mbadala ya kutatua kero hiyo na kwenye andiko la mradi wake kabla ya kutunukiwa shahada, aliamua kubuni mradi unaolenga kujibu kero hiyo.

Anaweka wazi kuwa wakufunzi pamoja na wataalamu kutoka Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), walipenda wazo lake hilo na kumsihi kujiunga na mradi wa DTIB ulio chini ya Tume hiyo unaolenga kuendeleza mawazo endelevu ya kiteknolojia kwa vijana.

Anasema alipomaliza chuo mwaka 2015 alikwenda moja kwa moja kwenye ofisi za mradi huo ambapo alitumia mwaka mzima kujifua ili kuhakikisha kuwa wazo lake linatimia. Mwaka wote wa 2016 ulikuwa ni mwaka wa kufanyia kazi wazo lake hilo, huku akishirikiana na wataalamu wa tume hiyo hasa waliopo kwenye mradi wa DTIB.

Namna ya kuitumia

Anasema kwa sasa mradi wake umeshatoka kuwa wa makaratasi na umeingia kwenye utendaji zaidi ambapo anaongeza kuwa kwa sasa wananchi wameshaanza kuutumia.

Anafafanua kuwa, kwa kuwa kila mtu ambaye anakuwa amepakua huduma hiyo kwenye simu yake, ana uwezo wa kumuona dereva yeyote wa bajaji, bodaboda au teksi anayekuwa yupo karibu yake kwa wakati huo na hivyo anakuwa na wigo mpana zaidi wa kujadiliana bei na yeyote.

Kashaigili anasema tofauti na ilivyokuwa awali ambapo mteja alikuwa akilazimika kusimamisha mtoa huduma na kujadiliana bei, kwa sasa anaweza kufanya hivyo kwa simu yake ya mkononi moja kwa moja. Watumiaji

Anasema kuwa tayari bajaji 1,500, teksi 1,000 pamoja na bodaboda 50 zimeshajiunga na huduma hiyo, huku kwa upande wake akishirikiana na wafanyakazi wake wamejipanga kuhakikisha huduma hiyo inawawezesha watanzania.

Kashaigili anasema abiria hatalazimika kumpatia fedha mtoa huduma ya usafiri iwe bajaji, teksi na bodaboda ila atafanya malipo yake moja kwa moja kwenda kwenye akaunti maalumu ya Twende ambao ndio wana jukumu la kumlipa mtoa huduma.

Anasema hiyo inasaidia zaidi kudumisha huduma iwapo wangekuwa wanalipwa moja kwa moja huenda ingekuwa shida. Kijana huyo anasema kuwa ofisi ya Twende ndiyo itakayopokea fedha hizo na kisha kuzilipa kwa mtoa huduma, lakini hata hivyo anasema kwa mteja ikifikia Sh 50,000 anaweza kupewa fedha yote.

Twende App hivi sasa inatoa mbadala sahihi wa malipo kupitia Tigo Pesa kwa namba binafsi za Tigo Pesa kwa madereva na inapatikana katika mfumo wa Android na hivi karibuni itapatikana kwa watumiaji wa simu zilizo na mfumo wa iOs.

“Nimesukumwa na kasi ya maendeleo ya miundombinu na nguvu ya ujasiriamali hapa nchini.

Ninategemea kuwapatia wakazi wa jiji la Dar es Salaam chaguo wanalolimudu, rahisi na linalofaa kwa ajili ya usafiri salama.” Anasema malipo hayo yanafanywa kwa njia ya Tigo Pesa na mteja anaweza kutumia simu yake hiyo katika kutoa maksi kuhusu mwenendo mzima wa mtoa huduma huyo na kwa wale ambao watalalamikiwa kampuni yake itawaondoa kwenye usajili wao kwenye huduma hiyo ya Twende.

Historia yake Kijana huyo alisoma shule ya msingi Kyazi iliyopo Misenyi Bukoba mkoani Kagera kuanzia mwaka 1998 hadi 2004 alipomaliza darasa la saba kabla ya kujiunga na Sekondari mwaka 2005 hadi mwaka 2008 katika sekondari ya Chang'ombe, jijini Dar es Salaam kwa masomo ya kidato cha kwanza hadi cha nne.

Mwaka 2009 hadi mwaka 2011 alijiunga na masomo ya kidato cha tano na sita sekondari ya Tosamaganga ambapo ndipo mapendo ya masomo ya sayansi yalipoanzia.

Wasemavyo wadau waliomsaidia Kashaigili anasema kuwa kutokana na ubunifu wake huo, amepata ushirikiano kutoka kampuni ya Tigo ambayo imemdhamini kwa njia mbalimbali.

Mkuu wa Zana za Kidijitali wa Tigo Tawonga Mpore anasema,

“Huduma hii ni kielelezo cha Tigo kujikita katika mageuzi ya mtindo wa maisha ya kidijitali kwa kutoa suluhisho kwa changamoto zinazowakabili watumiaji wa usafiri wa nchi kavu".

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Dk Hassan Mshinda, alisema huduma hiyo ni ya pili kutolewa na tume hiyo ambapo mradi wa kwanza ni Tigo Backup iliyobuniwa na kijana wa miaka 24, Godfrey Magila.