CHEF ISSA

UNAPOTAKA kuzungumzia mafanikio ya Watanzania wanaoishi na kufanya biashara katika mataifa ya ughaibuni, ni vigumu kutomtaja Issa Kapande maarufu kama Chef Issa.

Chef Issa ni mmiliki wa mgahawa mkubwa unaotoa huduma za chakula cha Kitanzania uliofunguliwa nchini Sweden Novemba mwaka jana.

Kinachomfanya kuwa Nyota mbali ya ukubwa na mafanikio ya mgahawa huo katika siku za hivi karibuni, ni mgahawa huo kuanza kutumika katika kutoa maelezo na taarifa za utalii kwa watalii kutoka Sweden wanaopanga kutembelea Tanzania, hatua ambayo inatajwa kuwa italeta manufaa makubwa.

Balozi wa Tanzania nchini Sweden, Dora Msechu ndiye aliyewaongoza Watanzania katika tukio hilo muhimu katika kupeperusha bendera ya Taifa letu kuzindua mgahawa huo wa Chef Issa.

Balozi Msechu alimpongeza Issa Kapande na mkewe kwa kufanikisha kuwapo kwa mgahawa huo ambao umeweka rekodi kuwa mgahawa mkubwa kuliko yote ya Kiafrika katika nchi za Ulaya.

Aidha, alimshukuru Torvald Brahm mwenyeji wa mji huo kwa kumuunga mkono Issa hadi kufanikisha ndoto yake ya kuwa na mgahawa wa kwanza wa Kiafrika katika mji wa Trollhattan utakaotoa huduma ya chakula cha kitanzania.

Katika uzinduzi huo ambapo wenyeji wa manispaa hiyo akiwemo Meya na Mwenyekiti wa Trollhattan, Paul Akerlund na msaidizi wake Peter Eriksson walikuwepo, balozi ambaye ndio kwanza alikuwa ameanza kazi hiyo nchini Sweden alielezea kufurahishwa na juhudi za Chef Issa.

Balozi Msechu akitoa pongezi zake alisema; “Issa ameonesha njia kwamba inawezekana kwa watu waliopo ughaibuni sio tu kuajiriwa, bali kujiajiri katika nyanja mbalimbali. Alisema hilo linawezekana kutokana na kufuatilia kwa karibu taratibu za wenyeji na kisha kutumia mafunzo yaliyopo kukamilisha ndoto.

“Ni dhahiri kuwa, Chef Issa kwa kupitia taaluma yake ya upishi amewezeshwa kumiliki mgahawa huu hapa Trollhattan, Sweden kwa hilo, napenda tuishangilie na kuipigia makofi Sweden na Trollhattan.”

Alisema anampongeza kijana huyo ambaye pia amewekeza mkoani Mtwara. Katika mahojiano, Mpishi Mkuu Issa Kapande alisema mafanikio yake yanatokana na juhudi kubwa na nia aliyoiweka katika kujifunza na kufundisha wengine katika mitandao ya wapishi wakuu.

Anasema akiwa amefanya kazi katika nchi 17 na tayari akiwa na vitega uchumi nchini, alianzia nia ya kuwekeza Sweden mwaka 2009 wakati alipohamia nchini humo akitokea Uswisi. Anasema alianza kwa kuomba vibali, lakini mchakato kamili ulianza mwaka 2013.

”Tulilazimika kufanya utafiti kidogo,” alisema na kuongeza kuwa katika utafiti huo walihoji watu 300 na kujua mwelekeo hasa wa shughuli yao unastahili kuwaje.

Kapande ambaye ni mhitimu wa Chuo Kikuu cha Manchester Metropolitan na Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Menejimenti ya Hoteli cha Uswisi, amesema amepambana vikali na mkewe hadi kufikia hatua ya kuanzisha mgahawa huo ambao upo katika eneo la ukubwa wa mita za mraba 810.

Kapande ambaye mwaka jana alitwaa tuzo ya dhahabu katika upishi akiwa na timu ya Sweden Magharibi alisema kuna umuhimu mkubwa kwa wapishi wa nyumbani kukubali kubadilika na kufanya kazi kwa pamoja kwa lengo la kujifunza na kufunza ili kuwa na aina nyingine ya mapishi katika Nyota wa wiki CHEF ISSA Kasi yake kuitangazakuendeleza sekta.

Pamoja na uhodari wa kupika vyakula mbalimbali, ndani ya mgahawa huo pia watu mbalimbali wanapatiwa taarifa za utalii Tanzania, hatua ambayo inasaidia kwa kiwango cha juu sana katika kukuza na kutangaza utalii wa Tanzania.

Watu maarufu waliopikiwa na Chef Issa Ingawa ni kipindi kifupi kimepita tangu mgahawa huo uzinduliwe rasmi na kukiwa hakuna viongozi maarufu waliobahatika kufika, Chef Issa mwenyewe amepata sifa ya kuwapikia chakula watu mbalimbali maarufu duniani katika maisha yake ya upishi.

Chef Issa katika kazi yake ya upishi, amebahatika kuwapikia watu mashuhuri duniani, baadhi wakiwa Andrew Young, Mchungaji Jesse Jackson, Robert Mugabe (Rais wa Zimbabwe), Paul Kagame (Rais wa Rwanda), Benjamini Mkapa (Rais mstaafu wa Tanzania), Raila Odinga (Waziri Mkuu wa zamani wa Kenya), Daniel Arap Moi (Rais wa zamani wa Kenya), Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje wa Marekani, Hillary Clinton na mumewe Bill Clinton, mke wa Rais wa zamani wa Marekani, Laura Bush.

Wengine ni Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein, mwigizaji Chris Tucker, Rais wa zamani wa Afrika Kusini, Mzee Nelson Mandela (sasa marehemu), Koffie Olomide, Youssour ndour, Arsene Wenger (Kocha wa Arsenal ya England), Gianluca Vialli (nyota wa zamani wa Italia aliyewahi kuichezea na kuinoa Chelsea ya England), Rais wa Congo DRC, Joseph Kabila, Billy Gates na wengine wengi.

Chef Issa akishirikiana na ma-Chef wa timu ya Stockholm, Sweden, waliwahi kushiriki na kushika nafasi ya kwanza katika kipengele cha timu za kanda kwenye mashindano ya Kombe la Dunia la Mapishi mwaka 2014 yajulikanayo kama Villeroy & Boch Culinary World Cup yaliyofanyika Luxemborg.

Huo ulikuwa ni mwanzo wa Chef Issa kutambuliwa kuwa ni mpishi maarufu duniani na hivyo kuanza kuzungumzwa na mahoteli makubwa na yenye hadhi kubwa duniani.

Mafanikio hayo hayakupita kimya kimya, bali aliyekuwa Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete alijitokeza na kumpongeza Chef Issa alipofanya ziara nchini Sweden Desemba 2014.

Mbali ya hilo, ushindi huo ulimfanya Chef Issa kupewa mwaliko maalumu wa kibalozi katika Ubalozi wa Tanzania Sweden, ambapo Balozi Msechu na wafanyakazi wa ubalozi walimpokea gwiji huyo wa upishi kwa furaha na kumpa huduma za hali ya kibalozi.

Ni kipindi hicho na katika historia ya nchi ya Sweden, uongozi wa Kanda ya Mkoa wa Trollhattan uliamua kufika katika mgahawa wa Chef Issa na kula chakula cha mchana chenye hadhi ya Kitanzania, tukio ambalo linadaiwa kuweka historia mpya kwa vyakula vyenye asili ya Afrika kuanza kupendwa na kukubalika kwa kasi nchini Sweden.

Aidha Jarida la Wizara ya Maliasili, Makumbusho na Utalii katika mji wa Trollhattan na Vanersborg wameamua kuijumuisha Tanzania Restaurant ya Chef Issa kwenye orodha ya migahawa bora kwenye miji hiyo miwili, huku jarida la biashara na uwekezaji la Fokus Vast limethibitisha rasmi na kupongeza mgahawa huo kuwa ni mgahawa sahihi kwa mapishi ya kiafrika na Kitanzania.

Tukio la kukumbukwa Mnamo Oktoba 22, 2015 kijana mmoja wa Kiswidishi alivamia shule ya Krona iliyopo mji wa Trollhatan uliopo jirani na mji wa Goteborg ambao ni mji wa pili kwa ukubwa nchini Sweden.

Kijana huyo alivamia shule hiyo akiwa amevalia mavazi ya Halloween na kuanza kuchoma visu watoto. Alifanikiwa kuchoma visu walimu wawili na watoto wawili na maaskari wawili kabla ya polisi kumpiga risasi na kumuua dunia hapo hapo.

Watu aliowajeruhi walikimbizwa hospitali ambapo mwalimu mmoja na mwanafunzi mmoja walifariki dunia na wengine walipona. Baada ya kumpekua, Polisi walikuta barua yenye maelezo na sababu ya huyo muuaji kuamua kufanya hivyo.

Aliandika kuwa nimeamua kufanya mauaji haya kwa sababu sikubaliani na serikali yangu kwa sasa kukubali wimbi la wahamiaji kuongezeka. Hali kwa sasa imekuwa tete ambapo karibu kila wiki kwa nyumba wanayoishi wahamiaji imekuwa ikichomwa moto au kambi waliyokuwa wamehifadhiwa wakimbizi kutoka Sirya.

Oktoba 33, 2015 ndio yalikuwa maziko ya kijana huyo wa Kiafrika aliyeitwa Ahmed Hassan aliyefariki katika mauaji hayo ya kibaguzi na kuzikwa na maelfu ya watu kutoka ndani na nje ya Sweden.

Baada ya maziko na huduma za chakula cha mchana kilichoandaliwa na Tanzanian Restaurant kwa wageni maalumu tu ambao walifikia 1,000, walaji wote waliuzungumzia mgahawa huo kuwa chaguo sahihi kwa mapishi ya kiafrika.

Miongoni mwa walioshiriki chakula hicho ni Waziri wa Elimu wa Sweden, Gustav Fridolin, Meya wa Jiji la Trollhattan, Paul Akerlund Mohamed Adulahi Mohamedi maarufu kama “Farmajo’ ambaye alikuwa Waziri Mkuu wa Somalia kati ya mwaka 2010 na 2011 ambaye hivi majuzi amechaguliwa kuwaRais mpya wa Somalia.