Vijana: Kuna maisha baada ya sikukuu

OYA Masela! Leo bila shaka hakuna asiyejua ni siku gani, na bila shaka kila mmoja alisha jiandaa kinamna yake katika kuungana na ndugu zetu Wakristo duniani kwa kuzaliwa Masiya miaka zaidi ya 2000 iliyopita.

Najua jinsi baadhi yetu tulivyo jiandaa, hapa hakuna ubishi japo vijana wengi mnalalamika maisha ni magumu, lakini leo nikipita pita mitaani katika maeneo yetu ya kujidai ni lazima nitawakuta kibao mkiwa mmechafua meza kwa mazagazaga ya hapa moja baridi pale moto, nyama choma na totoz!! Hahahahaaaa!

Wapo niliowagusa lakini kiukweli sitafurahi sana kuona furaha yetu ya leo inatuingiza katika matatizo ambayo tutayajutia katika siku zote za maisha yetu. Furaha ya leo ikafanye wale ndugu, jamaa na maraki wakabaki na majonzi kama ambayo leo hii mimi ninayo kwa juzi tu kumpoteza raki yangu na jamaa yangu wa karibu Mpoki Bukuku aliyefariki kwa kugongwa na gari.

Ningependa vijana wenzangu leo tufanye kila kitu kwa kiasi. Tuwe na staha katika matendo yetu na tusifanye vitu kana kwamba leo ndio mwisho wa dunia na hakuna kesho ila tukumbuke hizi siku kuu zipo kila siku ni vile tu unavyoamua maisha yako yawe.

Siku kama ya leo wapo vijana wengi ambao wamejipanga kufanya maovu ya aina mbalimbali, wapo waliokusudia kunywa vilevi kupita kiasi, wapo ambao wamejipanga leo kwenda kufanya vitendo vya zinaa kwakua tu ni siku kuu lakini mwisho wa yote wapo ambao watafanya hivyo na kujikuta wanaingia matatizoni.

Ni vyema tukaitumia siku ya Krismasi kwa kujiepusha na vitendo vyote viovu ili kesho tuingie katika siku kuu nyingine na mwisho wa siku tukapate nguvu ya kufanya kzi na kulijenga taifa letu.

Daima majuto ni Mjukuu na baada ya kufanya yale maovu tutakayoyafanya leo tutasingizia kuwa ni pombe ilhali si kweli hakuna pombe inayofanya matendo mabaya bali ni wewe mwenyewe uliyefanya hayo kwa ujinga wako.

Tufurahi wote na familia zetu kwa amani na upendo na katu tusishiriki katika uhalifu wa aina yeyote kwani kufanya hivyo kutatuingiza katika mikono ya sheria