Jarida la Wanawake: Tusherehekee siku ya leo na familia

LEO ni Sikukuu ya Krismasi ambapo Wakristo duniani kote wanasherehekea kuzaliwa kwa bwana Yesu Kristo.

Sikukuu ambayo inatambulika zaidi ya kifamilia hivyo hakuna budi leo kukaa na familia na kusherehekea kwa pamoja. Hivyo ni vema wanawake kutumia nafasi hiyo kuandaa mazingira ya watoto na akinababa kuvutiwa kukaa nyumbani kama kuandaa nyumba na vyakula vitakavyoonesha utofauti ndani ya nyumba.

Bila kutumia gharama kubwa ni vema kuandaa mazingira kwa kuyafanya tofauti kwa namna yoyote huku ukifanya maandalizi ya vyakula ambavyo havijazoeleka kula mara kwa mara nyumbani hapo.

Vile vile siku ya leo ni vema kuepuka masuala ya ugomvi na migogoro ila hakikisha nyumba inatawaliwa na amani na upendo wakati wote mkiwa pamoja nyumbani kwa kutolalamika au kutoa maneno yasiyofaa kwa watu wote hapo nyumbani.

Kama inawezekana kwa kushauriana na baba au wanafamilia wengine hapo nyumbani kama mna uwezo wa kutoka nyumbani na kwenda kutembea kwa ndugu jamaa na marafiki au sehemu nyingine kubadilisha hali ni vema kwenda kwa pamoja.

Ni vema katika hili wanawake kutumia nafasi hii kuwashauri akinababa kwa siku hii ya leo kutulia nyumbani na kuachana na kwenda kutembea katika baa na kushindwa kula hata chakula cha mchana pamoja jambo ambalo si sahihi hata kidogo.

Ni vema siku hii kuifanya ya familia kweli na iwapo ikitokea baba amekaidi na kuondoka kwenda kutembea peke yake nje ya nyumbani mama usikubali kujikosesha amani na kuharibu sikukuu yako.

Hakikisha unakaa na watoto wako na ndugu wengine kusherehekea sikukuu hii muhimu kwa familia na kamwe usimkaribishe shetani katika kutengeneza migogoro kwenye familia kwani itasababisha kuanza mwaka bila kuwa na amani jambo ambalo ni hatari kwa mustakabali wa familia na watoto kwa ujumla.