Jicho: Watoto walindwe katika kusherehekea Mwaka Mpya

NICHUKUE fursa hii kukutakia msomaji wa safu hii heri ya mwaka mpya. Ni jambo la kumshukuru Mungu kuona mwaka mwingine.

Wapo ambao mauti yamewafika zikiwa zimesalia dakika chache kuanza kwa mwaka mpya. Lakini kwa wewe ambaye umejaliwa, unapaswa kushukuru sana kwani kuishi kwako ni kwa neema. Ndiyo maana wapo waliokesha kwenye nyumba za ibada wakimshukuru Mungu kwa fursa hii ambayo baadhi hawakubahatika kuuona mwaka mpya.

Lakini pia, wengi wanasherehekea kwa namna tofauti wakiwapo wanaokwenda kwenye kumbi za starehe, ufukweni na wengine kutembelea ndugu, jamaa na marafiki. Wengine wanasherehekea kwa kula, kunywa na hata kuvaa nguo mpya.

Lakini pia wapo ambao huamua kusherehekea kwa kuendelea na kazi mbalimbali za uzalishaji ikiwemo, kilimo, biashara na maofisini. Wakati watu wakisherehekea kwa namna tofauti, nawiwa kutoa angalizo kwa wazazi na walezi juu ya suala zima la ulinzi wa watoto.

Kumekuwapo na matukio mbalimbali ya kusikitisha yanayowakumba watoto wakati wa sherehe kama hizi. Mathalani, tukio la siku ya Krismasi la mwanafunzi wa shule ya Msingi Seke, jijini Arusha aliyepoteza maisha baada ya kuzama majini wakati akiogelea, linatoa funzo kwa wazazi, walezi na jamii kwa ujumla kuwa makini na watoto.

Taarifa zilieleza kuwa, mtoto huyo alifia majini kwenye bwawa la kuogelea katika hoteli moja ya kitalii jijini Arusha. Katika tukio hilo ambalo baadhi ya vyombo vya habari viliripoti kuwa limegubikwa na utata, mtoto huyo mwenye umri wa miaka 12 alikwenda na wenzake kuogelea.

Utata huo unatokana na kuwapo na dhana tofauti; wapo wanaoamini kwamba mtoto huyo alisukumwa na wengine wakidai kuwa alijigonga kwenye ukingo wa bwawa wakati akiruka kwenye maji. Utata mwingine ni wa mtoto huyo kuhama bwawa la watoto na kuingia la wakubwa ambako ndiko inadaiwa alipata ajali.

Kwa ujumla, hili ni tukio lenye simanzi ambalo kwa vyovyote vile, familia haihitaji kutoneshwa kidonda. Polisi pekee ndiyo wenye uwezo wa kuchunguza na kuja na ukweli halisi wa tukio. Matukio ya watoto kuzama wakiogelea wakati wa kusherehekea sikukuu (hasa za kidini na mwaka mpya) pia yamekuwa yakiripotiwa kwa wanaokwenda ufukweni.

Ikiachwa matukio ya watoto kuzama maji wakati wakisherehea, itakumbukwa pia maafa yaliyowahi kutokea mkoani Tabora ambako watoto wapatao 20 walipoteza maisha wakati wa kusherehekea Idd el Fitr baada ya kukosa hewa kwenye disko toto. Pia tumekuwa tukishuhudia watoto wanaotangazwa baada ya kupotea wakiwa mitaani kusherehekea.

Sina lengo la kukumbusha matukio yenye simanzi katika siku kama hii ambayo watu wanafurahia kuuona mwaka, isipokuwa, inanibidi nifanye hivyo katika kuonesha namna ambavyo jamii inapaswa kuwajibika kuhakikisha sikukuu hazitengenezi kumbukumbu ya machozi. Ni wajibu wa wazazi kuwa karibu na watoto wanapokuwa mbali na maeneo ya nyumbani .

Haiingii kichwani kuona watoto, tena wa chini ya miaka 10, wakiwa kwenye kumbi za starehe, ufukweni, barabarani na maeneo mengine ya kusherehekea bila uangalizi wa wazazi. Nakubaliana na msemaji wa Jeshi la Polisi, Advera Bulimba ambaye hivi karibuni, alikaririwa akisema, wazazi ambao watoto wao watapotea katika kipindi cha sikukuu watalazimika kuisaidia polisi ikiwamo kutoa maelezo ni kwa nini wamepotea.

“Tutawaita watusaidie wakati watoto wanapotea wao walikuwa katika mazingira gani,” alikaririwa Bulimba akisema na kuthibitisha kuwa, imekuwa ni kawaida kipindi cha sikukuu vituo vya polisi vinajaa watoto waliookotwa katika maeneo mbalimbali, ikiwamo fukwe za bahari. Wakati nikiendelea kuwatakia watu wote mwaka mpya wenye furaha na mafanikio, pia niendelee kusisitiza wazazi na walezi kuwa ulinzi wa watoto uko mikononi mwao.

Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.