POROJO za anko Sagati: Tusake kizazi kwa Wabrazili, tutakenua kisoka

KATIKA habari ambazo zilivuta wasomaji duniani ni ile iliyosema kuwa timu ya mpira wa miguu ya Wanawake ya Zimbabwe imekubali kwenda Brazili, lengo la safari hiyo ni kwamba wanawake hao wakafanye mapenzi na wanasoka nguli wa Brazili ambao wamestaafu.

Lengo la kufanya hivyo ni kwamba ili wapate kizazi cha mpira cha Wabrazili. Na wanawake 10 wakiwemo watano ambao wanacheza kwenye timu ya taifa ya wanawake wamekubali kwenda huko na Serikali ya Rais Robert Mugabe itagharimia safari hiyo kwa kipindi chote wanawake hao watakapokuwa huko Brazili.

Zimbabwe ina mkakati wa kujenga kizazi cha mpira na mojawapo ya mbinu wanazotumia ndio hizo za kuhakikisha kwamba wanapata kizazi kutoka Brazili ambako soka ndio chakula chao cha kila siku. Chama cha soka cha Zimbabwe (ZIFA) kimethibitisha hilo kwamba hayo ni makubaliano ambayo yalifikia kati ya chama hicho na mamlaka za Brazili.

“Tunafurahi kwa hatua ya wanawake hawa 10 kukubali kusafiri kwenda Brazili chini ya mpango wetu wa kujenga kizazi cha mpira wa miguu. Hatua hii tumeichukua baada ya kushauriwa na daktari wetu wa timu ambaye alishauri tutafute kizazi cha Wabrazili. Wanawake wote hao wamefanyiwa vipimo vya afya wako salama na namna gani watoto wao watatunzwa hilo tutazungumza na mama zao,” alisema Philip Chiyangwa mmoja wa maofisa wa ZIFA.

Habari hii ilinivutia sana sio kwa sababu tu kwamba wanawake hao wameamua kwenda kula raha huko Brazili. Ila ubunifu walioufanya wenzetu hawa wa Zimbabwe ambao naamini ndoto yao ni kuhakikisha siku moja na wao wanacheza kombe la dunia.

Ni habari kidogo ya kuchekesha, lakini nadhani na sisi tunaweza kuwaiga Wazimbabwe, kwamba tuwapeleke dada zetu Brazil ili mradi tu tuwaambie wawe macho na Zika, lakini lengo wajamiane na Wabrazili ili miaka ijayo taifa letu liweze kupata wanasoka nyota kama wale wa Brazili.

Tuwape maelekezo kabisa kwamba mkienda huko sakeni akina Kaka, Ronaldo de Lima, Oscar, Coutinho, Adriano, Carlos, Fernandinho, Alver na akina Neymar na wengine wengi ambao wamekuwa wanang’ara katika timu ya Brazili. Nalisema hili kwa sababu tumejaribu kufanya mbinu zote angalau tuweze kuvuka katika hatua hii ya sifuri, lakini imeshindikana.

Tumewaleta makocha wakiwemo wa kutoka Brazil, lakini hawakutufikisha popote, sasa dawa ni kutafuta kizazi cha Wabrazili na sisi tuweze kung’ara kama ilivyo kwa mataifa mengine.

Angalia wenzetu wa mataifa ya magharibi ambayo mengi yalitawaliwa na Wafaransa, kwa kuwa kuwa Ufaransa iliendelea kuchukulia kuwa makoloni yake yote ni sehemu ya Ufaransa, Wafaransa wengi walikaa kwenye nchi za Cameroon, Ivory Coast na kwingineko na matunda yake mnayaona.