Haya ndio Maisha: Mwaka 2017 uwe mwaka wenye mafanikio kwako

KUNA kila sababu ya kumshukuru Mungu kwa kuingia mwaka mpya wa 2017, maana wako wengi walitamani kuingia mwaka huu, lakini wametangulia mbele za haki.

Hatuwezi kujitapa wala kujidai kuwa ni kwa nguvu zetu, tumefika hapa ila ni kwa neema ya Mungu haijalishi wewe au mimi ni muumini wa madhehebu gani au muumini wa dini gani. Mwaka 2016 umepita ukiwa na mazuri na mabaya yake, kila mmoja wetu anajua mwenyewe mwaka huo kwake anaweza kuzungumzia vipi au aliuonaje?

Wako waliofanikiwa, na kufurahia sana matunda ya kile walichokuwa wamejipangia wakati wanauanza mwaka huo uliopita, lakini wako wengine wanashukuru sana kuwa mwaka huo umekwisha maana kwao ulikuwa mwaka wenye changamoto nyingi.

Naamini kila mtu anapoanza mwaka mpya anakuwa amejiwekea malengo ama matamanio ya kuona anafanikisha jambo fulani katika maisha yake. Wako waliopanga kuona mwaka huu mpya wanajiendeleza kimasomo, wako wanaotamani kuona mafanikio makubwa katika familia zao, wako wanaotamani kazini wapate promosheni, wako waliopanga kuona wanajenga ama kumaliza kujenga.

Kimsingi kila mmoja amejiwekea kuona anafikisha yale anayojipangia kuona mwaka unakuwa wa mafanikio. Kuna wengine wamehama na viporo vya mambo yao, vya mwaka 2016 ambavyo wanaamini mwaka huu watakamilisha malengo yao na kuongeza malengo mengine.

Lakini ili kufanikiwa lazima ujitoe na ujitume kwa moyo wako wote ili kufanikisha malengo yako na kuachana na porojoporojo. Wako watu wana mipango mingi mizuri lakini kwa nadharia inapokuja suala la kufanya kwa vitendo hakuna kitu, halafu baadaye ni kulalamika na kunung’unika.

Unarukaruka lakini ukifika mwisho wa mwaka ndio unagutuka unaanza kujishutumu, mbona sijafanya hiki, mara kile wazungu wanasema , ‘it’s too late, the year is over!’ Kuna wengine wamezoea kubebwa tu, hawataki kujishughulisha kwa lolote, badilikeni sasa, mwaka huu uwe wa tofauti.

Kama ni kusoma omba msaada soma, kama ni kazi tafuta kwa bidii fanya kazi acha kuwa ombaomba, kama biashara tafuta mtaji anza, maana miaka na maisha yanavyokwenda itafikia miaka hakuna wa kukubeba.

Nakushauri mwaka huu mpya umeanza onekana wa tofauti, jipange na utimize malengo yako ili usiwe mtu wa kujilaumu na kulalamika utakapofika mwisho wa mwaka huu. Nawatakia kila la heri mwaka huu mpya wa 2017!