Kama Mzazi: Walimu bila maadili wachukuliwe hatua

KABLA ya kuingia moja kwa moja kwenye hoja niliyoiandaa kwa ajili ya safu hii ya Kama Mzazi leo, napenda kuwapongeza kwa kupata rehema za Mungu kuwavusha salama kuingia mwaka mpya wa 2017.

Hakuna ubishi kwamba wapo wenzetu ambao hawakubahatika kuuona mwaka kutokana na sababu mbalimbali, ikiwa ni pamoja na magonjwa na ajali zilizowafika na kisha kupoteza uhai. Kwa wale wenzetu waliopoteza maisha basi Mungu aweze kuwasamehe na kuwapokea kwa rehema zake.

Lakini wakati bado tupo katika shamrashara za kuukaribisha mwaka mpya, yapo matukio ambayo safu hii bado inayakumbuka na kwamba isingependa yaendelee kupata nafasi katika mwaka huu mpya kama ilivyokuwa mwaka jana.

Tunaweza kusema ni matukio yaliyoudhi na kuleta kero na ambayo yamefanywa na watu ambao katika hali ya kawaida wasingethubutu kudiriki kufanya. Hao si wengine bali ni baadhi ya walimu wa shule za msingi na sekondari ambao walijigeuza kwa makusudi kwa kukiuka maadili ya kazi zao za kuwa walezi wa wanafunzi na badala yake kujitumbukiza kuwa wapenzi wao.

Wakati walimu nane walitiwa mbaroni mkoani Mwanza kwa kujihusisha kimapenzi na wanafunzi wao, wengine walikwenda mbali zaidi kwa kuishi nao kinyumba kama mume na mke katika badhi ya wilaya zetu hapa nchini. Ni jambo linalotia aibu na ni kinyume cha maadili ya kazi ya ualimu.

Watoto wetu wa kike na kiume wanaanza siku yao nyumbani kwa wazazi na walezi wao na sehemu kubwa ya siku yao hupata malezi ya kitaaluma na ulinzi wa maisha yao kwa walimu wao.

Wazazi na walezi katika hali ya kawaida hutakiwa kushirikiana kwa karibu na walimu kwa lengo moja la kumjenga mtoto kimaadili, kitaaluma na kimalezi ili wakue na hatimaye waweze kulitumikia taifa lao wakiwa wameiva kwa kila hali.

Lakini kwa mtindo wa walimu hao wachache, inaelekea kunaanza kujengeka utamaduni ambao wote kwa ujumla lazima tuukemee na tusiruhusu uendelee kuota mizizi katika jamii zetu.

Kwani tukifika hapo, basi imani ya mzazi au mlezi kumwacha mtoto wake kwa walimu inaweza kuanzia kupotea na hili linaweza kutufikisha mahali pa kukata tamaa na kutoaminiana kati ya wazazi na walimu. Kama Mzazi inasema hili lisipewe nafasi katika mwaka huu mpya, bali itafutiwe mbinu ya kukabiliana nayo bila kufanya ajizi.

Katika hili ni vyema kila mzazi, mlezi na mwenye mapenzi mema na malezi ya watoto wetu, kuwa tayari kushirikiana na mamlaka za serikali na jamii kutoa taarifa yoyote itakayoonesha dalili ya mtoto kurubuniwa kuwa mpenzi na mwalimu wake.

Ni kazi ambayo siyo rahisi kuitekeleza lakini iwapo kila mzazi au mlezi atakuwa makini katika kufuatilia mwenendo wa mtoto wake kimaadili, kimasomo na mahusiano yake na walimu na wanafunzi wenzake, kutakuwa na kila aina ya uwezekano wa kugundua njama za aina hiyo mapema na iwapo hilo likitokea, basi mhusika afikishwe kwenye vyombo vya dola ili naye avune anachostahili.

Wazazi na jamii kwa umoja wao wakishikamana katika hili, ujahili unaofanywa na baadhi ya walimu kwa wanafunzi wao kwa kuwageuza kuwa wapenzi utadhibitiwa kama siyo kukomeshwa kabisa. Kwa hili, Kama Mzazi inasema tushikamano kukabiliana nao mpaka kieleweke.