Jicho: Migogoro ya wakulima, wafugaji hadi lini?

MATUKIO ya kujeruhiana na hata kuuana ambayo chanzo chake ni migogoro kati ya wakulima na wafugaji, yameendelea kugubika mkoa wa Morogoro .

Tukio la hivi karibuni la mkazi wa kijiji cha Dodoma Isanga, kata ya Masanze wilaya ya Kilosa, Augustino Mtitu aliyechomwa mkuki mdomoni na kutokea shingoni, hakika linasisimua mwili. Ashukuriwe Mungu kuwa, mkazi huyo ambaye ni mkulima, alikimbizwa hospitali, akafanyiwa upasuaji na kuondoa mkuki huo.

Taarifa zilizotolewa ni kwamba, Mtitu na wakulima wengine wanane walijeruhiwa katika vurugu zilizohusisha jamii ya wafugaji na wakulima wa kijiji hicho . Inaelezwa katika kuzuia vurugu zilizotokana na wafugaji kulisha mifugo katika shamba la maharage na mahindi katika kijiji hicho, mtu huyo ndipo alichomwa mkuki.

Matukio haya ya mauaji na kujeruhiana, hususani katika Mkoa wa Morogoro, ni mengi na yanataka kuonekana kama ni ya kawaida kutokana na kujitokeza mara kwa mara. Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchembe amekaririwa hivi karibuni akitaja wilaya za Kilosa, Mvomero na Morogoro kuwa zimekithiri kwa vitendo hivyo.

Kila inaporipotiwa kuhusu migogoro hii, huwa natamani kufahamu watu wanaofanya vitendo hivi vya mauaji kama huwa wanapewa ‘stahili’ yao. Najikuta nawaza kwa sauti kuwa huenda kesi zinazohusu watuhumiwa wa mauaji au kujeruhi , ama hukumu zake zinachelewa kutolewa au yawezekana zinatupwa kwa madai ya kukosa ushahidi.

Katika kuwaza kwangu kwa sauti, naona kutokana na hali hiyo ya watuhumiwa kutotiwa hatiani na kupewa adhabu kali, inaweza ikawa sababu ya baadhi ya watu (wakulima na wafugaji) kuendelea kujichukulia sheria mkononi kutenda uhalifu.

Vile vile huwa najikuta nikitengeneza nadharia kuwa, huenda vyombo vya habari hatufuatilii kuripoti juu ya hatua zilizochukuliwa dhidi ya wahalifu hao. Yawezekana wapo waliohukumiwa vifungo jela miaka kadhaa au hata kunyongwa; lakini taarifa hizo haziwekwi wazi kiasi cha kuwa fundisho kwa watu wengine wenye nia ya kutenda uhalifu huo.

Hata hivyo, kwa kuwa sina uhakika juu ya takwimu zinazoonesha kesi zilizofunguliwa, zilizopo mahakamani, hukumu zilizotolewa na aina ya hukumu kwa washitakiwa, basi niishie kusema kwamba, kila mamlaka inayohusika na kukabili vitendo hivi, itimize wajibu wake migogoro hii ikome.

Wajibu huu uhusishe jamii, polisi, mahakama kuhakikisha kuwa kesi dhidi ya watuhumiwa wa mauaji na kujeruhi, zinaendeshwa kwa haraka na kunakuwa na ushahidi wa kuwatia hatiani watu hawa. Inawezekana hawa wanaotenda uhalifu huu, wamechukulia mazoea.

Wanajiona wako juu ya sheria kiasi cha kutoogopa mamlaka yoyote na mikakati mbalimbali ambayo imekuwa ikiwekwa. Kauli ya Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba aliyoitoa hivi karibuni kwamba atakayekamatwa, atachukuliwa hatua kali za kisheria, itekelezwe kwa vitendo.

Lakini pia, mikakati na mipango ya kudumu juu ya namna ya kukabili migogoro hii, haina bodi kutekelezwa kwa vitendo kuhakikisha migogoro hii haiendelei kupukutisha maisha ya watu na wengine kusababishiwa ulemavu. Katika kufuatilia, inaonesha kuwa ipo mikakati mingi imeshafanyika na inaendelea kufanyika lakini bado migogoro hii inaendelea.

Migogoro hii inayoendelea inanikumbusha kamati teule ya bunge iliyoundwa mwaka 2015 kuchunguza sababu za migogoro baina ya wakulima na wafugaji, wawekezaji na watumiaji wengine wa ardhi amba Ikiwa na wajumbe watano chini ya mwenyekiti wake , (aliyekuwa mbunge wa Simanjiro), Christopher Ole Sendeka iliweka wazi kwamba, migogoro ya ardhi inatishia kutoweka kwa amani, umoja na utangamano wa wananchi katika maeneo yenye migogoro na taifa kwa ujumla.

Kamati ikaitaka serikali kuharakisha usuluhishi wa mgogoro baina ya wakulima na wafugaji. Ikataka serikali kutenga njia za kupitisha mifugo kwa ajili ya kufuata malisho, majosho na maji kwa mujibu wa Sheria ya Maeneo ya Malisho na Rasilimali za Vyakula, ya mwaka 2010.

Spika wa bunge wa wakati huo, Anne Makinda akaeleza sababu za kuridhia kuundwa kwa kamati hiyo kuwa kulitokana na malalamiko ya wabunge bungeni, kuhusu migogoro ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji, ambayo kwa muda mrefu haijapatiwa ufumbuzi na kusababisha madhara ikiwamo mauaji.

Wakati nikiamini kuwa si mimi peke yangu ninayejiuliza swali hili: Migogoro ya wakulima, wafugaji hadi lini?, ni vyema serikali na wadau wengine wakarejea mikakati , mipango na mapendekezo mbalimbali yaliyowahi/yamekuwa yakitolewa juu ya namna ya kukomesha hali hii inayoleta doa kwa taifa juu ya suala zima la amani na usalama. Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.