POROJO za anko Sagati: Noah inapobeba abiria 34!

GARI la Noah lina uwezo wa kubaeba abiria wanane tu, lakini cha ajabu juzi gari moja limekamatwa limebeba abiria 34!

Licha ya watoto hao 34 pia kulikuwa na mwalimu wao mmoja aliyekuwa amekaa kiti cha mbele na kuwaacha watoto wamebanana huko nyuma. Abiria hao 34 ni watoto wanaosoma katika shule za Upanga,Bunge,Diamond na Kisutu walikutwa na polisi wamerundikwa kwenye gari hilo Noah jambo ambalo ni la kushangaza.

Kutokana na uajabu wake, mitandao ya kijamii pia ilivutiwa na picha hiyo na hivyo kuanza kusambaa kwenye mitandao ya kijamii kuonesha tukio hilo ambalo sio la kawaida. Ni picha ambayo ilizusha maswali mengi, kwamba je ni uongozi wa shule hizo ndio ambao umeingia mkataba na Noah hiyo kubeba watoto hao?

Ni Wazazi wenye watoto wanaosoma kwenye shule hizo ndio ambao wamechangishana na kuikodi Noah hiyo iwe inawabebea watoto wao na kuwapeleka na kurejesha nyumbani? Lakini ni mzazi gani atakubali mtoto wake ateseke kiasi hicho?

Kwani ukiangalia picha hiyo utawahurumia watoto wenyewe, kwani utakuna kwenye viti vimebebana na vingine vimechoka kwa kuwapakata wenzao. Kwenye buti huko nako vimerundikwa kama vifaranga, wengine walikutwa wamechuchumaa na wengine wameinama jambo ambalo linaonesha namna watoto hao walivyokuwa wanateseka kwenye usafiri huo.

Kwa wale ambao wanajua magari ya Noah ni kwamba mbele anakaa abiria mmoja na dereva na nyuma wanakakaa abiria sita, hivyo kufanya gari hilo kuwa na uwezo wa kubeba watu wanane tu yaani akiwemo na dereva. Sasa maajabu ya Musa ya Noah kubeba watu 34 kwa kweli haya ni maajabu ambayo sio ya kawaida.

Sielewi wazazi wanalipa kiasi gani kwa shule hizo kwa ajili ya usafiri wa watoto wao. Lakini ukweli ni kwamba wanafunzi wengi wamekuwa wanarundikwa kwenye magari haya ya shule kama vifaranga. Polisi wanatakiwa kufuatilia kwa kina kuona magari hayo yanavyowababanisha watoto.

Wazazi tunalipa fedha nyingi mno kuhakikisha watoto wanatumia usafiri ili waweze kufika shuleni kwa urahisi. Lakini wenye shule nao kwa kuwa wanataka faida mara dufu wamekuwa wanahakikisha wanabana matumizi bila kujali kama wanawaumiza watoto.

Hili la wanafunzi 34 ni mfano tosha kwamba wazazi wenye watoto wanaosoma kwenye shule hizo wanalipishwa fedha na uongozi wa shule hizo, lakini kwa kupenda urahisi shule tano zimeamua kushirikiana kubeba watoto wanaoelekea njia moja.

Hili ndio linasababisha sasa watoto wanarundikwa kama vifaranga kwenye maboksi, jambo ambalo halikubaliki hata kidogo. bila kujali kwamba katika njia hiyo kuna watoto wangapi wanaamini tu kwamba gari moja aina ya Noah linawatosha. Haya yawezekana ni mateso ya muda mrefu ambayo wameyapata watoto wetu wanaosoma kwenye shule hizo.

Wazazi sasa umefika wakati wa kufuatilia usafiri wanaotumia watoto wenu kujua kama fedha unayotoa inalingana na huduma wanayokupa. Kwa hili la watoto 34 kurundi kwenye gari moja halikubaliki hata kidogo.