Vijana: Tuache kumlaumu Sizonje tufanye kazi

NAWASALIMU ndugu zangu! Mhali gani… Dah! Mimi niko poa kabisa namshukuru Mungu kwa wema na rehema zake ananipigania mimi na familia yangu na siku zinasonga.

Ebwana tuache utani jua linawaka ile mbaya! Na baadhi ya vijana sasa naona wanatumia jua hili kama kigezo cha kutofanya kazi na kuishia kulalamika tu kila kukicha. Mlalamiko ambayo kimsingi sioni kama yanatija kama sote tukiamua kuacha kufanya kazi na kujificha jua ambalo hatujui litaisha lini.

Ah! Lakini kuna mtindo siku hizi umeibuka mtaani, kila mtu unaemgusa “Bwana vipi maisha yanaendaje..” atakujibu “magumu sana ‘Sizonje’ anakaba kila kitu hakiendi.” Wapo vijana hawajishughulishi kutafuta riziki za halali na mwisho siku wanamsingizia ‘Sizonje’, wapo ndugu zangu wengijne wanakwepa majukumu ya familia na kijamii nao ukiwauliza nini tatizo ‘Sizonje’.

Asa jamani kila kitu Sizonje, hivi mnadhani bila Sizonje kufanya hivi anavyofanya kuna mtu nchi hii atafanya kazi kweli, au mlitaka tuendelee kujenga matabaka ya wenye nacho na wasipo nacho? Acheni bwana. Mnakera sana na hasa mimi mnanikera sana, hebu tufanye kazi, halafu wale wanaotupa kazi waone tunavyowajibika na kuleta tija ndipo tuseme Sizonje anakaba.

Mara zote wawivu huwa hawaishi maneno na hata angekuwa na utaratibu wa kupita na gari mtaani na kumwaga fedha, bado wapo ambao wangelaumu kuwa Sizonje anatoa noti za wekundu tu kila siku bwana sisi tunataka hizi za elfu kumi na tano.

Wanadamu hawana shukrani, mnasema Mjomba yeye aliachilia fedha sana mtaani wakati wake wa uongozi lakini hebu angalia ni wangapi walifanya vya maana au waliishia tu kusema kila jengo zuri mjini ni la Mtoto wa Mjomba Yule aitwae naniliu. Ni vyema sasa vijana wenzangu tukaamka na kuacha kulalamika na badala yake tutumie fursa chache zilizopo kujipatia kipato.

Mi nawaambia fedha zipo ila ni kwa wale tu wanaojishughulisha, na wale tulio zoea kuishi kwa mizinga kwakweli hatutaacha kumsingizia Sizonje kuwa kaficha fedha. Na ninavyozidi kumuelewa Sizonje sidhani kama kuna siku atalegeza uzi ili fedha zije mtaani hata kwa wasiofanya kazi, tuache kuishi kama hadithi ya Fisi na Mkono wa binadamu ambao fisi alikuwa anaunyemelea akidhani jinsi unavyorushwa akitembea basi upokaribu kudondoka.