Jarida la Wanawake: Tuepuke laana kwa kutupa watoto

HAKIKA akinamama siku hizi wamekuwa na roho za kikatili kiasi cha kusababisha maumivu na machozi kutokana na kuwa wauaji, kwani jamii inategemea mwanamke kumlinda mtoto wake kwa sababu mbalimbali, lakini imekuwa tofauti kwani sasa mwanamke amekuwa hatari kwa mtoto anayemzaa.

Yamekuwepo matukio ya ukatili wa kutisha, baadhi ya akinamama wamekuwa wakidiriki kujifungua na kutupa watoto iwe kwa kuwafunga katika mifuko na kuwatupa jalalani au kwa kuwatumbukiza katika vyoo, jambo ambalo ni hatari sana na dhahiri inaonesha ni kujitengenezea laana.

Nasema ni kujitengenezea laana kwani kila mwanamke akifikiria changamoto mbalimbali unazokabiliana nazo katika kutafuta mtoto, wakati wengine wanapata shida kutafuta watoto kwa miaka mingi bila mafanikio, wako wengine wanateseka katika maisha yao ya ndoa kwa kukosa watoto lakini cha ajabu wako wanaobarikiwa kupata watoto halafu wanaamua kuwaua.

Kitendo hicho kinaashiria kuwepo kwa ukatili usiopimika kwa wanawake hivyo ni vema kuupinga kwa nguvu zote kwani inaweza kusababisha laana kwa wanawake wote nchini kwa kutokukubali hali hiyo iendelee kwa kuwakatisha uhai watoto.

Kuna baadhi wanakamatwa na polisi kutokana na vitendo hivyo, lakini wako wengine wanafanya vitendo hivyo lakini hawajafikiwa na vyombo vya dola, hivyo mwito wangu ni kwa wanawake, kwamba kila mwanamke katika familia na mtaa kuwa mlinzi wa mwenzake na anapofanya vitendo hivyo afikishwe katika vyombo vya sheria.

Pia kwa waliokamatwa wanatakiwa kuchukuliwa hatua kali, ikiwa ni pamoja na kunyang’anywa watoto hao ikiwa wamenusurika kufa kwani ni dhahiri mama aliyefanya kitendo hicho hakumhitaji mtoto na hivyo hawezi kuwa na mapenzi na mtoto huyo.

Vilevile wale ambao watoto walikufa basi wapewe adhabu kali ambayo hawatasahau maishani ili kudhibiti vitendo hivyo vya kikatili ambavyo ni dhahiri vinapingwa kokote duniani kwa imani ya dini yoyote na kwa sheria za nchi kuua ni dhambi hivyo hakuna sababu ya kuwapa adhabu ndogo.

Ni vema wanawake wakahakiki laana hii, inaepukika kwani hakuna sababu yoyote inayoweza kukufanya kumtupa mtoto uliompatia shida ya kubeba mimba miezi tisa na kupata uchungu kujifungua kisha kuishia kumtumbukiza chooni hakika hii ni laana inayohitaji kukemewa kila kona na hususan wanawake wenyewe kwani ni kashfa na aibu katika jamii.