Jicho: Fuatilia gari la shule la mtoto wako

HIVI karibuni, katika gazeti hili, ilichapishwa picha habari iliyoonesha watoto wa shule tatu za msingi za jijini Dar es Salaam waliokuwa wamepakiwa kwenye gari moja ambalo lilikamatwa na askari wa usalama barabarani.

Gari hiyo ilikamatwa na askari wa kituo kikuu cha askari wa usalama barabarani kwa kuzidisha kiwango cha abiria; kitendo kinachohatarisha usalama wa watoto hao. Watoto hao walionekana wakishuka kwenye gari hilo aina ya Toyota Noah huku ikibainika, baadhi walikalishwa kwenye buti.

Gari hilo lenye uwezo wa kubeba abiria wanane, inasadikiwa lilikuwa na wanafunzi wapatao 30. Kweli haya siyo maajabu tu, bali ni hatari!. Tatizo la usafirishaji wa wanafunzi (watoto) katika hali isiyo salama, naamini ni kubwa kuliko inavyotegemewa.

Hili ni kwa pande zote mbili; kwa maana ya magari ambayo wazazi wanaweza kuamua kuyatafuta wenyewe na kulipa mwenye gari, au magari yanayomilikiwa moja kwa moja na shule na wazazi hulazimika kuchangia gharama za usafiri.

Si suala la kificho, baadhi ya magari hayo yenye nembo ya ‘school bus’ , yamekuwa yakionekana barabarani yakiwa yamejaza watoto kupitia kiasi. Mengine mwonekano wake unadhihirisha wazi kuwa ni mabovu.

Nakumbuka katika mitandao ya kijamii, iliwahi kuwekwa gari aina ya Toyota ambayo pia ilikamatwa na askari wa usalama barabara maeneo ya Posta ya zamani jijini Dar es Salaam ikisafirisha watoto wa awali wakitoka shuleni kwenda nyumbani.

Toyota hiyo ilioneshwa ikiwa imefunikwa turubai, ndani kukiwa na watoto ambao ilielezwa walikuwa wakitoka jasho kutokana na joto kubwa. Pamoja na hayo machache yaliyowahi kukamatwa na polisi, naamini wakiamua kufanya ufuatiliaji wa kina wa mfumo wa usafirishaji wanafunzi, wataini kasoro nyingi kwa shule nyingi; ikiwamo ubovu wa magari husika.

Kasoro nyingine ambayo baadhi ya shule zimekuwa zikifanya, ni kuachia madereva kazi hiyo ya kusafirisha watoto hao bila kuwapo mwangalizi/mlezi. Nakumbuka iliwahi kutokea jijini Dar es Salaam , mtoto alidondoka barabarani kutoka kwenye basi la shule, akakanyagwa na tairi la nyuma na kupoteza maisha.

Taarifa zilieleza kwamba, mtoto huyo alikuwa akicheza na wenzake ndani ya gari na katika michezo hiyo, alisukumwa na wenzake kupitia dirishani, akadondoka barabarani na kisha kukanyagwa na tairi la nyuma la gari hiyo. Inawezekana kungekuwa na mlezi tofauti na dereva, hayo yasingetokea.

Lakini pia haitoshi gari la shule kuwa na dereva na kondakta, bali inapaswa liwe na mlezi kwa ulinzi makini wa watoto. Wazazi na walezi wengi inawezekana hawafahamu haya yote yanayotokea zaidi ya kufahamu kulipa fedha za usafiri kila mwezi wakiamini kuwa watoto wao wako katika mikono salama.

Unakuta mzazi anajinyima kwa ajili ya kumnusuru mtoto wake na usafiri wa daladala ambao ndiyo unaaminika kuwa rafiki kwa watoto wakati kumbe hata hiyo ‘school bus’ anayoilipia feda nyingi, si rafiki na si salama kwa ustawi wa mtoto.

Unakuta mzazi anaamini kuwa mtoto wake anasafiri kwenye ‘school bus, wakati kumbe anasafirishwa kwenye buti la ‘school noah’ au anasafirishwa ndani ya ‘school pick up’. Kwa ujumla, hii ni changamoto kwa wazazi na walezi.

Tunahitaji kuwa makini na kufuatilia kwa karibu usalama wa watoto katika magari hayo ya shule. Haitoshi kulipia fedha za usafiri bila kujiridhisha na magari yanayotumika, usimamizi uliopo na aina ya watu wanaoendesha magari hayo. Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.