Zingatia miiko utoaji huduma katika biashara

SIKU moja nilikutana vioja katika baa Dar es Salaam, ambapo, mhudumu alikuwa akihudumia wateja vinywaji, huku akila wali na njegere wakati huo huo. Wakati akifanya hivyo, mwenzake alikuwa akiwapa vinywaji wateja wanne waliokuwa kwenye meza jirani na niliyokuwa nimeketi, kwa mtindo wa kuviweka kwenye kwapa, badala ya chombo maalumu kama vile vikapu vidogo vya plastiki au trei.

Kuonesha kuwa kwao mtindo huo wa kuhudumia wateja ‘alimradi’ ndio uliozoeleka, wahudumu hao wanawake hawakujali kuonekana wa ajabu, kwa sababu, licha ya baadhi ya watu nikiwemo mimi kuonesha kuwashangaa, waliendelea kuhudumia hivyo.

Cha kusikitisha ni kuwa, mteja mwanamke aliyekuwa miongoni mwa wateja wanne katika meza hiyo ya jirani na niliyokuwa nimeketi, aliyepelekewa chupa ya soda ikiwa imebebwa kwapani na kuikataa, akiomba chupa isafishwe au abadilishiwe, hakusema ni kwa sababu gani hivyo kuonekana anaringa.

Niligundua kuwa mteja yule alitaka kinywaji kingine kwa kuwa alicholetewa kilikuwa kimewekwa kwapani hivyo hakupenda.

Wenzake hawakuiona kasoro hiyo kwa sababu vya kwao vililetwa vikiwa vimeshikwa mikononi katika eneo la midomo ya chupa ambalo pia, wataalamu wa usafi katika huduma wanasema ubebaji huo si salama kwa afya.

Nimeona nizungumze hili katika safu hii kuwakumbusha watoa huduma za vinywaji na vyakula mahali popote walipo kuwa, biashara yoyote ina miiko. Kwa sababu hiyo, ni vizuri kuizingatia ili biashara ya huduma inayotolewa ifanikiwe.

Mazoea siku zote yana tabu yake, hasa ikiwa mhudumu anakuwa amewazoea wateja wake kupita kiasi na kutojali tena kuwathamini kwa huduma bora.

Miiko ya biashara ambayo ndiyo maadili yenyewe ya biashara inaweza kusaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza au kuondoa uzembe na mazoea yanayoweza kuwafanya wahudumu ‘waijeruhi’ biashara waliyoajiriwa kuifanya.

Kutokana na kushuhudia vioja hivyo, nililazimika kutafuta maelezo ya wataalamu kutoka katika mitandao mbalimbali, kujua endapo kubeba vinywaji hovyo kwa namna yoyote kuna athari kwa mteja na biashara.

Nilituma maswali katika mitandao; www.ask.com na kwenye www. answers.com na kupata majibu yaliyonipa ujasiri wa kuzungumza haya ninayoyazungumza leo katika safu hii.

Kwanza, inaelezwa kuwa, kula huku ukifanya shughuli ya kuhudumia wateja vyakula au vinywaji ni aibu, uchafu na kutomthamini mteja.

Mtandao wa www.answers.com unasema, ndiyo maana katika hoteli za kati na kubwa au katika baa na migahawa ambayo wahudumu wamepata elimu ya kazi ya kutoa huduma ya vinywaji na chakula, hutengewa muda maalum wa kula, ili wanapokuwa ‘bize’ na wateja wasishike mawili. Mtandao huo umehoji hivi;

“Itakuwaje (mhudumu) unapokuwa na chakula mdomoni halafu mteja akakusemesha jambo na kutaka jibu la papo hapo?” Wakati mtandao huo ukieleza na kuhoji hivyo, www.answers.com inasema, kuna uwezekano mhudumu anayezungusha vyakula au vinywaji kwa uzembe, bila kuvifunika na huku akitafuna kwa kujaza chakula mdomoni akamchefua mteja kwa namna mbalimbali kulingana na jinsi anavyotafuna.

Unasema, “Wengine hawana nidhamu ya kutafuna wala ya kufungua midomo kwa staha... mteja anapoona vyakula mdomoni anaweza kuhisi kinyaa na kuachana na hitaji la huduma aliyoifuata mahali hapo. Hatua hiyo mara nyingi humsababishia mwenye biashara (si mhudumu mzembe) hasara”.

Kwa maelezo ya mtandao huo, kupoteza mteja mmoja tu katika biashara yoyote ile ni pigo.

Kadhalika, mtandao wa www. ask.com unasema, kwa maeneo ambayo wateja ni wakali, mhudumu mwenye tabia ya kubeba vinywaji au vyakula kizembe huweza kuripotiwa kwa meneja na kupewa onyo au kufukuzwa kazi.

“Hasa katika eneo la vyakula, mhudumu anapaswa kuwa makini na mwenye kuthamini usafi kwa ajili ya afya yake na ya mteja anayemhudumia. Kubeba kinywaji bila kuwa na kifaa kitakachozuia mikono ya mhudumu usigusane nacho moja kwa moja ni kosa, www.ask. com inaeleza.

Kwa ufupi, mitandao hiyo imenifungua macho na kunijuza mambo mengi ambayo hapa kwetu hayazingatiwi na wahudumu au wamiliki wa biashara za aina hiyo.

Inaelezwa kuwa, kwa bara la Ulaya na nchi nyingine zinazoendelea ambazo raia wake wanajua haki zao za kuhudumiwa kwa umakini, wanazikataa huduma mbaya na wanawaeleza wahudumu wachafu kuwa hawapendi wawahudumie.

Madhara kwa afya Ingawa mitandao hiyo miwili haijaweka bayana madhara yanayoweza kusababishwa na ubebaji usiofaa wa vinywaji na vyakula, wakati wa kuhudumia wateja (mfano halisi ni huo wa kuweka soda kwapani), mtandao mwingine, www.hospitalityinfocentre.co.uk unasema, ubebaji huo unaweza kusababisha maradhi kwa mteja na mhudumu mwenyewe.

Kwa ufupi, mtandao huo unasema, “Kwapa ni sehemu ya mwili inayofahamika kwa kutoa na kuhifadhi jasho, hivyo, ni eneo lisilostahili kugusishwa kitu chochote kinachoingizwa kwenye mdomo wa binadamu”.

Mbali na mtandao huo, www. traveldoctor.com nao unaeleza kuwa, mteja anapaswa aridhishwe na mazingira anayopewa huduma, ili asitie mashaka wakati wa kutumia huduma hiyo. Unasema, kitendo cha kuwa na wasiwasi kinaweza kumfanya akaugua kwa hofu, hivyo kuiona biashara ya huduma aliyoifuata kuwa ni mbaya.

“Ni vizuri wahudumu wa vinywaji na vyakula wakaheshimu taratibu za usalama wa afya ya watu na mazingira kwa kufuata maelekezo wanayopewa shuleni wakati wakijifunza masuala muhimu ya kuhudumia wateja kwa ukarimu,”www.traveldoctor.com unasema.

Kutokana na yaliyoelezwa katika mitandao hiyo, ninawashauri wafanyabiashara wa vyakula na vinywaji wahakikishe wanawapa mafunzo wahudumu wasivurunde, biashara zifanikiwe. Kwa maoni wasiliana na Mwandishi kupitia Simu; 0752 779090 au Barua pepe; namsp2000@ yahoo.com.