MARUFUKU POMBE ZA VIROBA: Huu ndio uongozi uliotukuka

NILIPOSIKIA sauti yenye mamlaka ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ikisema kwamba kuanzia kesho Machi mosi ni marufuku pombe za kwenye pakiti ndogo maarufu kama viroba kuuzwa, nilijisikia furaha moyoni.

Bila shaka, kama utasoma makala haya hadi mwisho utajua kwa nini nilifurahi na kuunga mkono hatua hii. Waziri mkuu akiwa katika ziara mkoani Manyara, alisema: “Sasa hivi viroba vimeenea kila kona hata watoto wa shule za msingi wanatumia kwa sababu ni rahisi kuweka mfukoni na kutembea navyo... Kuanzia tarehe moja Machi, tutakayemkamata ameshika pombe ya viroba, sisi na yeye.”

Wakati mimi nikiunga mkono hatua hiyo ambayo kwangu imekuja ikiwa imechelewa sana, kama ambavyo kuna Watanzania wanatetea au kupinga kampeni dhidi ya dawa za kulevya kwa waziwazi au kwa njia nyingine, kuna wanaotetea pombe za viroba ziendelee kuuzwa! Wapingaji hawa, huku wakitoa sababu zao ambazo hazijai kiganjani ni pamoja na madai kwamba muda uongezwe ili wanaotengeneza viroba waendelee na biashara hiyo ‘hatari’ kwa madai kwamba watapata hasara na kwamba wengine wamekopa benki.

Lakini wapo wanaodai kwamba kwa kuwa viroba vinavyoaminika kuwa na asilimia kubwa ya kilevi vinauzwa bei rahisi (Sh 500 na vingine Sh 1,000), kwa kuvipiga marufuku watalazimika kunywa pombe hatari zaidi wakimaanisha gongo ili kukidhi haja zao.

Nikianza kutalii hoja za wale wanaodai kwamba watapata hasara, na mmoja nilimsikia akizungumza kwa kujinafasi katika moja ya vituo vyetu vya redio, nikawa sijui hayo anayapata wapi wakati Waziri Mkuu alikaririwa akisema maneno haya: “Tumekaa na wenye viwanda na kukubaliana kuwa wanaotengeneza pombe waziweke katika ukubwa unaokubalika.”

Kutokana na madhara ambayo yanasababishwa na pombe hizo za viroba, kama nitakavyoyajadili hapa chini kwa ufahamu wangu, faida ya kuvipiga marufuku kwa jamii ni kubwa maradufu kuliko hasara ambayo wazalishaji wataipata hata kama serikali isingelikaa na watengenezaji wa hivyo viroba kwanza.

Ninapoanza kutaka kuorodhesha hasara za pombe za kwenye viroba sijui nianze na ipi, lakini labda kwa vile naishi uswahilini, ngoja nianze namna hii. Pale jirani yangu, kuna duka kubwa linalouza bidhaa mchanganyiko.

Mara kadhaa, asubuhi na mapema nimeshuhudia watu, wakiwemo vijana wadogo sana, wakinunua viroba hivi, wakavinyonya kufumba na kufumbua na kisha kuondoka zao.

Hii maana yake ni nini? Ni kwamba watu hawa, wanaamkia kwenye ulevi na hivyo wanakwenda kwenye shughuli zao tayari wakiwa wameelewa.

Kwa hatua hii kweli wanaweza kuzalisha mali ipasavyo? Je, kwa nguvu kazi hii inayolewa asubuhi na muda wowote inaotaka na hivyo kushindwa kuzalisha ipasavyo ni hasara iliyoje kama tunataka kujenga nchi ya wachapa kazi watakaoibeba nchi yetu na kuikimbiza katika uchumi wa kati, uchumi wa viwanda? Pili, kama nilivyosema, baadhi ya watu ambao nimekuwa nikiwashuhudia wakinunua pombe za viroba na mwenye duka akiwa hana hiyana kumuuzia yeyote anayetaka kiroba, wamo hata wanafunzi.

Wakati watoto hawatakiwi kuonekana kwenye baa na stoo za pombe, lakini hali ni tofauti kwenye maduka. Kila mtu, kila mtoto anaweza kununua kiroba. Je, kwa mtindo huu tunajenga taifa la namna gani? Huku uswahilini ninakoishi miye, vijana wengi sana wanakataa shule na mara tu baada kushindikana kwenda shuleni, hawaishii kunywa viroba pekee bali wanajiingiza pia kwenye dawa za kulevya.

Kwa mtazamo wangu, unywaji wa viroba ni njia pia ya kuwapeleka vijana wetu katika matumizi ya dawa za kulevya, sigara na matendo mengine ya hovyo katika jamii kwani ulevi ukiwemo wa pombe kama nitakavyojadili baadaye, unapunguza uwezo wa akili kufanya mambo mazuri.

Katika kitabu chake alichokitaa ‘Maswali yanayoulizwa sana na wasio Waislamu juu ya Uislamu,’ Dk Zakir Naik, Mkurugenzi wa Peace TV ameorodhesha madhara kadhaa ya pombe na kwa mtazamo wangu wanywa viroba huyapata zaidi.

Dk Naik ambaye ni daktari wa magonjwa ya binadamu anasema katika ubongo wa binadamu, kuna eneo linalomdhibiti au kumzuia mtu kufanya jambo ambalo linaaminika kuwa baya au kosa katika jamii (inhibitory centre).

Mlevi wa viroba (bila shaka hata pombe nyingine) akishalewa, eneo la ubongo la kudhibiti tabia linakuwa lenyewe pia limedhibitiwa na pombe na ndio maana anaweza kutukana, kukojoa hadharani na kadhalika.

Hawa tunawashuhudia sana uswahilini wakishalewa viroba. Dk Naik pia anazungumzia tatizo la zinaa, ubakaji na VVU. Anasema kwa mujibu wa Idara ya Makosa ya Jinai ya Marekani, mwaka 1996 peke yake iliorodhesha wastani wa makosa 2,713 ya ubakaji uliokuwa ukitokea kila siku nchini humo.

Taarifa za kitengo hicho zilisema kwamba wengi waliohusika na vitendo vya ubakaji ni walevi na kwamba walevi wengi pia walihusika katika kubaka watoto wao, mama au dada zao.

Dk Zakir pia anasema sababu mojawapo ya kusambaa kwa maambukizi ya virusi vya vinavyosababisha ugonjwa wa Ukimwi katika maeneo mengi duniani ikiwemo India ni pombe. Dk Zakir ni raia wa India.

Dk Naik anasema ‘mla’ viroba huweza kumtaka mapenzi yeyote huku akiwa hakumbuki pia kutumia kondomu. Anasema kuna orodha ndefu ya magonjwa yanayohusishwa au ambayo asili yake ni pombe ikiwa ni pamoja na ugonjwa wa ini uitwao Cirrhosis, saratani ya koo, saratani ya kichwa na shingo pamoja na saratani ya ini (Hepatoma).

Pombe pia huweza kusababisha saratani ya matumbo. Magonjwa yanayohusiana na moyo kama Cardiomyopathy, Hypertension, Coronary Artherosclerosis, Angina (ugonjwa wa moyo unaosababisha maumivu kifuani) na shinikizo la damu chanzo chake pia kinaweza kuwa pombe kwa mujibu wa Dk Naik.

Anasema magonjwa yanayohusu kupooza (kiharusi) na kisukari pia wakati mwingine huhusishwa na pombe. Lakini eneo lingine ambalo wengi wameligusia sana na mimi katika makala haya nimelifanya la mwisho ni viroba kuwa chanzo cha ajali.

Ajali nyingi za barabarani zinazosababisha vifo na ulemavu pamoja na uharibifu wa mali zinatokana na matumizi ya pombe na viroba vinanyooshewa sana kidole.

Binafsi, nimeshuhudia vijana kadhaa wanaoendesha bodaboda wakiwa wananyonya viroba kwenye duka hilo la jirani na ndio maana siku hizi nawaza sana ninapolazimika kupanda bodaboda kwa sababu naamini kuna asilimia kubwa ya waendesha bodaboda wanaokunywa viroba tangu asubuhi kama nilivyoeleza hapo juu.

Mtu anapozungumzia hasara ya mkopo wa mtengeneza viroba, anaweza pia kueleza ni hasara kiasi gani taifa linapata kutokana na vifo au kutibu watu wanaovunjika viungo kwa ajali zinazosababishwa na pombe za viroba? Mbali na viroba kusababisha uchafuzi wa mazingira, lakini kubwa ninalotaka kumalizia makala hii ni ukweli kwamba siku hizi baadhi ya madaktari wameamua kuwa huru kusema wazi kuwa ulevi wa pombe ni ugonjwa kamili na siyo kama walivyokuwa wakisema zamani kuwa ni mtu ‘kutawaliwa’ au kuwa na uraibu (addiction).

Kama ndivyo, basi ni afadhali tupunguze ugonjwa huu unaouzwa kwenye viroba, kila sehemu na kila wakati hadi kwa watoto wetu kuliko kuuacha ukizidi kuharibu jamii. Naamini hatua hii ya kupiga marufuku pombe za viroba kuanzia kesho ni ya kuungwa mkono sana na kwa kweli imekuja ikiwa imechelewa kwani madhara ambayo viroba vimeshasababisha katika jamii kama mtu atafanya utafiti, nadharia yangu inaonesha kuwa ni makubwa. Na Hamisi Kibari TUKUBALIANE KUTOKUBALIANA Hali ikiwa