POROJO ZA ANKO SAGATI:Maige na utamu wa uwaziri
- Imeandikwa tarehe 02 Juni 2012
- By Shadrack Sagati
- Imesomwa mara: 1724
U WAZIRI mtamu bwana asikwambie mtu. Ndio maana mbunge anaponyang’anywa wadhifa huo hata kama atakuwa na mamilioni ya ubunge lakini afya yake ni lazima iyumbe.
Tumewahi kuwaona mawaziri waliopigwa chini namna wanavyotembea barabara wakizungumza peke yao. Ule ufalme wa kuhudumiwa kuanzia ofisini hadi nyumbani unakoma.
Gari la bure kila siku linawekwa mafuta huku huduma kibao unapewa na Serikali kwa nini mtu aache kuchanganyiwa akinyang’anywa cheo hicho wakati bado alikuwa anakihusudu.
Hivyo msimshangae ndugu yangu wa Msalala ambaye baada ya kunyang’anywa tonge mdomoni amegeuka mtu wa kupiga mawe wabunge wenzake na viongozi wenzake ndani ya CCM.
Ni lazima achanganyikiwe maana kuongoza wizara yenye utajiri wa mali za asili ni jambo zito na kila mtu katika maisha yake anapenda afikie hatua hiyo.
Hiyo ndio hatua kubwa ya kimaisha hasa kwenye siasa achilia mbali kutembea na ving’ora. Maige alikuwa anaongoza hifadhi zaidi ya 10 zilizojaa utajiri.
Alikuwa anaongoza vitalu vya uwindaji ambavyo vina pesa mbaya, alikuwa anaongoza mapori tengefu ambayo yana pesa lukuki kutoka nje ya nchi. Kote huko ni pesa tu, tena wizara yenyewe ina ndege kibao za kusafiria mabosi na watalii.
Akitaka kwenda Serengeti hawezi kusafiri na basi ni ndege, akitaka kwenye Mikumi ndege ipo inamsubiri maana nani wa kupanda ndege hizo kama sio bosi wa wizara hiyo?
Halafu ghafla tu anaondolewa kwenye wizara hiyo tena kabla hata hajajiandaa. Alienda Dodoma akijua hilo halipo, lakini anatoka huko akiwa miongoni mwa mawaziri wanaotakiwa kung’oka.
Akapiga kelele kujitetea, wapi Rais akaridhika na tuhuma dhidi yake na akakubali kumwondoa kwenye huo ulaji. Hapo ulitaka yeye afanye nini kama sio kumbwatukia kila mtu anayekuja mbele yake.
Hao ndio aina ya mawaziri tulionao bwana! Hawaoni kama cheo ni dhamana. Anadhani yeye amezaliwa na cheo hicho na ndiye pakee anastahili kukaa pale na sio mtu mwingine. Anasahau kuwa kabla yake alikuwapo mtu na sasa hivi hayupo.
Ya nini sasa wewe Maige unajiona msafi ambaye ni wewe pekee ulifaa kuongoza wizara hiyo? Ngoja wengine wajaribu nao wakishindwa wataondolewa kama wewe.
Hivyo kutapatapa kwako huku mara umvae Lembeli na Kamati yake ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, hutujakaa sawa mara umerusha dongo kwa Halmashauri ya CCM kuwa kwa nini haikukuita kukuhoji juu ya tuhuma hizo.
Bado haitoshi umeendelea kuwatupia lawama viongozi wako. Sasa umemvaa hadi bosi wako wa chama Nape sasa unamwita gamba sugu linalotakiwa kuondolewa kwenye chama.
Jamani hilo gamba leo hii Maige ameliona wakati hayuko kwenye uwaziri. Mbona hakuwahi kulisema hilo huko nyuma. Mara tumsikie akiahidi kuwasha moto bungeni, hilo ni jukumu lake hana haja ya kutangaza kwenye midia.
Ni kweli uwaziri ni mtamu, ngoja Maige aweweseke maana kanyang’anywa tonge mdomoni wakati bado anahitaji kujipanga. Pole Maige ndio siasa hiyo, lakini punguza kuweweseka.


