Mfumo wa elimu unazidisha umasikini
- Imeandikwa tarehe 10 Juni 2012
- By Basil Msongo
- Imesomwa mara: 1419
SEMENI waungwana, mambo vipi, kuna jipya gani hapo, bila shaka mambo si mabaya, kwa mnaojinafasi poleni kwa starehe, mlio na shida, ombeni mtapewa, tafuteni mtapata, mkikosa msikate tamaa.
Namshukuru Mungu kwa ninachokipata, nazidi kutafuta nisivyonavyo, na ikiwezekana, vilivyopo viongezeke ili litimie lile neno kwamba, hakuumbwa kutaabika bali kuyafurahia maisha. Usishangae wala kuhoji hilo neno lipo kwenye kitabu kipi , huo ni mtazamo wangu, maisha bora kwangu na kwako yanawezekana, shida zinavumilika lakini umasikini haukubaliki.
Poleni vijana mnaotaabika popote ulipo, naamini ninyi ni wengi kuliko wale ‘mambo safi’, msijichukie, msiyachukie maisha, jipeni moyo kwamba ipo siku na ninyi hamtajiuliza mtapata vipi fedha, mtatafuta namna ya kuzitumia.
Jipangeni, maisha si lelemama, Tanzania ndiyo hii, hapa ndiyo kwenu, Taifa linawategemea, msibweteke au kukata tamaa, tambueni nafasi yenu hapo mlipo, na kwa nchi yenu, timizeni wajibu wenu, kwa kuwa wale wameweza, na ninyi mnaweza.
Serikali nayo itimize wajibu wake kwa vijana hasa ili kuwawezesha kumaliza umasikini unaowakabili. Huu si muda wa porojo au kutoa ahadi zisizotekelezeka, tunahitaji majibu ya dhati ili kutatua kero husika kwa wakati mwafaka.
Vijana hawahitaji majibu ya kuwafurahisha au kuwapa moyo, wao na Watanzania kwa ujumla wameshaelezwa mambo mengi ya kuwapa moyo, sasa wanataka mikakati inayotekelezeka kwa kuwashirikisha wao ili kumaliza matatizo yanayowakabili na si utendaji wa mazoea na fikra zisizoendana na kasi ya mabadiliko ya dunia ya leo.
Kwa mfano, mfumo wa elimu yetu ni chimbuko la tatizo la umasikini kwa vijana wengi nchini, kama Tanzania itaendelea na mfumo huu, kundi hili na Watanzania kwa ujumla wataendelea kuwa masikini, tunahitaji kuunda tume ili kulibaini hili? Au tunahitaji fedha za kigeni?
Mfumo wa elimu Tanzania unawajengea wahitimu msingi imara wa kuajiriwa, lakini viongozi wa Serikali wanawahamasisha wajiajiri. Nina mashaka na dhamira za viongozi wa nchi hii kwa kuwa wanasema wasichopaswa kukisema, na hawasemi wanachotakiwa kukizungumza, aidha kwa bahati mbaya au makusudi .
Siamini kama ni kweli wanaipenda Tanzania kama wanavyotushawishi tuamini, na kuna upendo basi huwa ni wa dharura. Huwezi kumaliza umasikini wa vijana kwa kuwapa mitaji au kuunda vikundi wakati hawafahamu namna bora ya kufanya biashara.
Ninaamini kwamba, Serikali inatambua kuwa, tatizo la msingi kwa vijana si mitaji, ni mfumo wa elimu, kwa kuwa hauendani na hali halisi ya dunia ya sasa. Vijana wanasema wapo kibiashara zaidi, lakini waulize kama wanazifahamu A, B, C za biashara.
Mfumo wa sasa uchumi ni wa kibepari, suala la biashara halikwepeki, mtaala wa elimu Tanzania umelizingatia hilo? Ni lini mtoto wa Tanzania ataanza kufundishwa biashara tangu akiwa shule ya msingi ili aweze kujiajiri akihitimu darasa la saba, sekondari au chuo?
Ni lini elimu ya biashara itaingizwa kwenye mitaala yote ya elimu kuanzia elimu ya msingi? Kuna mfumo wowote wa kuwawezesha wanaohitimu katika vyuo vya ufundi kupata mitaji? Siku njema.
This email address is being protected from spambots. You need JavaScript enabled to view it.



