Suluhisho la mapigano Kilosa lipatikane haraka

Hali ya mapambano kati wakulima na wafugaji katika wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro, halina budi kushughulikiwa kwa umakini unaostahiki kwa lengo la kudhibiti hali hiyo au kuitokomeza.

Tunafarijika kuona kwamba viongozi wa serikali, wapo wilayani humo katika kuendesha mikutano ya kutafuta suluhu ya amani kwa wakulima na wafugaji ili wananchi hao, waweze kuwa huru na kurejea katika hali zao za kawaida, kuendesha shughuli zao za kila siku, huku wakidhibiti wenzao wachache, wanaonekana kutaka kuleta kuendeleza mifarakano.

Baadhi ya viongozi hao, wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Stephen Kebwe na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba jana waliendesha mikutano katika wilaya hiyo ili kurejesha maelewano, baina ya pande hizo mbili, ambazo katika katika hali ya kawaida kila upande unamtegemea mwenzake katika maisha.

Hakuna ubishi kwamba hali ya kurejesha maridhiano, haina budi kusimamiwa kwa makini na kuhakikisha kwamba wale wote wanaotaka kuendeleaza hali hiyo ya mifarakano na kwenda kinyume cha maridhiano, wanachukuliwa hatua kali.

Ni vizuri wahusika katika migogoro hiyo, wakubaliana kutumia busara ili kufikia muafaka wa kuishi kwa amani na kutatua migogoro hiyo kwa maelewano na kuachana na kiburi cha kila upande, kushikilia msimamo na maslahi yake, hata kama yanaumiza upande mwingine.

Suala la mapambano, tena ya silaha, ni la kihalifu na zipo sheria ambapo wahusika katika hili, watakamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria, kama ilivyotokea kwa waliomjeruhi kwa kumrushia mkuki mdomoni na kutokea nyuma ya shingo mwananchi mmoja wilayani Kilosa, Augustino Mtitu na kisha watuhumiwa 12 kutiwa mbaroni na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria Tunashauri kwamba hali ya kishari ya aina hii, isipewe nafasi kuendelezwa, kwani siyo dalili nzuri kwa amani na usalama wa wakazi wa Kilosa na maeneo ya jirani.

Sote kwa umoja wetu, tupige vita kwa kila hali, kuielea hali hiyo katika jamii yetu. Kuna habari kwamba baadhi ya viongozi, wakulima na wafugaji, wanahusika kwa namna moja au nyingine katika kuchochea migogoro.

Sisi tunapongeza hatua zinazochukuliwa na serikali katika kukabiliana na hali hiyo. Tunataka wachochezi hao, wasakwe na wakibainika wachukuliwe hatua zinazostahiki.

Lakini pengine jambo la msingi na huenda ndilo linaweza likawa suluhisho la kuduma la migogoro hiyo wilayani humo ni kutekeleza uamuzi wa Baraza la Madiwani wa Kilosa la kuhakikisha kwamba kila upande, unaendesha shughuli zake katika maeneo waliyopangiwa, kwa maana kwamba wafugaji wafuge katika maeneio waliyotengewa na wakulinma nao walime maeneo yao waliyotengewa, bila kuingiliana bila sababu za msingi.

Hili likisimamiwa kwa umakini, migogoro hiyo itakwisha, siyo kwa Kilosa tu, bali hata maeneo mengine nchini, yenye mapambano baina ya wakulima na wafugaji. Viongozi wa serikali, wa kidini, kijamii na wananchi kwa ujumla wao, wajielekeza katika kufikia muafaka wa kupata ufumbuzi huo wa kudumu katika maeneo yenye migogoro hiyo.