Hospitali ya Mloganzila ifunguliwe haraka

KATIKA gazeti letu la jana kulikuwa na habari kuwa Taasisi ya Tiba na Mifupa Muhimbili (MOI), imeelemewa na majeruhi wa ajali na sasa inaomba hospitali zaidi ya nne, zijengwe katika jiji la Dar es Salaam.

Mkurugenzi wa Tiba wa Moi, Dk. Samuel Swai ndiye aliyetoa ombi hilo, alipohojiwa kuhusu majeruhi wanaopokelewa kwa siku katika taasisi hiyo.

Swai anaomba Serikali kuongeza uwezo katika hospitali za mkoa jijini Dar es Salaam, ambazo ni Temeke, Amana iliyopo Ilala na Mwananyamala wilayani Kinondoni; au kujenga taasisi nyingine nne kama MOI. Anasema hatua hiyo, itapunguza msongamano wa majeruhi wa ajali, wanaofika kutibiwa MOI, ambao kwa siku ni wastani wa wagonjwa 30.

Kati ya wastani wa wagonjwa 30 wanaofika MOI kwa siku, 20 hadi 25 wanahitaji upasuaji. Kati ya hao walioumia vichwa ndani ya ubongo ni watano hadi 10, waliobaki wameumia sehemu mbalimbali za mwili ikiwemo mifupa mirefu mikono, miguu, mifupa ya paja na nyonga.

Walioumia migongo ni wawili hadi watatu, na mmoja wao huwa amepoteza mawasiliano kwenye mikono na miguu au miguu peke yake. Kati ya majeruhi hao, wa bodaboda ni 10 hadi 15, ambapo kati ya hao huwa wameumia mno maeneo ya vichwa, migongo na miguu. Watoto wanaofikishwa hapo, wengi wao wamevunjika viwiko, mguu wa paja au mikono.

Tunaunga mkono ombi hilo la MOI, kwa kuzingatia hali ngumu waliyonayo katika kutoa huduma kwa wagonjwa. Mathalani, wanafanya kazi hiyo kwa saa 24 na kuna siku wanapokea wagonjwa kati ya 60 hadi 100 kama kuna ajali ya basi. Tatizo lingine la hospitali hiyo ni vifaa tiba, ambavyo ni shida na havipatikani kirahisi.

Vifaa hivyo ni lazima vitoke nje ya nchi, hasa vyuma vinavyowekwa kwenye pingili za miguu au mifupa mirefu. Changamoto nyingine ni uhaba wa damu pamoja na uwezo mdogo wa baadhi ya watu kulipia huduma.

Lakini, wakati MOI wakiomba zijengwe hospitali zingine nne kubwa, kuna hospitali mpya ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), iliyopo Mloganzila, Kibamba, wilaya ya Ubungo jijini Dar es Salaam. Ilielezwa mwaka jana kwamba ingefunguliwa rasmi na kuanza kutoa huduma mwezi huu, lakini hadi sasa haijaanza.

Hospitali hiyo iliyojengwa kisasa, kwa kutumia mifumo mbalimbali ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), itakuwa ya kwanza kutumia mfumo wa teknolojia, unaochukua vipimo kwa mtambo maalumu na kuwasilisha majibu kwa njia ya mtandao.

Kwa mujibu wa Makamu Mkuu wa MUHAS, Profesa Ephata Kaaya, hospitali hiyo, itatoa tiba ya magonjwa mbalimbali, yakiwemo moyo, saratani na figo na pia kufundisha wataalamu wa afya.

Tayari hospitali hiyo ya Mloganzila, imeshajengwa na kufungwa vifaa tiba vya kisasa vya digitali, vinavyotumia zaidi teknolojia ya Tehama, zikiwemo mashine za X-ray, MRI, CT-Scan, mashine maalumu kwa ajili ya kupimia magonjwa ya wanawake na mashine maalum za kupima na kutibu meno, koo, masikio na pua.

Tunaomba hospitali hiyo ya Mloganzila, ifunguliwe haraka na iwe na kitengo cha tiba ya mifupa, kitakachopunguza wagonjwa wanaokwenda MOI, hivyo kuokoa majeruhi wengi