Karibu Tanzania Waziri Wang Yi

Taarifa kwamba Waziri wa Mambo ya Nje wa China, Wang Yi anazuru Tanzania Jumatatu ijayo, zinaleta hamasa ya aina yake katika kuimarisha ushirikiano wa kihistoria, uliojengwa kwa miaka mingi baina ya nchi hizo mbili.

Tunapenda kumkaribisha kwa furaha Waziri huyo, kwa kuja kuwatembelea watanzania na kujionea mwenyewe jinsi wanavyopambana katika harakati za kujikwamua kutoka katika umasikini na kujiletea maendeleo endelevu na ustawi kwa taifa lao.

Tayari ziara hiyo inaonesha mwanga wa neema kwa watanzania, kufuatia kusudio la nchi hiyo la kutarajia kujenga viwanda takribani 200 kati ya sasa mwaka 2020; huku watanzania wapatao 200,000 wakitarajia kupata ajira.

Tunafarijika zaidi kwa kuona kwamba mpango huo, unaenda sambamba na Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa mwaka 2016/2020 na pia ahadi ya Rais John Magufuli ya kupania kujenga Tanzania ya viwanda.

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali na Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikano wa Afrika Mashariki, Mindi Kasiga aliwaeleza waandishi wa habari juu ya mpango wa ujenzi wa viwanda, hivyo alipokuwa akizungumzia ziara ya waziri huyo wa China jana.

Alisema Desemba 2015, kwenye mkutano wa wakuu wa nchi za Afrika na China, Tanzania ilichaguliwa kuwa miongoni mwa nchi nne barani Afrika zitakazowezeshwa kupiga hatua kwenye maendeleo ya viwanda.

Kwa mujibu wa Mindi, ipo miradi mingine ya miundombinu ambapo China imeahidi kuisaidia Tanzania, ikiwa ni pamoja na maboresho makubwa ya Reli ya Tazara, ujenzi wa bandari ya Bagamoyo na ujenzi wa Reli ya Kati.

Hakuna ubishi kwamba miradi na mipango hiyo, inayofanywa na nchi zetu mbili hizo, inatuelekeza katika kujenga ustawi wa kiuchumi na kijamii kwa wananchi wetu, tena kwa vitendo na hatuna budi kuhakikisha kwamba ushirikiano huo, hauvurungwi kwa hila zozote zile.

Udugu uliojengeka tangu enzi za Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na Mao Tse Tung, uliofikia hatua kubwa ya ujenzi wa Reli ya Tazara, uendelee kuimarishwa na kudumishwa kwa kila hali na wananchi wa nchi zetu zote mbili.

Waziri Wang Yi tunakukaribisha Tanzania kwa moyo mkunjufu na ujisikie uko nyumbani katika mikono salama ya wananchi wa Tanzania. Karibu sana.