Maandalizi Michezo Madola ianze mapema

MICHEZO ya 21 ya Jumuiya ya Madola itafanyika Gold Coast, Australia kuanzia Aprili 4 hadi 15 mwakani na tayari nchi zimeanza kujiandaa.

Wakati tukielekea katika michezo hiyo ya Jumuiya ya Madola, bado hatujasahau ushiriki wa Tanzania katika Michezo ya 31 ya Olimpiki iliyofanyika Rio de Janeiro nchini Brazil, ambako hatukufanya vizuri. Tanzania katika michezo hiyo ilipeleka timu za riadha na kuogelea tu huku washiriki wake wakiendelea kurudi mikono mitupu baada ya kufanya vibaya.

Ni kweli tulifanya vibaya na sababu kubwa ni kushindwa kuziandaa mapema na kitaalam timu zetu, ambazo zilishiriki michezo hiyo. Kifimbo cha Malkia kitatua nchini Aprili 8 mwaka huu na tayari Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) imeanza maandalizi kwa ajili ya kukipokea kifimbo hicho.

Kifimbo hicho ni ishara ya kuanza na kukaribia kabisa kufanyika kwa michezo ya Jumuiya ya Madola, ambayo huko nyuma ilikuwa ikishirikisha timu zilizotawaliwa na Uingereza. Bado hakuna Chama au Shirikisho la Michezo ambalo tayari limeanza maandalizi kwa ajili ya michezo hiuyo ya Jumuiya ya Madola na badala yake wanasubiri siku zikaribie, ndio wakurupuke na kuanza kusaka fedha za mazoezi.

Huko nyuma Tanzania ilifanya vizuri na hata kurudi na medali kutoka katika michezo hiyo ya Jumuiya ya Madola pale wachezaji wetu walipofanya vizuri katika michezo ya riadha na ndondi. Pia tuliweza kupeleka timu za baiskeli, kuogelea, judo na mingine, lakini michezo tuliyowahi kupata medali ni riadha na ndondi tu.

Michezo ya mwakani itakuwa tofauti kidogo kwani yenyewe itakuwa na viwango vya kushiriki tofauti na huko nyuma, ambapo wachezaji walipelekwa tu bila mradi kushiriki. Viongozi wa vyama vya michezo pamoja na mashirikisho ya michezo husika kuhakikisha wanakuwa na mipango madhubuti ya kuanzia kusaka fedha na hadi mazoezi ya timu zao ili ziweze kushiriki vizuri.

Kama viongozi wa michezo wataendelea kufanya vitu kimazoea, basi watarajie mawili, moja kushindwa kabisa kupeleka timu katika michezo hiyo au kuendelea kuvurunda. Kuanza kwa maandalizi ya ujio wa Kifimbo cha Malkia, ambacho hupokewa na kiongozi wa nchi kinapotembelea, kuwashtue viongozi wa michezo hapa nchini na kuanza maandalizi mapema.

Tanzania ilikuwa na rekodi nzuri katika Michezo ya Jumuiya ya Madola, kwani katika miaka ya nyuma tulikuwa tunarudi na medali mara kwa mara hasa katika mchezo wa riadha. Kwa upande wao, TOC wenyewe tayari wameanza maandalizi kwa ajili ya ujio wa Kifimbo cha Malkia wa Uingereza, hivyo na viongozi wa michezo muanze kuziandaa timu zenu mapema na kuacha kukurupuka.