Tukabili athari za jangwa kwa vitendo

MOJA ya matatizo makubwa yanayokabili nchi yetu kwa sasa ni uharibifu wa mazingira ;na watalamu wanasema asilimia 61 ya Tanzania, ipo hatarini kugeuka jangwa kutokana na uharibifu huo.

Kutokana na hali hiyo, tunaunga mkono kauli ambazo zimekuwa zikitolewa na Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira na Muungano, January Makamba katika ziara zake mikoani, ambako amekuwa akihimiza wananchi kushirikiana na serikali kukomesha uharifu huo.

Waziri huyo amekuwa akisema kuwa uharibifu wa mazingira, unatishia uhai na ustawi wa Tanzania kwa kila hali. Hata wakati akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha kwa Mwaka 2016/17 bungeni mjini Dodoma mwaka jana, January alisema kila mwaka nchi yetu inapoteza hekta 372,000 za misitu ambazo ni sawa na eka milioni moja.

Alisema kwamba katika kipindi cha miaka 10 iliyopita, Tanzania ilipoteza eneo la misitu lililolingana kwa ukubwa na nchi ya Rwanda. Hali hii inasikitisha na juhudi kubwa na za aina yake, zinatakiwa zifanyike ili kuweza kuikabilina nayo.

Kuna sababu nyingi zinazosababisha uharibifu wa mazingira na mojawapo ni mahitaji na matumizi ya nishati, ambayo yanaelezwa kuwa asilimia 90 yanategemea mazao ya misitu. Kiasi kikubwa cha nishati inayotumika nyumbani kwa ajili ya kupika chakula na matumizi mingine ni kuni.

Mathalani, jiji la Dar es Salaam pekee lenye watu zaidi milioni 5, hutumia magunia kati ya 200,000 hadi 300,000 ya mkaa kwa mwezi. Ni wazi kuwa kwa mwaka wakazi wa jiji hilo, wanatumia magunia mengi mno.

Mbali na kupongeza kauli za waziri huyo, tunapongeza pia serikali kwa kuandaa mkakati wa kitaifa wa miaka mitano wa upandaji na utunzaji miti, utakaogharimu Sh bilioni 105.2. Ni wazi kuwa mkakati huo, utakaohusisha watu wote katika vitongoji, vijiji, mitaa, kaya na taasisi, utapunguza tishio hilo.

Ni vizuri utekelezaji wa mkakati huo, uhamasishe wananchi watumie nishati mbadala ya kuni, kama vile umeme na gesi asilia. Miundombinu ya nishati hizo inazidi kusambazwa kwa wingi na serikali.

Nishati hizo mbadala zisambazwe kwa kasi kubwa mijini, vijijini pamoja na taasisi za serikali, kama vile shule za sekondari, vyuo vya elimu, vyuo vya ufundi, vituo vya afya, hospitali na magereza, kwa sababu baadhi ya taasisi hizo nazo hutumia kuni nyingi.

Aidha, kwa upande wa vijijini, Mradi wa Usambazaji Umeme Vijijini (REA) upewe kipaumbele kinachostahili ili kudhibiti matumizi ya mkaa, ambao ndiyo chanzo kikubwa cha kuteketeza misitu na kusababisha nchi kugeuka katika jangwa.

Tunaamini kwamba kama kutakuwa na uwekezaji mkubwa wa fedha na rasilimali kwenye nishati na kuhimiza nishati mbadala kwa matumizi ya majumbani, tutadhibiti uharibifu wa mazingira na kujiokoa na hali ya jangwa. Sote tushikamane katika hili.