Hii ndiyo serikali tunayoitaka

MWISHONI mwa wiki Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakati akiwa ziarani mkoa wa Ruvuma alitoa kauli nzito kwa waendeshaji wa Mgodi wa Ngaka, TANCOAL, akiwataka watimize masharti ya mkataba.

Kauli ya waziri mkuu kwa TANCOAL inadhirisha mwendelezo wa ufuatiliaji wa karibu wa serikali ya awamu ya tano wa mikataba mbalimbali inayogusa sekta ya madini. Ufuatiliaji huu wa karibu unaonesha dhamira ya serikali ya kufanikisha maisha ya watanzania kuwa bora zaidi kwa kusimamia kikamilifu raslimali za taifa.

Ikumbukwe kuwa katika mikutano mingi ya mabunge iliyopita, kelele kubwa ni mikataba ya madini mikataba ambayo pamoja na kuelezwa ni siri lakini ilikuwa inaonyesha kutosaidia wananchi kuondokana na umasikini.

Ndio maana gazeti hili linathubutu kutoa pongezi kwa Msimamizi wa serikali, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kwa kuonesha nini maana ya usimamizi wa karibu wa raslimali za taifa ili ziweze kuwasaidia watanzania wenyewe.

Hoja ya waziri Mkuu Kassim Majaliwa ya kuitaka kampuni ya TANCOAL Energy inayochimba makaa ya mawe kwenye mgodi wa Ngaka itimize masharti ya mkataba iliouingia na Serikali mwaka 2008, si hoja ya mchezo hasa ukiangalia maslahi yetu kupitia mali zetu kwenye miundombinu,umeme na gawio.

Kampuni ya TANCOAL ambayo iliundwa Aprili 3, 2008 na kampuni tanzu Intra Energy (T) Limited ambayo hisa zake ni asilimia 70 na Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) lenye asilimia 30 ya hisa; kutotekelezeka kwa vipengele vya mkataba huo vinatunyima miundombu ya kurahisisha usafiri na pia bei ya mkaa na umeme wa megawati 400 kutokana na makaa hayo.

Kwa mujibu wa mkataba huo, TANCOAL ilipaswa kugharamia dola za Marekani milioni 14.49 kwa ajili ya ujenzi wa barabara na madaraja ili kuwezesha malori makubwa na madogo yaweze kufika mgodini na kusomba makaa hayo.

Aidha kwa mujibu wa mkataba huo tena, TANCOAL ilipaswa kuwekeza mtaji wa Dola za Marekani milioni 82 lakini hadi sasa imewekeza kiasi cha dola milioni 14 ambazo ni sawa na asilimia 12 tu ya ahadi iliyotolewa.

Kutokana na maeneo yote kutotekelezwa kwa mujibu wa makubaliano yaliyoelezwa katika mkataba mwaka 2008 ni dhahiri kauli ya serikali ya kutaka maelezo ni sahihi, hatuwezi kwa miaka yote 9 kukaa watu na watu wanaovuna bila kupanda inavyostahili.

Tunaamini kauli ya Waziri Mkuu ya kutaka maelezo na pia maelekezo yake kwa Mwenyekiti wa Bodi ya NDC, Dk Samuel Nyantahe kuwa afuatilie kwa makini mambo yanayoendelea ndani ya shirika hilo, ni mwendelezo wa serikali ya awamu tano kuhakikisha maliasili za taifa hili zinasaidia kukabiliana na umaskini uliokithiri wa wananchi wake.

Kwa mara nyingine tena tunampongeza msimamizi wa serikali, waziri Mkuu majaliwa kwa kuonesha mfano wa ufuatiliaji na hasa alipotaka pia kuwapo na uwasilishaji wa mkataba huo kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili vipengele vinavyoibana NDC kiuendeshaji na kupata gawio viweze kuangaliwa upya.

Kwa namna hii ya ufuatiliaji, kila mtu atawajibika na hakutakuwa na longolongo katika matumizi ya raslimali zetu kwa manufaa yetu si kutajirisha matumbo ya wengine kwa kukosa maarifa, uzalendo na uthabiti wa ufuatiliaji.