Vyombo vya usafiri baharini viwekewe vifaa vya mawasilino

AJALI ya jahazi iliyokuwa inasafiri kutoka Tanga kwenda Pemba, imesababisha Watanzania wenzetu 12 kupoteza maisha na wengine 33 kujeruhiwa usiku wa juzi kuamkia jana; huku 25 kati yao wakiwa bado wanaendelea kupata matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Bombo, mkoani Tanga.

Tunapenda kuungana na Rais John Magufuli na watanzania wote, kuwapa pole wenzetu waliofikwa na msiba huo, kwa kuwapoteza wapendwa wao na wale walionusurika katika ajali hiyo, tunawatakia wapone haraka ili waweze kurejea katika shughuli zao za kawaida za kupambana na maisha.

Tunafarijika kusikia kutoka kwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tanga, Benedict Wakulyamba kwamba jeshi lake kwa kushirikiana na majeshi ya Wanamaji, Zimamoto na Uokoaji pamoja na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanga kwamba wanaendeleza jitihada za kutafuta abiria wengine wa ajali hiyo kwa sababu idadi ya abiria walikuwemo katika chombo hicho kilichopata ajali, haijajulikana.

Taarifa ya Kamanda huyo pamoja na mambo mengine, zilieleza pia kwamba idadi kubwa ya vyombo vinavyosafirisha abiria kati ya Tanga na Pemba, havina mifumo rasmi ya utambuzi. Sambamba na hilo, alisema pia kuwa ndani ya vyombo hivyo, hakuna vifaa vya mawasiliano, ambavyo vingeweza kutumika kwa kufanya mawasiliano kati abiria waliomo ndani ya chombo na nchi kavu wakati wa ajali kama hizo.

Tungependa kutumia nafasi hii, kuwakumbusha wamiliki wa vyombo vya usafiri kati ya Tanga na Pemba, kulichukua suala la ukosefu wa vifaa vya mawasiliano kuwa ni changamoto, ambayo wanatakiwa kuishughulikia mara moja bila kufanya ajizi ili kujihakikishia uwepo wa vifaa hivyo muhimu katika boti zao.

Hakuna ubishi kwamba kama jahazi hilo lingekuwa na vifaa vya mawasiliano, huenda vyombo vinavyoshughulika na usalama baharini vilivyo nchi kavu wakati ajali hiyo inatokea majira ya usiku wa manane, kama ilivyoelezwa huenda abiria wangeweza kupata msaada wa kuwaokoa mapema zaidi na kupunguza hata idadi ya vifo.

Kutokana na umuhimu wa kuwepo kwa vifaa hivyo kwenye boti, tungependa kuvikumbusha vyombo vyenye dhamana ya usalama baharini wakiwemo polisi, kuhakikisha kwamba vifaa vya mawasiliano vinakuwemo ndani ya vyombo hivyo bila kufanya ajizi. Uwezo wa kulisimamia hilo upo na hakuna sababu kwa nini lisifanyike tena kwa umakini unaostahiki.

Kwa wale ambao watakuwa wakaidi wa kutekeleza hilo, basi sheria ichukue mkondo wake. Tungependa pia kuwakumbusha abiria wanaosafiri katika vyombo hivyo kuwa wa kwanza kujihakikishia kwamba vyombo vya mawasiliano vimo kabla ya kulipa nauli kwa ajili ya kujihakikishia wepesi wa kuita msaada pale ajali inapotokea, badala ya kusubiri huruma ya Mungu peke yake. Hili linawezekana abiria wakishikamana kwa pamoja kukataa hila yoyote ya kukosekana kwa vifaa vya mawasiliano kwenye boti. Hili linawezekana, tulisimamie.