Yadumu Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar

LEO ni miaka 53 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar yaliyorejesha heshima kwa kisiwa hicho mintarafu ubinadamu, haki na wajibu.

Pamoja na kuwapongeza wenzetu wa Zanzibar kwa kuadhimisha siku hiyo muhimu katika kalenda, tunapenda watu wote tujiulize kwa mara nyingine tena, nini chanzo cha mapinduzi hayo. Tunasema tujiulize kwa kuwa wengi wa waliozaliwa sasa huenda wanasahau historia ya visiwa vya Pemba na Zanzibar na kujikuta wakimeza historia ambayo si ya kweli na yenye udhalilishaji mkubwa kwa utu wa mwafrika.

Kujua sababu ya mapinduzi hayo matukufu ndio njia njema ya kuenzi maana yake na madhumuni na walio na kifua kujua maana halisi ya mapinduzi kwa siku za leo na kesho kwa kuangalia historia. Inatupasa tukumbuke kwamba sababu kubwa ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 hata kama wengine hawapendi kukubali, ni kudhalilishwa na kunyanyaswa kwa waafrika ambao ndio wenyeji wakazi wa visiwa hivyo.

Ni dhahiri watu wenye ngozi nyeupe na waarabu walijiona kwamba wao ndio mabwana wakubwa wakijigawia mamlaka na rasilimali za Zanzibar huku watu weusi wakiwa watumwa wa mazingira yanayowazunguka. Mapinduzi hayo yalifanyika baada ya njia za kawaida za kidemokrasia kushindwa kutokana na hila za mtawala wa kiarabu na watu wanaofanana nao.

Ikumbukwe kwamba mwaka 1963 katika uchaguzi Chama cha African Afro-Shirazi kilishinda kwa zaidi ya asilimia 54 ya kura zote na kutwaa viti 13 katika Baraza la Wawakilishi lakini kwa hila, wapinzani waliokuwa na asilimia 45 za kura na kwa pamoja viti 18 ndio walipewa serikali.

Kwa wanafuata historia watakumbuka kwamba kitendo cha mwaka 1963 kilikuwa ni sawa na kitendo walichofanyiwa waafrika mwaka 1961. Kitendo kile cha maudhi na kuzingatia mgogoro wa utengenezaji wa katiba ya Zanzibar mjini London wananchi wazawa wa Zanzibar ilibidi wapange utaratibu wa kuangusha serikali.

Huwezi kusonga mbele usipojua historia ndio maana tunasema kwamba kulikuwa na sababu za mapinduzi na sababu hizo ndizo zilizoweka serikali ya Mapinduzi na sababu hizo hizo ndizo zitakazofanya mapinduzi daima katika visiwa hivyo.

Sote tunaamini kwamba, mapinduzi haya yalileta faida kubwa kwa wananchi wa Zanzibar, faida ambayo imewafanya si tu kuwa na sauti katika rasilimali zao, bali pia kuwaondolea unyonge kwa kuwapatia maeneo ya kuishi na makonde ya kujitafutia riziki.

Kutokana na ukweli huo, mtu ambaye anapinga mapinduzi atakuwa na maslahi yake binafsi, maslahi ya watawala wa zamani ambao wamepokonywa tonge na kugawiwa kwa wananchi wengine. Pamoja na makovu ya mapinduzi wakati umefika kwa wananchi wa Zanzibar kuwa pamoja kuijenga Zanzibar yenye staha na ustawi mkubwa wa nchi na watu wake.

Tunaamini Wazanzibari wana nia ya dhati ya kujikwamua katika umaskini kwani kazi ya kwanza ya kujiondoa kwenye minyororo ya utumwa wa kikoloni kwa kupindua utawala wa sultani Januari 12, 1964 ilikuwa imefanyika kwa maslahi ya umma wanaokandamizwa.

Wakati ule wakiongozwa na Mzee Abeid Amaan Karume, Wazanzibari walifanikisha mapinduzi na kuwathibitishia Waarabu kwamba kulikuwa hakuna sababu ya kutawaliwa abadani na sasa chini ya uongozi wa Dk Mohamed Shein, ni lazima kuyafanikisha mapinduzi kwa kuwa pamoja na kuongeza uzalishaji mali. Mungu Ibariki Zanzibar.