Jiji lifanye haraka uamuzi wa matumizi ya shilingi bilioni 5.8

Daily HBL Jumamosi HBL Jumapili GAZETI hili jana liliandika habari yenye kichwa cha habari ‘Serikali yarejesha asilimia 49 za UDA’.

Kiasi hicho cha hisa, zilikuwa zinamilikiwa na serikali katika Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA), ambapo baada ya shirika hilo kubinafsishwa kwa kampuni ya Simon Group, kulizuka utata juu ya zilipo hisa hizo.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, George Simbachawene alifafanua katika taarifa yake kwamba utata ulishughulikiwa na serikali, kufanikiwa kurejesha asilimia 49 ya hisa zake na baada ya kuuza hisa hizo, halmashauri ya jiji la Dar es Salaam ililipwa Sh bilioni 5.8 na mwekezaji Simon Group.

Kwanza tungependa kuipongeza serikali kwa kushughulikia kwa umakini utata uliojitokeza hadi kufanikiwa kuzipata hisa zake. Lakini pili, jambo ambalo linatia wasiwasi wakazi wa Dar es Salaam na wananchi kwa ujumla wao ni mvutano uliopo kati ya jiji na manispaa, kutofikia muafaka wa matumizi ya fedha zilizopatikana yaani Sh bilioni 5.8.

Kwa mujibu wa taarifa ya Simbachawene kwa Rais John Magufuli juzi, alipokuwa anazindua rasmi Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka na miundombinu, alisema jiji na manispaa zinavutana juu ya matumizi ya fedha hizo. Alifafanua kwamba wengine wanataka kila manispaa ipewe mgawo wake huku wengine wakitaka wajenge vituo vitatu vya mabasi ya mikoani.

Hawajapata muafaka na bado wanaendelea kubishana. Tunaunga mkono Rais kwa kuwapatia muda wa siku tano viongozi wa jiji hilo kongwe, wawe wameamua watazitumia fedha hizo kwa miradi gani.

Sisi tunawashauri viongozi wa jiji, waketi na wataalamu wao ili wafikie suluhisho la busara katika kuchagua miradi itakayoleta mapato ya uhakika kwa jiji letu na wakazi wake bila kupoteza muda, badala ya kuendeleza malumbano.

Tunawaomba pia wasisubiri Rais awachagulie aina ya miradi, kwani wao wako katika hali nzuri zaidi katika kufanya maamuzi juu ya miradi yao ya kuwaletea maendeleo, kwani wao ndiyo wanalifahamu jiji lao kiutendaji na watendaji wake.

Hapa tungependa kuwakumbusha viongozi wa jiji kwamba wakati huu ni wa kuachana na tofauti zao za kisiasa na kiitikadi, kwa kushirikiana kufanya uamuzi utakaowaletea maendeleo endelevu wakazi wa jiji na serikali kwa ujumla, kwani kila mmoja wetu anahitaji maendeleo bila kujali itikadi za kisiasa na tofauti nyingine zozote.

Katika hili, viongozi wa jiji msipate kigugumizi kwa wale wanaopinga miradi ya maendeleo bila sababu za msingi, kwani wanaweza kushughulikiwa kwa mujibu wa sheria na taratibu. Miradi mingi imeshindwa kuanza kutekelezwa kutokana na kukosekana kwa fedha, lakini kwa hili jiji hawana sababu, kwani fedha zipo. Fanyeni uamuzi haraka fedha zitumike kuleta maendeleo endelevu.