TFF ipange ratiba ya FA mapema

MZOZO uliopo tangu mwishoni mwa wiki iliyopita ni malalamiko ya wadau wa soka kuhusu upangwaji na upanguliwaji wa ratiba za michuano mbalimbali iliyo chini ya Bodi ya Ligi Tanzania na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Kumekuwa na malalamiko ya mara kwa mara kuhusu upanguwaji wa ratiba ya Ligi Kuu, na tangu michuano ya Kombe la Shirikisho (FA) ianze, mtindo huo umekuwa ukiendelea.

Wiki iliyopita, TFF ilitangaza mabadiliko ya ratiba ya Ligi Kuu, ambapo mechi ya Simba na Yanga iliyokuwa ichezwe Februari 18 mwaka huu, ikahamishwa mpaka Februari 25.

Mabadiliko hayo yamefanyika ili kupisha ushiriki wa michuano ya kimataifa kwa Yanga inayoshiriki Ligi ya Mabingwa Afrika.

Kidogo lilieleweka hilo ingawa tunaamini TFF walitakiwa kupanga ratiba zao mapema, kwani michuano ya CAF ilishajulikana tangu mwanzo kwamba itakuwepo na kwa mujibu wa kalenda ya michuano hiyo ni rahisi kufahamu tarehe za mechi, kwani karibu miaka yote huwa ni hizo hizo.

Baada ya mzozo wa ratiba hiyo ya Ligi Kuu, ukahamia kwenye michuano ya Kombe la FA. TFF ilitangaza ratiba hiyo kwa kushtukiza huku michuano ikijulikana na timu shiriki zikijulikana.

Ratiba ya mechi za mwishoni mwa wiki iliyopita ilitolewa huku timu nyingine zikiwa zimewapa mapumziko wachezaji wake na kuambiwa inatakiwa uwanjani baada ya siku mbili, hali iliyolazimika kuwarudisha wachezaji wake kwa maandalizi ya mechi hizo.

Baada ya malalamiko ya viongozi wa timu shiriki za kombe hilo, kauli ya TFF ilikuwa timu zote zilizokuwa zikilalamika, hazisafiri mechi zao zinachezwa kwenye mikoa yao, hiyo si sababu ya kitaalamu. Kwa wafuatilia masuala ya soka, hatuna shaka watakubaliana nasi kwamba ratiba hiyo ilikuwa ya kiubabaishaji.

Tunaamini kabisa, TFF inao uwezo wa kufuata upangwaji wa ratiba unaofanywa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kwenye michuano yake. CAF na duniani kote, ratiba hupangwa mwanzo wa msimu na kama ikibadilishwa ni kutokana na dharura ya hali ya juu kwelikweli, lakini si kwa TFF.

Michuano ya Kombe la Fa ni mikubwa lakini ratiba yake inapangwa kama michuano ya Kombe la Mbuzi, hilo haliwezekani. Sasa raundi ya tano ya michuano ya FA imemalizika na tayari timu zilizosonga mbele zimeshajulikana, ni imani yetu ratiba itapangwa mapema na kuondoa usumbufu uliojitokeza wakati huu kwa klabu shiriki.