Hongera TADB kwa kufikiria kilimo kisichosubiri mvua

BENKI ya Kilimo Tanzania (TADB) imesema kukosekana kwa mvua za uhakika ni moja ya changamoto katika utoaji wa mikopo kwa wakulima wadogo ambao wengi wanalima kwa kutegemea mvua.

Pamoja na kusema hivyo benki hiyo pia imetoa kauli nyingine kwamba kutokana na mabadiliko ya tabianchi ambayo yamechangia kukosekana kwa mvua, benki hiyo imejipanga kuwakopesha wakulima ili waweze kununua vifaa vya umwagiliaji, hivyo wao kupata chakula na taifa kuwa na chakula cha kutosha.

Sisi tukijua mazingira tata yanayokabili taifa hasa katika kuhakikisha inajitosheleza kwa chakula, Benki kwa kutambua adha inayowakumba Watanzania wanaolisha mamilioni, fikira yao mpya ni ya kuungwa mkono na kupongezwa.

Tunasema ni hatua ya kupongeza kwa kuamini kwamba kauli hiyo iliyotolewa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Francis Assenga imelenga hasa kuondokana na kilimo cha kutegemea mvua, kilimo ambacho kwa sasa kinatia shaka maisha ya kawaida ya watanzania kutokana na mabadiliko makubwa katika uwingi wa mvua na msimu wa mvua.

Kwa kuzingatia kwamba benki hiyo ni benki ya kusaidia kilimo, inafaa ichukue hatua haraka za kutambua haja ya wakulima wadogo ili kuwabadili wao kutegemea zaidi maji yaliyo katika hifadhi ya dunia na hivyo kutengeneza ukijani mpya utakaosaidia kulisha taifa.

Inafaa ikumbukwe kwamba chakula nchini Tanzania hakitegemei wakulima wakubwa, kinategemea zaidi mkusanyiko wa wakulima wadogo na faida ya ziada wanayopata katika maisha yao ya kilimo.

Pamoja na benki hiyo kuweza kukopesha wakulima hadi kufikia Desemba, mwaka jana Sh bilioni 6.5 kutoka Sh bilioni moja kwa ajili ya kuboresha kilimo, fikira ya sasa ya kuwezesha wakulima wadogo kuwa na mfumo imara na thabiti wa kunyweshea mazao na hivyo kuacha kutegemea mvua ni hatua inayostahili kuungwa mkono na wadau wote.

Tunasema na wadau wote kwa sababu ili kilimo cha umwagiliaji kifanikiwe kuna watu wengi wanatakiw akusghiriki kuanzia watafutaji wa maji chini ya ardhi, wachimbaji, na wasambazaji wa maji katika maeneo husika ambapo wakulima wadogo hao wana mashamba yao.

Hapa si tu wataalamu wa ugani wanaotakiwa kutoa msaada bali na wataalamu wa teknolojia ya umwagiliaji pamoja na mashine husika. Ndio kusema wakati umefika kwa Benki kukamilisha masuala muhimu yanayohusu mfumo wa mkopo kwa ajili ya kuendesha kilimo kisichotegemea mvua, lakini pia wakati wanafanya hivyo wanahitaji kutoa elimu ya kutosha ya namna ya kukopa fedha hizo ili kuinua kilimo.

Ni dhahiri kuna changamoto ya uelewa wa taratibu za kibenki kwa viongozi wa vyama vya wakulima wadogo pamoja na wanachama wanufaikaji, hali ambayo isiporekebishwa hata ukija mfumo huo ambao utasaidia wasitegemee mvua utakuwa hauna maana.

Na hakika benki ikizingatia yote hayo wataweza kuwaondoa wakulima wetu wadogo kutoka kilimo cha kutegemea mvua na kuifanya sekta ya kilimo kuwa zaidi ya kujikimu , tukijitoisheleza kwa chakula na pia kuinua upatikanaji wa mali ghafi kwa ajili ya viwanda vyetu.