Mamlaka zote za maji mijini zikaguliwe

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amehitimisha ziara yake katika mkoa wa Njombe juzi kwa mafanikio makubwa. Katika ziara hiyo, alihutubia mikutano ya hadhara, alikagua miradi mbalimbali ya maendeleo na kutoa maagizo kwa viongozi wa serikali kuondoa kero mbalimbali za wananchi.

Akizungumza na wananchi katika mkutano kwenye viwanja vya Shule ya Sekondari Mpechi katika Halmashauri ya Mji wa Njombe, Majaliwa aagiza Mamlaka ya Maji ya Mji wa Njombe (Njuwasa) kukaguliwa.

Alimwagiza Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Christopher Ole Sendeka kuwapeleka wakaguzi wa hesabu, kukagua mapato na matumizi ya Njuwasa.

Tunapongeza agizo hilo la Waziri Mkuu, ambaye alisema wakaguzi hao, mbali na kukagua mapato na matumizi ya mamlaka hiyo, pia waangalie kama wananchi walihusishwa katika ukokotoaji wa gharama za malipo ya ankara za maji.

Tunatambua kuwa Majaliwa alilazimika kutoa agizo hilo, baada ya wananchi kuilalamikia mamlaka hiyo kupitia mabango, waliyomuonesha kwamba wanatozwa ankara kubwa ya maji, lakini huduma hiyo inapatikana kwa kusuasua katika mji huo.

Suala hilo lilibainika zaidi, baada ya Waziri Mkuu kumtaka Mkurugenzi Mtendaji wa Njuwasa, Daudi Majani kutoa ufafanuzi juu ya suala hilo, ambapo Majani alisema kwa mwezi wanakusanya Sh milioni 75, zinazotumika kuendesha na kuboresha huduma.

Ndipo Waziri Mkuu akasema, “maji hakuna, unasema unaboresha, unaboresha huduma gani? Wananchi wanalalamika maji hakuna na mnawatoza gharama kubwa, Mkuu wa Mkoa kesho peleka wakaguzi, wakakague kwa mwezi anakusanya kiasi gani na anafanyia nini.”

Ni wazi kuwa hali hiyo, ya Mamlaka ya Maji ya Mji wa Njombe kudai kuwa inaboresha huduma wakati wananchi wanalalamika hakuna maji, haipo Njombe tu, bali ipo katika miji mingine pia nchini.

Kwa ujumla, mamlaka nyingi za maji mijini zimeshindwa kuboresha huduma hiyo na kila siku watu wanahangaika kupata bidhaa hiyo nyeti. Hata miji michache ambako kuna maji, yanapatikana kwa kusuasua.

Mathalani, katika jiji la Dar es Salaam, kuna watu wengi wanatozwa ankara kubwa za maji, lakini huduma haipo; na kama ipo basi ni ya kusuasua.

Vile vile, maeneo mengi hayana huduma hiyo na haijulikani lini yatapata. Pia yapo maeneo yalishajengewa visima, lakini kwa sasa visima hivyo vimebaki sanamu, kwa sababu maji hayatoki.

Hata katika jiji la Arusha, kuna maeneo mengi hayana maji na bado wananchi wanapelekewa ankara.

Tatizo hilo lipo pia katika mji wa Shinyanga, ambako wananchi wamekuwa wakilipia ankara kubwa ya maji wakati hawapati maji.

Tunaomba wakaguzi wapelekwe katika mamlaka zote za maji mijini, wakakague mapato na matumizi ya mamlaka hizo na ankara za maji zinazotozwa.