Wageni wauza ardhi wasifumbiwe macho

KWA muda mrefu kumekuwa na tabia ya baadhi ya raia wa kigeni kuja nchini na kudai wao ni wawekezaji. Lakini, baadaye watu hao hujipatia ardhi ambayo baadaye huitumia kupata mikopo kutoka benki za hapa nchini.

Tunasisitiza kuwa mwekezaji yeyote anayekuja Tanzania ni sharti awe na mtaji, teknolojia na utaalamu wa kile anachotaka kufanya. Tunataka aache kutumia rasilimali zilizopo nchini kujipatia fedha.

Tunampongeza Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi aliyesema hivi karibuni kuwa wageni kama hao, watanyang’anywa ardhi hiyo na kutimuliwa.

Aidha, adhabu hiyo itolewe pia kwa wamiliki wa ardhi Wazungu, ambao wamekuwa wakiwauzia wageni wenzao ardhi walizopewa kuziendeleza kwa kilimo, ufugaji au uwekezaji mwingine wenye tija na badala yake kuyakalia maeneo hayo na baadaye kuyafanyia udalali.

Lukuvi alisema tayari serikali iko mbioni kutaifisha mashamba yasiyopungua kumi wilayani Babati mkoani Manyara na mengine kadhaa katika wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani kutoka kwa wageni, ambao ama wameshindwa kuyaendeleza, au wamebadilisha matumizi yake na hata wale walioamua kuyauza kwa wawekezaji wengine kinyemela.

Waziri huyo alisema hayo katika ziara ya kushtukiza aliyoifanya karibuni katika Ranchi ya Darakuta iliyopo kijiji cha Gijameda ndani ya Bonde la Kiiru wilayani Babati mkoani Manyara.

Tunampongeza Waziri Lukuvi kwa kufanya ziara za kushtukiza katika maeneo mbalimbali nchini kufahamu kero za masuala ya ardhi, zinazokabili wananchi na kuzishughulikia.

Tunaunga mkono ziara hizo, kwani kumekuwepo na malalamiko ya muda mrefu ya wananchi katika maeneo mbalimbali kuhusu wageni kumiliki maeneo makubwa ya ardhi na kutoyatumia, badala yake kuyauza kwa wageni wenzao.

Kwa hakika, ziara hizo za kushtukiza zimekuwa na manufaa makubwa kwa wananchi, kama vile kuwezesha migogoro ya ardhi kushughulikiwa papo hapo.

Kwa mfano, katika ranchi hiyo ya Darakuta, Lukuvi aliwaagiza wamiliki wake kulifanyia marekebisho makubwa eneo hilo wanalotumia kwa ufugaji wa kibiashara ili liwe na tija zaidi, ikiwamo kuongeza ajira kwa wananchi wa kawaida.

Ranchi hiyo inamilikiwa na wageni kutoka Uswisi.

Hata hivyo, shamba la Darakuta siyo miongoni mwa maeneo ambayo wizara ina mpango wa kuyarudisha kwa wananchi.

Halmashauri za wilaya zibanwe ili kutayarisha ripoti maalumu za masuala ya ardhi na kisha kupeleka ripoti hizo kwa Waziri Lukuvi.

Ripoti hizo zieleze majina ya mashamba makubwa, yanayomilikiwa na wawekezaji wakubwa, ikiwemo wageni. Hali hiyo itaiwezesha serikali kuchukua hatua kwa wageni madalali wa ardhi. Ni vyema hatua hizo, zichukuliwe haraka.