Hongera waliofaulu kidato cha 1V

MATOKEO ya mtihani wa kidato cha 1V uliofanyika Novemba mwaka jana yametangazwa na kuonesha kuwa watahiniwa 244,762 ambao ni asilimia zaidi ya 70 ya wanafunzi waliofanya mtihani huo, wamefaulu.

Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), Dk Charles Msonde alieleza wakati akitangaza matokeo hayo kwamba ufaulu huo ni ongezeko la asilimia 2.44.

Kwanza, tunapenda kuwapongeza wanafunzi wote waliofaulu vyema katika mitihani hiyo, ikiwa ni matokeo halisi ya umakini, nidhamu pamoja na usikivu walioufanya kutoka kwa yale waliyokuwa wanafundishwa na walimu, wazazi na walezi wao. Kwa maneno mengine watoto wetu hao wamevuna kile walichotarajia katika maandalizi yao ya mitihani ya kitaifa.

Tungependa pia kutoa pongezi maalumu kwa wanafunzi walioibuka kuwa wanafunzi bora, pia shule bora kitaifa kwa wote wasichana na wavulana kwani tunaamini hali ya ushindani baina ya shule mbalimbali zikiwemo za wasichana na wavulana ni muhimu katika kuhakikisha uwepo wa ubora wa kitaaluma.

Safari hii hali imekuwa ya kufurahisha zaidi baada ya kubaini kwamba mwanafunzi bora wa kwanza kitaifa ni mvulana, lakini wasichana nao wakatoa mwanafunzi wa pili kitaifa. Raha iliyoje kushuhudia ushindani huo mkali kati ya wanafunzi wetu wa kike na wa kiume.

Tungependa kuwakumbusha wanafunzi waliofaulu kwamba wamepata tiketi ya kuendelea na masomo yao ya kidato cha V na hivyo kuwa tayari kukabiliana vilivyo katika elimu ya ngazi hiyo.

Jambo la msingi ambalo hawana budi kulitambua na kulifanyia kazi ni kwamba kila hatua ya elimu atakayopanda katika maisha ya elimu huwa na ugumu wake na njia pekee ya kufanikiwa ni kuendelea kuwa na nidhamu na bidii ikiwa ni pamoja na kuwasikiliza walimu wao kujiweka katika hali nzuri ya kupata ufaulu unaohitajika katika ngazi husika.

Katika ngazi inayofuata ni vizuri wakatambua kwamba ndiyo ngazi ya daraja kwao kujiunga na vyuo vikuu na vyuo vingine vya kati iwapo watafaulu kwa madaraja yanayokubalika kitaaluma. Juhudi na nidhamu ziimarishwe kuwawezesha kuvuka vyema katika ngazi hiyo nyeti na muhimu katika maisha yao ya kusaka elimu.

Wahenga walisema elimu ni ufunguo wa maisha hawajakosea nao hawana budi kuendelea kuutafuta ufunguo huo muhimu maishani mwao. Tungependa pia kuwapa ushauri wanafunzi ambao katika matokeo hayo hawakufanya vizuri kwamba wayachukulie matokeo hayo kama changamoto ya kujifanyia tathmini na kusonga mbele katika kusaka elimu hiyo kupitia vyuo mbalimbali vya kati vikiwemo vyuo vya ufundi stadi hususani Veta kujifunza taaluma mbalimbali.

Hapa tunapenda kuwakumbusha kwamba kwa kupitia mafunzo ya Veta wanaweza kuendelea kupanda ngazi ya elimu na hatimaye kujiunga pia na vyuo vikuu. Jambo la msingi katika hili ni kuchukua hatua za kujiunga na vyuo hivi badala ya kukata tamaa kubaki nyumbani bila utaratibu wowote.