Simiyu changamkieni soko la kuuza mchele Zanzibar

GAZETI hili jana lilichapisha habari yenye kichwa cha habari cha ‘SMZ wataka tani 100,000 za mchele wa Simiyu.’

Hiyo ilikuwa ni kauli iliyotolewa na Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Balozi Amina Salum Ali katika ziara yake ya kikazi ya siku tatu mkoani Simiyu.

Mbali na bidhaa ya mchele, Waziri huyo alieleza kwamba Zanzibar wana mahitaji makubwa wa mazao ya dengu, choroko, mbaazi na alizeti na kwamba viwanda vingi vimekuwa vikikosa uzalishaji, kutokana na kukosa malighafi kama hizo huko Zanzibar.

Hakuna ubishi kwamba katika Tanzania Bara, siyo mkoa wa Simiyu peke yake, bali karibu mikoa yote imekuwa akipata taabu kupata soko la uhakika la bidhaa mbalimbali zinazotokana na kilimo, ikiwa ni pamoja na mchele na mazao hayo mengine yaliyotajwa.

Kwamba Waziri Amina ameleta ujumbe huu wa aina yake kwa wakulima wa mkoa wa Simiyu, tunapenda wananchi hususan wakulima wa mkoa huo, kuchukua nafasi hiyo ya soko la wazi la bidhaa hizo zinazohitajika na wananchi wenzetu wa upande mwingine wa Muungano kuwa ni fursa kubwa na haina budi kutumiwa kwa umakini unaostahili.

Kwamba soko la uhakika kwa mazao hayo sasa lipo, hakuna ubishi kwamba ni changamoto kubwa kwa wakulima wa Simiyu na mikoa mingine kuweza kujipanga kwa uhakika ili kutekeleza matakwa ya soko hilo kwa bidhaa hizo, ambazo zitawapatia wakulima hamasa ya kibiashara na kuwaletea kipato cha uhakika na ustawi katika maisha yao.

Katika hili, tunapenda kuwakumbusha viongozi wa mkoa wa Simiyu, wakiwemo wabunge, viongozi wa kata na vijiji, wakulima na wananchi kwa ujumla, kujipanga kwa kujiwekea mikakati ya makusudi ya kuzalisha mazao hayo yenye soko la uhakika Tanzania Visiwani.

Kwa hili, tunapenda kutoa pongezi kwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka kwa kusema kwa uhakika kwamba wananchi wa mkoa huo, wana uwezo wa kuzalisha kiasi hicho cha mchele kutokana na ukweli kwamba asilimia 90 wa wananchi wake ni wakulima na wafugaji.

Suala la msingi kama tulivyoeleza hapo awali ni kwa wananchi wajipange kulima kwa uhakika na kuzalisha kiasi hicho kinachohitajika na ziada, kwani wasiwasi wa kukosa soko sasa unaweza kuwa historia, kama kiu ya wenzetu wa Zanzibar ya kupata bidhaa hiyo na nyingine, itatimizwa kikamilifu.

Hakuna njia ya mkato, bali kinachotakiwa ni kujipanga kuchapa kazi ya uzalishaji mazao hayo ili kujikwamua kiuchumi na kujiletea maendeleo endelevu.

Wakati mkoa huo umeshapata nafasi hiyo ya soko, tunapenda kutoa mwito kwa mikoa mingine nayo isibaki kuwa watazamaji, bali nayo ijipange katika uzalishaji wa mazao hayo ili hata kama wenzao wa Simiyu watashindwa kukidhi haja ya soko hilo, basi nao washiriki katika kusafirisha bidhaa hizo kwenda Zanzibar.

Wakulima wetu wasisubiri, bali watekeleze kwa vitendo kwa kupata fursa hiyo. Kazi kwenu!