Mji wa Dodoma uboreshwe haraka

WIZARA ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo imetangaza kuwa imehamia rasmi mjini Dodoma kuanzia juzi.

Hatua hiyo imechukuliwa huku wizara nyingine zikiwa zinaendelea kufunga virago Dar es Salaam kuhamia katika mji huo, ambao ni makao makuu ya nchi.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa wizara hiyo, ofisi zao zimehamishwa kutoka jengo la PSPF Dar es Salaam kwenda Dodoma, mtaa wa Makole Uhindini, katika Jengo la LAPF ghorofa ya nane.

Tunapongeza mno hatua hiyo ya Wizara ya Habari, kwani imekuwa moja ya wizara za mwanzo, kutekeleza kwa vitendo agizo la Rais John Magufuli la kuhamia katika mji huo. Hatua hiyo ya wizara zote, zilizokwishahamia Dodoma, inaidhihirishia jamii na dunia kwa ujumla kuwa Serikali ya Awamu ya Tano inatekeleza kwa vitendo ahadi zake kwa wananchi.

Tumevutiwa na taarifa ya wizara hiyo ya habari, iliyoeleza kuwa baadhi ya shughuli za wizara hiyo, zitaendelea kutolewa jijini Dar es Saalam katika ofisi zetu zilizopo Uwanja wa Taifa na kwamba kuanzia sasa barua zote zitumwe kwa Katibu Mkuu Dodoma S.L.P 25.

Kwamba shughuli za Idara ya Habari (Maelezo) kwa sasa zitaendelea kutolewa pale pale ilipo ofisi hiyo katika mtaa wa Samora, Posta jijini Dar es Saam, hadi itakapotolewa taarifa nyingineyo.

Mbali na Wizara ya Habari, Wizara ya Katiba na Sheria nayo ilihamia rasmi katika ofisi zake mpya mjini Dodoma mwanzoni mwa wiki hii na Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, nayo itahamia huko wiki mbili zijazo.

Nayo Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi imesema awamu ya kwanza ya uhamisho, itahusisha watumishi 41 watakaohamia Dodoma kuanzia Februari 14 na 15, mwaka huu huku wengine 47 watahamia huko kati ya mwezi huu na Juni mwaka huu.

Kwa upande wake, Waziri wa Katiba na Sheria imezindua rasmi ofisi za wizara hiyo mjini Dodoma katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) na tayari watumishi 31 wa wizara hiyo wamehamia huko. Wizara nyingine iliyohamia Dodoma ni Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, iliyohamia huko wiki iliyopita.

Hatua hizo zote, za ofisi nyingi za serikali kuhamia huko kwawingi na kwa muda mfupi, maana yake ni kwamba Dodoma ndiyo mji unaopewa umuhimu mkubwa kitaifa kwa sasa, baada ya Dar es Salaam, ambalo ni jiji la kibiashara.

Hivyo ni dhahiri kuwa mji wa Dodoma, unatakiwa ufanyiwe mageuzi makubwa kwa sasa, hasa ya utoaji wa huduma za kibiashara na za kijamii, kwa sababu idadi ya watu inaongezeka ghafla; na pia kuna mahitaji makubwa wa ofisi na nyumba za makazi.

Tunaomba uongozi wa serikali mkoa wa Dodoma, kukabiliana na ongezeko hilo la watu, kwa kuboresha maradufu huduma mbalimbali, kwa mfano mabenki mengi yafungue matawi na pia zianzishwe shule nyingi za msingi na sekondari.

Hali kadhalika, mji huo usafishwe usiku na mchana na huduma za maji zipanuliwe kwa kasi. Masoko yaongezwe na wafanyabiashara wapeleke bidhaa nyingi huko, hasa vyakula.