Serengeti Boys iandaliwe vema Afcon 2019

MICHUANO ya Kombe la Mataifa Afrika ‘Afcon’ imemalizika mwishoni mwa wiki iliyopita mjini Libreville, Gabon ambapo Cameroon imetawazwa kuwa mabingwa mara tano wa taji hilo kubwa kwa ngzi ya kimataifa Afrika.

Sote ni mashahidi kwa namna Cameroon ilivyopambana na kutwaa ubingwa licha ya kutopewa nafasi ya kufanya hivyo tangu michuano hiyo ilipoanza.

Moja ya mambo ambayo yaliifanya Cameroon isipewe nafasi ya kutwaa ubingwa ni kikosi chake kuwa na wachezaji chipukizi wengi, tofauti na ilivyozoeleka kwenye michuano mingi ya nyuma hushirikisha kikosi chenye wachezaji wenye majina makubwa na wakongwe.

Lakini mbali na Cameroon, Senegal pia kikosi chake kilisheheni chipukizi wengi na wakongwe wachache. Lipo funzo kwa Shirikisho la soka Tanzania (TFF) linapaswa kulichukua wakati huu ikifanya maandalizi ya kushiriki michuano ijayo ya Afcon itakayofanyika miaka miwili ijayo, Cameroon 2019.

Tanzania kwa sasa ipo kwenye maandalizi ya kushiriki michuano ya Afrika kwa vijana wa chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys itakayofanyika Gabon Mei mwaka huu. Serengeti imepata nafasi hiyo baada ya kushinda rufaa yake iliyoikata kwa Shirikisho la soka Afrika (CAF) dhidi ya Congo Brazzavile iliyomtumia mchezaji mwenye umri mkubwa.

Kwa mujibu wa Rais wa TFF, Jamal Malinzi, Serengeti Boys inahitaji Sh bilioni moja ili ifanye maandalizi ya michuano hiyo. Tunavyoona, fedha hizo zikipatikana, zitumike ipasavyo kwenye kuandaa timu hiyo kushiriki fainali hizo za vijana, lakini pia ikiandaliwa kwa ajili ya Afcon ya wakubwa 2019.

Tunaamini kabisa ikiwekwa misingi imara, Serengeti ndiyo itakayoshiriki Afcon 2019 kama Taifa Stars na itafanya vizuri. Tunaamini miaka miwili inatosha kwa maandalizi hayo kwa timu ambayo imekuwa kwenye mashindano muda mrefu hivyo wachezaji wake watakuwa wameiva vya kutosha kupambana kwenye fainali za Cameroon.

Inawezekana kukichukua kikosi hicho na kuchanganya na wachezaji wachache wazoefu na kushiriki vizuri kwenye fainali hizo.

Wenzetu Cameroon wamefanya hivyo na matokeo yake wote tumeyashuhudia kwa mafanikio waliyoyapata. TFF huu ni wakati wenu kwa kushirikiana na serikali na kampuni mbalimbali kuweka mipango madhubuti kufikia malengo hayo. Kila lenye kheri Serengeti Boys.