Kauli za Askofu, Naibu Waziri zizingatiwe
- Imeandikwa tarehe 18 Septemba 2012
- By Mhariri
- Imesomwa mara: 502
WAKATI Askofu wa Kanisa la Anglikana jimbo la Ziwa Rukwa, Mathayo Kasagara akiwaombea wasimamizi wa mtihani wa Taifa wa darasa la saba ili kuepuka fedheha, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mlugo amewaonya wasimamizi hao dhidi ya vitendo vyovyote vitakavyosababisha fedheha hiyo.
Viongozi hao wawili wanataka mtihani huo unaotarajiwa kufanyika nchini kote kesho, usimamiwe kwa umakini mkubwa na kuhakikisha kwamba hakuna udanganyifu wa aina yoyote unaofanyika ukiwamo wa kupokea rushwa na kuvujisha mtihani huo.
Wamefanya hivyo wakizingatia kuwa Taifa limeshaingia katika aibu ya kuwa na watahiniwa wanaofaulu kwa udanganyifu na matokeo yake kuja kubainika baadaye kuwa hawana uwezo wa kimasomo kutokana na ama kuoneshwa majibu au kufanyiwa mtihani.
Kama alivyosema Askofu Kasagara, ni aibu kwa Taifa shule kufutiwa matokeo au kupitisha wanafunzi wasio na uwezo kimasomo kwa kuwa kuendekeza hivyo ni kuandaa viongozi mbumbumbu ambao wataliingiza Taifa katika kiza cha maendeleo.
Kwa upande wake, Mulugo alisema hatua kali zitachukuliwa dhidi ya msimamizi au mdau yeyote atakayeshiriki au kuhusika kwa namna yoyote katika udanganyifu huo ikiwa ni pamoja na kushushwa cheo au kufikishwa mahakamani na hatimaye kufungwa ikithibitika.
Nasi tunaunga mkono msimamo wa viongozi hao, tukiamini kwamba viongozi wajao wanapaswa kuwa na misingi bora kielimu ili kuweza kusimamia vema maendeleo ya nchi, kwani kinyume chake ni Taifa kuongozwa na watu wasio na nyuma wala mbele kitaaluma na matokeo yake ni maanguko.
Zimekuwapo tuhuma kwa baadhi ya wasimamizi kupokea rushwa kutoka kwa wamiliki wa baadhi ya shule, hususan za binafsi, ili kuwezesha ‘kupitishwa’ kwa wanafunzi wengi na kuonesha kuwa shule hizo zinafundisha vizuri ili kuvutia wateja wengi kwa lengo la kujipatia mapato yatokanayo na ada.
Lakini pia umekuwapo mchezo mchafu wa kuvujisha mtihani kwa wanafunzi ambao wamekuwa wakisaidiwa na walimu wao kuandaa majibu kwa ajili ya mtihani huo na siku ya kuufanya unakuwa rahisi kubandika majibu ambayo yalishafanyiwa kazi na matokeo yake ni wanafunzi hao kufaulu kwa kiwango cha juu.
Ufaulu huo mara nyingi umekuwa ni wa kupangwa, na matokeo yake huwa ni janga kwa Taifa na ndiyo sababu ya kugundulika kwa wanafunzi wanaoingia vidato vya kwanza huku wakiwa hawajui kusoma wala kuandika kwa kuwa huwa wameandikiwa mitihani na watu wengine.
Kesho tunatarajia wanafunzi wote 894,881 waliosajiliwa kufanya mtihani huo Mungu akijaalia waifanye vizuri, tukitarajia kuwa hakuna atakayejikuta katika tatizo la udanganyifu na hatimaye kufutiwa matokeo yake na kama itatokea, basi mhusika kwa maana ya mwanafunzi na aliyechangia hali hiyo wote wachukuliwe hatua.
Maombi ya Askofu Kasagara na onyo la Naibu Waziri Mulugo ni ishara, kwamba hakuna mtu aliye tayari kuona udanganyifu huo unaolitia Taifa aibu unatokea, hivyo ni jukumu la kila mmoja na kila upande kuzingatia hayo na kuhakikisha mtihani unafanyika kwa haki na kila mhusika anatimiza wajibu wake.
Watanzania walio wengi hawatarajii kushuhudia tena wanafunzi wakiingia hatua nyingine ya elimu huku wakiwa hawajui kusoma wala kuandika na wakiwa wamefanya mtihani wao wa darasa la saba na kuonekana wamefaulu; kama jinai itakuwa imefanyika, basi itendewe haki kupitia vyombo vya sheria.


