21Mei2013

 

Busara itumike kutatua kero za madaktari

JUZI madaktari chini ya uongozi wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), walikutana kujadili yatokanayo na vikao kati ya wajumbe wa madaktari hao na Serikali vilivyokuwa na lengo la kutatua kero zao.

Baada ya mkutano huo, Rais wa MAT, Dk Namala Mkopi, alinukuliwa na vyombo vya habari akidai kuwa wanatangaza mgogoro na Serikali kwa wiki mbili na baada ya hapo kama hawataridhika na hatua za Serikali, watatangaza mgomo.

Kimsingi kero kubwa walizokuwa wakilalamikia ni za kimaslahi zaidi na kuboreshewa mazingira ya kazi jambo ambalo kwa namna fulani limechangiwa na ugumu wa maisha ambao umekuwa ukikumba karibu kila fani kutokana na kupanda kwa gharama za maisha.

Tayari Serikali katika matamko yake wakati wa mgomo uliopita, iliweka wazi kuwa baadhi ya kero hizo zinapaswa kusubiri wakati wa Bajeti ya Serikali ili zitekelezwe katika bajeti ijayo.

Hata hivyo wakati kikao chenyewe cha bajeti kikitarajiwa kuanza kesho, tayari madaktari wamekutana na kuipa Serikali wiki mbili kutatua kero hizo na isipowaridhisha mgomo utangazwe katikati ya Bunge la Bajeti.

Tunajua kuwa madaktari wanazo hoja za msingi za kudai maslahi yao lakini tunashauri mbinu ya kudai, isitumie maumivu ya wagonjwa ambao wengi ni Watanzania masikini. Fani ya udaktari ni moja ya fani muhimu kwa Taifa na watumishi wake hawapaswi kugoma, bali kushughulikia kero zao kwa namna ambayo haitasababisha maafa kwa wagonjwa.

Tunawasihi madaktari kuweka uzalendo mbele wakitambua kuwa mgomo wa aina yoyote, unamuumiza zaidi Mtanzania wa hali ya chini ambaye hawezi kwenda hospitali binafsi kupata huduma.

Tunakumbuka machungu yaliyotokea kwa Watanzania masikini wakati wa migomo iliyopita, tunatarajia kuwa machungu yale yatakuwa funzo si kwa Serikali tu bali pia na madaktari ambao hata elimu waliyoipata, wengi wamesomeshwa na Serikali kwa kutumia kodi za Watanzania masikini.

Wakati umefika kwa viongozi wakiwemo wa kijamii na kisiasa, kuhakikisha kuwa jihudi za makusudi zinachukuliwa mapema kukabiliana na kero hiyo na kuepusha uwezekano wa kuibuka kwa mgomo mwingine.

Aidha, tunahadharisha kuepukwe ushabiki wa aina yoyote, hasa wa kisiasa katika suala hilo kwa kuwa madaktari si wanasiasa, ni watumishi wa Serikali na suala linalohusu uhai wa Mtanzania ni la kitaifa na wala si la kujitafutia umaarufu wa kisiasa.

Tunasema hivyo kwa kuwa kumekuwa na kawaida ya baadhi ya wanasiasa wetu kutumia mianya ya kero na mahangaiko ya Watanzania kwa manufaa yao zaidi kuliko kuwasaidia Watanzania.

Tunakemea mbinu hizo chafu za kisiasa ambazo kwa namna moja zinaweza kuingilia kati mchakato wa kukabiliana na kero hizo kwa kutia chumvi ili kuzidisha matatizo kwa Watanzania ili wao waonekane wakombozi wa Watanzania. Tunasisitiza busara zaidi itumike.