19Juni2013

 

Kila la heri Mkutano wa Nane wa Bunge

MKUTANO wa Nane wa Bunge unaanza leo mjini Dodoma ambapo wabunge na mawaziri pamoja na maofisa wengine waandamizi wa Serikali, watakutana kwa takriban miezi miwili kujadili masuala mbalimbali ya maendeleo ya nchi.

Mkutano huu huwa ndio mrefu kuliko mingine kwani unajumuisha kusomwa kwa taarifa ya uchumi wa nchi na hotuba ya bajeti ya nchi kwa kipindi kingine cha mwaka mmoja wa fedha.

Pamoja na mjadala huo, maswali mbalimbali yataulizwa na wabunge na kujibiwa na mawaziri na pengine kupata ufafanuzi kutoka kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, huku pia Waziri Mkuu akiulizwa maswali ya papo kwa hapo.

Ni matarajio ya Watanzania kwamba wawakilishi wao waliowachagua kuingia bungeni watawawakilisha ipasavyo kwa kuuliza maswali yanayogusa maslahi yao na hivyo kutazamia kero zao kutatuliwa.

Ni matumaini yetu pia kwamba mawaziri watakuwa na wakati mzuri wa kuelezea nini wanachokifanya katika kuwatatulia wananchi matatizo yao na hasa ikizingatiwa chekeche lililopita hivi karibuni katika Baraza la Mawaziri.

Inajulikana pia kwamba Kambi ya Upinzani nayo imejipanga barabara kuhakikisha inaibana Serikali katika masuala kadhaa, ambayo inaamini kwamba yanagusa wananchi na hivi kuhitaji msukumo wa kuyatekeleza.

Lakini pia kama ambavyo imekuwa kama ada ya Bunge hili, bila kujali tofauti za itikadi zao, wabunge watasimama pamoja katika kupinga masuala ambayo wanaamini hayana maslahi kwa wananchi na ambayo yanahatarisha ustawi wa Taifa.

Tunatanguliza pongezi zetu kwa wabunge watakaokuwa mstari wa mbele kufanya kile kinachoaminika kuwa ndicho kinachotakiwa na wananchi ambacho ni cha kuja na mipango ya kuwaletea maendeleo na si kujiletea wao.

Tunaamini pia kwamba mawaziri watakuja na bajeti za wizara zao zinazolenga katika kuwaletea wananchi maendeleo na tunadhani kazi kubwa ilifanywa na Kamati za Kudumu za Bunge katika kukosoa, kushauri na hata kukataa bajeti ambazo hazina maslahi kwa Taifa.

Kwa mwelekeo huo huo, tunaamini Watanzania katika Bajeti inayotarajiwa kusomwa Juni 14, kipaumbele kitakuwa katika kupunguzia wananchi ugumu wa maisha na kutoa mipango itakayowaletea nafuu na maendeleo.

Tunachukua fursa hii kuliombea Bunge mjadala mwema katika miezi hii miwili lakini pia tukiwatakia afya na siha njema wabunge wote ili waweze kufanya kazi yao kwa umakini na busara kubwa, lakini msisitizo ukiwa ni katika kumkomboa Mtanzania.

Hatutarajii wala kuombea matusi, kejeli na mapambano ambayo hayalengi kumsaidia Mtanzania bali yanalenga kujijenga kisiasa; kwani hilo si kipaumbele cha Watanzania wa leo ambao wameendelea kuteseka kwa kero mbalimbali.