Msimamo wa Ponda kwa sensa haufai
- Imeandikwa tarehe 13 Juni 2012
- By Mhariri
- Imesomwa mara: 1405
SERIKALI kupitia kwa Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), imekataa maombi ya mashehe ya kujumuisha kipengele cha dini katika dodoso zitakazotumika kuuliza maswali wakati wa Sensa ya Watu na Makazi.
Hatua hiyo imekuja baada ya mashehe hao wakiwakilishwa na Katibu Mkuu wa Shura ya Maimamu Tanzania, Shehe Ponda Issa Ponda, kuomba kipengele hicho kwa madai ya kutaka kuwa na uhakika na idadi ya watu wa dini mbalimbali nchini.
Hata hivyo, Mkurugenzi Mkuu wa NBS, Dk. Albina Chuwa alisema hilo halitawezekana, kwa sababu Serikali haipangi mipango yake kwa kutumia misingi ya itikadi za dini, kabila wala rangi na ndio msingi wa utulivu na amani iliyopo nchini hivi sasa.
Ponda kwa upande wake, akaona jibu la Dk Chuwa kama kikwazo kwa Waislamu na hivyo kutishia kuzuia waumini wa dini hiyo kushiriki sensa ambayo inatazamiwa kufanyika mwishoni mwa mwaka huu.
Sisi tunaungana mkono na Serikali, kwamba hapana sababu ya kujumuisha kipengele hicho katika sensa, kwa sababu kujua idadi ya Waislamu, Wakristo na Wapagani, hakuna mchango wowote wa maendeleo kwa Mtanzania.
Lakini suala la msingi ni kutaka kujua Watanzania wako wangapi na hivyo kujua pia jinsi ya kugawa huduma na pia kupanga mipango mbalimbali ya maendeleo kulingana na idadi ya watu waliomo nchini.
Masuala ya msingi kwa Mtanzania, ni kupambana na maadui watatu ambao ni umasikini, maradhi na ujinga, na ili kuwashinda, lazima idadi ijulikane ya ni wananchi wangapi wanahitaji huduma hizo.
Tunapingana na msimamo wa Shehe Ponda, kwamba kujua idadi ya Waislamu au Wakristo na Wapagani, sanasana kunaweza kuibua mgawanyiko wa ama Waislamu au Wakristo ni wengi kuliko wengine na hivyo kusababisha malalamiko.
Jambo la maana na la msingi ni kwa Watanzania kujitambua kuwa ni Watanzania na si ni wa kabila, dini au rangi fulani na hivyo huduma zitolewe sawa bila kuangalia asili, imani au rangi ya mtu.
Tunamsihi Shehe Ponda na wengine wenya msimamo kama wake, waachane nao na badala yake washiriki kikamilifu kuwaelimisha wananchi na hususan wafuasi wao wa kidini kuthamini na kupenda sensa na kujitokeza kuhesabiwa kwa kuzingatia misingi iliyopo.
Tusiendekeze ubaguzi wa kidini kwani mwishowe hautatusaidia zaidi ya kuchochea mgawanyiko na hatimaye vurugu za kidini ambazo hazina siha njema kwa Watanzania na hasa wapenda amani wa kweli.
Watanzania tukijisahau na kuanza kuhubiri utengano wa kidini na hasa kudhani kuwa dini hii ni bora na yenye haki kuliko nyingine kwa sababu ya wingi au uchache wa waamini wake, tutakuwa tunajichongea na hata kujichumia janga letu wenyewe.


