19Juni2013

 

Tujitolee damu kwa hiari wakati wote

LEO ni Siku ya Mchangia Damu Duniani, ambapo nchini maadhimisho ya kitaifa yanafanyika mkoani Kilimanjaro kwa kaulimbiu ya ‘Mchangia Damu ni Shujaa’. Ni siku ambayo ilibuniwa kwa ajii ya kumwenzi mchangiaji damu kwa hiari.

Siku hii pamoja na kuwaenzi wachangia damu duniani, lakini ni siku ya kutafakari na kuona umuhimu wa kuchangia damu kwa ajili ya akiba kwa wanaoihitaji, hususan wagonjwa na wale ambao wamekumbwa na matatizo ya ajali na kupoteza damu.

Ikumbukwe kuwa kumekuwa na majanga mengi duniani ambayo yanahitaji damu na hivyo ili ipatikane sharti wajitokeze watu kuchangia ili kusaidia wanaohitaji wanapokuwa matatizoni.

Lakini hata hivyo, si kila mtu anastahili kutoa damu kwa sababu kwanza afya ya mtoaji ndilo suala muhimu kabisa, huku pia uzito wa mtoaji ni suala ambalo linapewa kipaumbele ili mtoa damu asijeathirika anapojitolea.

Kwa mujibu wa wataalamu, mtu mwenye uzito wa chini ya kilo 50 hapaswi kuchangia damu, halikadhalika mwenye matatizo ya kisukari na shinikizo la damu na magonjwa mengine ambayo yanaambukiza.

Ni vema basi mtu asiye na matatizo kama hayo na mengine, akajitolea kuchangia damu ili kusaidia wale ambao wana mahitaji ya damu ili hatimaye kuokoa maisha yao kokote waliko.

Akinamama wamekuwa wakipatwa matatizo ya upungufu wa damu pindi wanapokuwa katika kipindi cha ujauzito na hata pale wanapojifungua, wengine hutokwa damu nyingi na hivyo kupungua mwilini na kuhitaji kuongezwa.

Ajali nyingi zimesababisha damu kumwagika, mapigano nayo yanasababisha damu kumwagika na hivyo kuhitaji damu ya kujitolea kwa hiari na damu kutumika na inayobaki kuwekwa katika akiba kwa ajili ya matumizi ya baadaye.

Ili kuweza kujitolea damu salama, tunapaswa kujikinga na uwezekano wa kupata maambukizi ya magonjwa mbalimbali na hasa ya zinaa ukiwamo Ukimwi, jambo linalosababisha damu ya mwathirika isiwe na faida yoyote kwa mhitaji.

Tunachukua fursa hii kuwapongeza watoa damu wote duniani na hasa nchini huku tukitambua kuwa leo mkoani Kilimanjaro, baadhi yao watatunukiwa vyeti vya kutambua mchango wao kwa jamii katika kujitolea damu.

Kwa kuwa leo pia kutakuwa na shughuli ya kujitolea damu katika viwanja vya Hindu Mandal mjini Moshi ambapo kiwango kinachotarajiwa ni lita 200, tunatoa mwito kwa wananchi kujitokeza katika viwanja hivyo na kujitolea damu kwa hiari, ili lengo hilo lifikiwe na ikiwezekana lizidi.

Hata hivyo, kujitolea leo damu isiwe mwisho wa kufanya hivyo, bali tuendelee kujitolea damu siku zote na wakati wowote, ili tuendelee kuwa na akiba ya damu kwa ajili ya kusaidia wanaoihitaji.