18Juni2013

 

Bajeti ni nzuri ila isimamiwe vizuri

JANA Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha wa 2012/13 iliwasilishwa bungeni na Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa mjini Dodoma ambayo sehemu yake kubwa ni inalenga kupunguza kama si kumaliza mfumuko wa bei.

Mipango mingi iliainishwa na Waziri ikiwa ni pamoja na kubainisha vyanzo zaidi vya mapato katika upandishaji wa bei za bidhaa mbalimbali ikiwa ni pamoja na vinywaji baridi, vikali pamoja na sigara na tumbaku ghafi.

Lakini pia katika hali ambayo haikuzoeleka nchini, Serikali ilitangaza kuanzishwa kwa kodi ya namba za magari ambapo kila mmiliki wa gari ambaye atataka kuandika jina lake badala ya namba, atatakiwa kulipia Sh milioni 5 kwa miaka mitatu.

Hiyo kama alivyosema Waziri Mgimwa, italiingizia Taifa mapato, kwani alisema kuna watu wanapenda kufanya hivyo lakini wamekuwa wanashindwa na huku wana fedha na watakuwa tayari kulipia kiasi hicho cha fedha na Serikali kupata fedha.

Pamoja na hayo, Dk Mgimwa alibainisha ongezeko la bei ya matumizi ya simu za mkononi ambapo zitakuwa sawa na zinazotumika katika mataifa mengine ya Afrika Mashariki ambapo alisisitiza kuwa hatua hiyo ni makubaliano ya nchi hizo.

Kwa hakika Bajeti hii inalenga kupunguza ugumu wa maisha huku ikiipa Serikali fedha nyingi ambazo zitatakiwa zitumike kwa malengo yaliyokusudiwa ya kutatua matatizo ya wananchi kwa kuwahudumia inavyotakiwa.

Katika kuzima kilio na malalamiko ya wasanii wa muziki na filamu nchini, sheria zitatungwa na taratibu zitawekwa za kuhakikisha kwamba kazi za wasanii hao haziibwi tena na maharamia, kwa lengo la kuhakikisha uasilia unatambuliwa na kila msanii anapata haki yake.

Kwa ujumla malengo ya bajeti hii ni kuboresha uzalishaji viwandani, kuboresha usafirishaji, huduma za afya, maendeleo ya mifugo na sekta za mawasiliano, ili kurahisisha mazingira ya kujiletea maendeleo mmoja mmoja na makundi ya wananchi.

Misamaha kadhaa imetolewa na Bajeti hiyo katika sekta mbalimbali kwa malengo ya kuhakikisha uzalishaji unafanyika kwa wakati na kwa utoshelevu ili kukabiliana na mahitaji ya msingi ya maisha ya binadamu.

Maeneo ya wagonjwa nayo yameainishwa kwa kutoa misamaha kwa vifaa vya tiba na uchunguzi ili viweze kupatikana kwa unafuu zaidi ili angalau kila maeneo ya tiba yanakuwa na vifaa husika kwa utoshelevu pia.

Baadhi ya bidhaa zinazozalishwa nchini zimepunguziwa ushuru na zile zitokazo nje kupandishiwa, mathalan juisi zinazotengenezwa nchini ambazo ushuru wake utakuwa Sh 8 kwa lita huku za nje zikiwa zimepanda na kuwa Sh 83 kwa lita.

Ingawa vinywaji vimepanda bei kama ambavyo imekuwa ikifanyika kila bajeti ya mwaka, lakini ni imani yetu kuwa kama Bajeti hii itasimamiwa vizuri na kwa umakini, ni wazi kuwa itapunguza mfumuko wa bei na kuwa mkombozi wa Mtanzania.

Isimamiwe vizuri ili wananchi wapate maendeleo.