Anza mwaka mpya kwa mikakati ya maendeleo

KATIKA sayansi ya mafanikio tumeelezwa kwamba yapo mambo mengi yanayohusika kutufikisha pale tunapotaka kuelekea na pia zipo njia tofauti zinazopendekezwa na wataalamu ikiwa ni pamoja na kupanga malengo unayotarajia kuyafikia.

Tunamshukuru Mungu kwa kutuwezesha kuumaliza salama mwaka 2016 na kubahatika kuingia mwaka 2017 kwa amani na utulivu. Katika sherehe za mwaka mpya wengi wetu tuliungana na ndugu na jamaa zetu kufurahia na kuukaribisha kwa shamrashamra mbalimbali huku wengine wakianza na mkesha wakiwa kwenye nyumba za ibada na wengine kwenye nyumba za starehe.

Jambo la msingi na la muhimu kukumbushana sasa ni kwamba sherehe na burudani hizo zimekwisha na tunatakiwa mapema kujiwekea mikakati ya malengo ya maendeleo yako kwa mwaka huu mpya. Naamini kabisa kila mtu ana mambo ambayo angependa kuyafanya, mambo ambayo yatamvusha kutoka hatua moja kwenda hatua nyingine kimaisha.

Kwa wale ambao wako katika ajira, je unataka mwaka huu uendeshe vipi katika harakati za kuongeza kipato chako halali nje ya mshahara wako wa kila mwisho wa mwezi? Inawezekana ungependa kununua kiwanja kwa ajili ya ujenzi wa nyumba yako ya kuishi au nyumba ya biashara.

Je umewahi kufikiria namna ya kupata fedha za kutekeleza adhma hiyo ya kujiletea maendeleo binafsi? Siku hizi zipo taasisi mbalimbali za fedha na benki mbalimbali za biashara ambazo ziko tayari kuwakopesha watu wenye malengo kama hayo niliyotaja hapo juu pamoja na mengine kwa ajili ya kujikwamua katika umasikini au kuongeza kipata zaidi ya kile unachopata katika ajira yako ya sasa au shughuli zako za ujasiliamali.

Hakuna njia ya mkato katika harakati za kusaka maendeleo endelevu nje ya kutumia fursa ya mikopo kupitia taasisi za fedha au benki mbalimbali ukizingatia kwamba mianya ya upatikanaji wa fedha kwa njia zisizoeleweka hazina nafasi katika Serikali ya Awamu ya Tano.

Ni wakati wa kila mmoja wetu kujifunza kwa kila hali matumizi bora ya taasisi hizo kwa lengo la kujiletea maendeleo endelevu. Ni vizuri kujukumbusha pia kwamba kwa wale wenye nafasi ya kujitafutia miradi ya aina hiyo, katika harakati hizo watakuwa wanatengeneza ajira ambazo katika hali ya kawaida zisingekuwepo.

Ningependa kusisitiza pia hapa suala la nidhamu katika usimaizi wa matumizi ya fedha za mradi utakazipata ili kukusaidia kuweza kufikia lengo la mradi husika. Kama ni maradi wa ujenzi wa nyumba ya kuishi au nyumba ya biashara basi fedha hizo ziende kweli katika utekelezaji wa mradi husika na siyo vinginvyo.

Tunatoa angalizo hilo kutokana na uzoefu kwamba wakopaji fedha katika benki na taasisi mbalimbali za fedha wakati mwingine hujisahao kwa kutumia fedha za mkopo kwa lengo lingine tofauti na awali.

Wengine hubadilisha mradi wa awali na kutekeleza mradi mwingine huku wengine hujitoa kabisa na kujitumbukiza katika suala la starehe baada ya kuona kwamba akaunti zao zina fedha za kutosha. Ni vizuri katika harakati za utafutaji hadi upatikanaji wa mkopo husika hakikisha unatekeleza yote kulingana na mradi uliokusudia.

Ndiyo maana hapo awali nileleza kwamba katika taasisi za fedha au benki zinazotoa mikopo kwa miradi mbalimbali huwa na wataalamu ambao kama mkopaji atawatumia vizuri katika kupata ushauri wa mradi wake, kuna kila uwezekano wa kufikia mafanikio katika lengo lake na pia namna bora ya kuweza kulipa mkopo wenyewe.

Mwaka mpya,mambo mapya na malengo mapya ya kujikwamua katika umasikini na kujiletea maendelea endelevu. Ni muhimu nikasisitiza kwamba hakuna kitu kizuri kisichokuwa na gharama zake hivyo ni wazi pia kwamba kujipatia kipato cha ziada katika kazi yako au biashara yako, huna budi pia kutumia gharama na mipango ya uhakika katika kupata miradi husika na kipatao cha ziada.

Msemo kwamba asiyefanyakazi asile unakwendana sawia na juhudi za uhalisia anazofanya binadamu katika kujikimu katika maisha yake ya kila siku. Inawezekana kama utajituma kwa kadiri uwezavyo kuboresha maisha yako ya sasa na mwaka mpya wa 2017.