Tunapouanza mwaka mpya, vyombo vya ulinzi vikabiliane na uhalifu

KWA kipindi cha nyuma, kumekuwepo na matukio ya mara kwa mara ya uhalifu yakiwemo ya uporaji, ujambazi na wizi wa kutumia silaha katika maeneo mbalimbali katika miji mikubwa nchini, hasa Dar es salaam.

Matukio hayo yamekuwa yakigharimu maisha ya watu pamoja na upotevu wa mali na hivyo kuchangia kurudisha nyuma maendeleo. Wakati mwingine matukio hayo yamekuwa yakisababisha baadhi ya watu kupoteza maisha.

Wakati uhalifu huo ukifanyika jeshi la polisi nalo limekuwa likijipanga na kutangaza hata katika baadhi ya vyombo vya habari kwamba limeimarisha ulinzi katika maeneo mbalimbali na hata sikukuu zilizopita tulitangaziwa kwamba ulinzi umeimarishwa.

Pamoja na hali hiyo na kwamba ndiyo tumeuanza mwaka, lakini juzi watu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi walipora fedha zinazosadikiwa kuwa zaidi ya sh milioni 25 katika makutano ya barabara za Mandela na Nyerere, eneo la Tazara, Dar es Salaam.

Fedha hizo zilikuwa zikipelekwa benki na gari aina ya Toyota Rav4 lenye namba za usajili T 455 DFN, mali ya kampuni ya kutengeneza mabati ya Sun Share. Uporaji huo ulifanyika wakati gari hilo likiwa kwenye foleni ya magari eneo hilo ambalo pia askari wa doria wametanda, huku wakionekana muda mwingi wakihangaika kukamata pikipiki zinazotokea eneo la Buguruni.

Eneo hilo pia huwa na askari wengi wakiwemo wa usalama barabarani na wengine wa doria ambao hukamata pikipiki. Najiuliza. Je, wale askari waliopo pale makutano ya barabara Tazara ni kwa ajili ya mapambo au wapo kikazi? Muda mwingi wamekuwa wakishughulika na bodaboda hawaoni kuwa kuna haja ya kufanya doria kwa magari yaliyosimama?

Ni vyema sasa Jeshi la polisi na vikosi vyake likajipanga upya na kutoa maagizo mapya kuhusu ulinzi wa raia na mali zao, kwani matukio kama haya hayafurahishi masikioni mwa watanzania, kuambiwa kuwa vyombo vya dola vimejipanga kuimarisha ulinzi halafu wakati huo huo uhalifu mkubwa kama huo unatokea katika maeneo waliyopo.

Matukio kama haya yanarudisha nyuma juhudi za maendeleo hasa katika kipindi hiki ambacho ni kigumu kiuchumi hasa kutokana na sababu mbalimbali na majukumu ambayo hukabili jamii ya watanzania walio wengi.

Nasema hivi kwa sababu kwa kawaida miezi hii watoto wengi ndiyo hurejea shule na wana mahitaji mengi yakiwemo madaftari, vitabu, sare za shule na ada na hivyo kuwafanya wazazi na walezi wengi hasa wenye kipato cha chini kuwa katika hali ngumu kiuchumi.

Hali hiii ndiyo pia husababisha uhalifu kuongezeka kwa kuwa watu wengi wana mahitaji ya fedha kulingana na majukumu yaliyopo. Kutokana na hali hiyo, ni vyema vyombo vyetu vya ulinzi na usalama kuongeza nguvu hasa katika kuimarisha ulinzi katika maeneo mbalimbali ya jiji na nje ya jiji ili kuondokana na kero ya uhalifu.

Tunaamini doria husaidia sana kama ikifanywa kwa weledi na huleta matokeo chanya katika maeneo husika. Pia nazishauri taasisi na kampuni zinazosafirisha fedha nyingi kuomba ulinzi wa polisi ili kuepukana na matatizo kama hayo ya uporaji wa fedha.

Polisi wamekuwa wakitoa matamko mara kadhaa ya kuwasihi wanaosafirisha fedha kusindikizwa, lakini bado kuna baadhi wamekuwa wakikaidi hili na mwisho wake kulalamika wanapoporwa fedha zao.

Aidha, waajiri wanapaswa kuwaangalia wafanyakazi wao kwa kuwa wengine siyo waadilifu na wakati mwingine huhusika katika mipanga matukio ya kihalifu.

Naamini kila mtu akisimama katika nafasi yake kwa uadilifu na kuonesha nidhamu, uhalifu utakoma na jiji litakuwa shwari na hivyo kumfanya kila mwananchi kufanya kazi zake za kumuingizia kipato kwa kujiamini.

Siku zote uhalifu hurudisha nyuma maendelo, hivyo chonde chonde Jeshi letu la polisi tunapouanza mwaka huu tuanze na nguvu mpya ya kuhakikisha tunakomesha tatizo hili ambalo ni adui kwa maendeleo yetu.