Tusisubiri madhara, Sheria ya kutembea na silaha za jadi ifutwe

AKIWA mkoani Morogoro juzi, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba alitoa agizo kwamba iwapo kutatokea tukio lolote la mkulima au mtu yoyote kuchomwa mkuki, mshale, mapanga, fimbo au sime, serikali itafuta sheria ya kutembea na silaha.

Kauli hiyo imetokana na ombi la Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk Stephen Kebwe aliyeiomba serikali kuifuta sheria hiyo kwa lengo la kupunguza vifo na majeruhi katika migogoro ya wakulima na wafugaji mkoani humo.

Tamko hilo limepokelewa kwa namna tofauti na wananchi kwa kuwa kumekuwa na ongezeko la biashara ya silaha hizo katika maeneo yanayotuzunguka na wengine kutembea navyo hadharani kama kinga yao.

Ni kweli kwamba sheria hii imetoa uhuru kwa tu yeyote kutembea na silaha na kumiliki silaha ya aina yoyote kwa lengo la kujilinda na wahalifu, wanyama wakali na hata wakati wa kuchunga mifugo, kwa upande wa wafugaji.

Kwa mfano, katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam hususani kwenye makutano ya barabara, wamachinga wengi wamekuwa wakitembeza silaha hizo kuziuza kwa watu mbalimbali wenye uhitaji na zimekuwa zikinunulika, kwani bila hivyo, wasingekuwa wanauza.

Miongoni mwa silaha hizo zinazouzwa ni pamoja na visu, sime na mapanga ambapo licha ya jeshi la polisi Kanda hiyo kukataza kufanyika kwa biashara hiyo, bado imekuwa ikiendelea kushamiri.

Ni dhahiri kuwa uuzwaji wa silaha hizo za jadi na kuruhusiwa kwa wananchi kutembea nazo hadharani, zinachangia majeraha na vifo pindi panapotokea tatizo fulani hususani kwa wakulima na wafugaji.

Hata hivyo, suala hili linahitaji uwanda mpana kwa ajili ya kulitafutia ufumbuzi kwa kuwa wafugaji wengi wa jamii ya kimasai wamekuwa wakitembea na sime kila mahali hata baada ya malisho na pindi wanapotofautina na wakulima, hujichukulia sheria mkononi kwa kuitumia ile silaha aliyonayo ambayo husababisha madhara.

Tangu miaka mingi iliyopita kumekuwa na madhara ya utumiaji wa silaha hizo, hivyo ifike mahali tuone madhara yatokanayo na sheria hiyo, licha ya kwamba ilitungwa na Bunge kwa nia njema.

Tunatambua kuwa kila silaha inayotumika ina kazi yake na sio kutumika kumdhuru mtu mwingine pasipo hatia yoyote, kwani ni kinyume na sheria ya nchi na mtu anayebainika kufanya hivyo huchukuliwa hatua za kisheria. Agizo hilo lisiishie midomoni badala yake litekelezwe kwa matendo bila ya kusubiri mtu kupata madhara ndipo hatua zichukuliwe.

Pamoja na kutoa tamko hilo, ingekuwa ni vyema zaidi Waziri Nchemba akawasilisha maombi hayo kwa mamlaka husika na kujadiliana kwa namna gani watakavyopata mbadala wa sheria hiyo kwa maana ya kuirekebisha au kuifuta kabisa, kwani madhara yake yamekuwa makubwa nchini.

Pia, naamini kurekebishwa au kufutwa kwa sheria ya kutembea na silaha kutasaidia watu kuwa na nidhamu na silaha hizo na hata biashara hiyo holela haitakuwepo, badala yake zitatumika kwa matumizi stahiki.

Nichukur fursa hii kumpongeza Waziri Nchemba kwa hatua hiyo pamoja na kuvibana vyombo vya dola na vya kisheria kuchukua hatua haraka kabla ya kusubiri wananchi kujichukulia sheria mikononi kwa kuwapa adhabu stahiki ili iwe funzo kwao.

Pia utekelezaji wa agizo hilo unapaswa kufanywa kwa ushirikiano kati ya serikali na wananchi ambao watawataja watu wanaotumia hovyo silaha zao za jadi kwa kusababisha madhara kwa wananchi wengine.